Tafuta

Askofu mkuu Nyaisonga: Siku ya Wagonjwa Duniani 2020: Changamoto ya Bima ya Afya Tanzania. Askofu mkuu Nyaisonga: Siku ya Wagonjwa Duniani 2020: Changamoto ya Bima ya Afya Tanzania. 

Askofu mkuu Nyaisonga: Changamoto ya Bima ya Afya, Tanzania!

Katika maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2020, Askofu mkuu Gervas Nyaisonga amewahimiza watanzania kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha afya yao kwa kujikatia Bima ya Afya. Ameishauri Serikali ya Tanzania kuchunguza changamoto zinazojitokeza ili kuzipatia ufumbuzi wa kudumu, ili kuboresha afya ya wananchi wa Tanzania: kiroho na kimwili!

Na Thompson Mpanji, Mbeya & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya XXVIII ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2020, ambayo imeadhimishwa hivi karibuni sehemu mbali mbali za duania, umeongozwa na kauli mbiu “Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kuelemewa na mizigo, nami nitawapumzisha”. Mt. 11:28. Baba Mtakatifu anasema huu ni mwaliko kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watu wanaoelemewa na sheria pamoja na mifumo kandamizi ya kijamii, ili aweze kuwakirimia tena matumaini mapya. Yesu anataka kuwaponya, kuwafariji na kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani, kwa kushiriki katika maisha yake.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kutibu, kujali na kuwaonjesha wagonjwa huruma na upendo kama sehemu ya mchakato wa uponyaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Faraja, huruma na upendo kwa wagonjwa, viwaguse pia wanafamilia wanaowatunza na kuwahudumia wagonjwa hawa! Kristo Yesu, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, aliweza kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi katika sekta ya afya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utu, heshima na haki msingi za wagonjwa zipewe kipaumbele cha kwanza na kamwe wasiwe ni mawakala wa utamaduni wa kifo kwa njia ya kifo laini au sera za utoaji mimba. Watu wana haki ya kuishi! Wafanyakazi katika sekta ya afya wanapaswa kusimama kwa miguu yao wenyewe, huku wakiongozwa na dhamiri nyofu na kamwe wasiwe ni wakala wa wanasiasa wanaotaka kutumia magonjwa kwa mafao yao binafsi!

Ni katika muktadha huu hivi karibuni, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya, katika maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2020 amegusia kuhusu changamoto zinazowakabili wagonjwa na familia maskini nchini Tanzania kuhusu Bima ya Afya, ili kuangalia changamoto zilizopo na hatimaye kuzipatia ufumbuzi wa kudumu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote! Amewahamasisha watanzania kuhakikisha kwamba wanakata Bima ya Afya kadiri ya uwezo wao, ili kukabiliana na kupanda kwa gharama za kuchangia huduma ya afya, ili kulinda na kudumisha Injili ya uhai! Amewashukuru waamini wanaoendeleza sera na mpango mkakati wa Kristo Yesu katika kuhubiri, kuganga, kuponya na kufariji kwa kusaidia kuwaweka watu huru wanaoelemewa na mzigo wa magonjwa na umaskini. Waamini waendelee kushuhudia utu wema, ukarimu na upendo kwa wagonjwa, ili Mungu atukuzwe na binadamu aweze kutakatifuzwa. Wagonjwa wahudumiwe kwa Neno, matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa dawa na ushauri unaotolewa na madaktari na wauguzi.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, amesema, Serikali inawajibu wa kuhakikisha kwamba, watanzania wanapata tiba bora kwa magonjwa yanayowasibu. Iangalie na kuchunguza changamoto zinazojitokeza katika Bima ya Afya ili kuzipatia ufumbuzi wa kudumu, ili kweli nia njema ya kuwapatia watanzania tiba kwa kuboresha afya zao na hatimaye kuwa na uhai tele iweze kudhihirika bayana! Huduma kwa wagonjwa ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na watu wote kuanzia kwa mgonjwa mwenyewe, familia na jamii katika ujumla wake, ili kuboresha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Magonjwa, umaskini na ujinga na maadui wakuu wa maendeleo fungamani ya binadamu! Magonjwa yanapunguza furaha, amani na utulivu wa ndani.

Askofu mkuu Nyaisonga amewataka watanzania kujilinda na kujitunza, kwani kuna magonjwa yanayoweza kutibika na yale ambayo hayana tiba wala chanjo na kwamba, ni heri kukinga kuliko kutibu. Amekumbushia kwamba, ugonjwa wa UKIMWI bado upo, kumbe, watanzania wanapaswa kubadili tabia sanjari na kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara. Wazazi na walezi wawe ni mifano bora ya kuigwa na jamii na kwamba, madaktari na wauguzi watekeleze vyema dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia sheria, kanuni, maadili na utu wema; unyenyekevu, upole, huruma na upendo vitawale katika huduma yao. Amewataka watanzania kuwa makini na manabii wa uwongo wanaojitokeza kwa kufanya miujiza ya uponyaji. Watanzania wawe wakweli katika kulinda na kutunza afya zao!

Askofu Mkuu Nyaisonga
20 February 2020, 13:35