Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anasema, kwa Wakristo Pango la Noeli ni ishara ya kushangaza sana, kwani hapa ni mahali alipozaliwa Mtoto Yesu: Ni mahali pa kusali, kutafakari na kukaa kimya! Papa Francisko anasema, kwa Wakristo Pango la Noeli ni ishara ya kushangaza sana, kwani hapa ni mahali alipozaliwa Mtoto Yesu: Ni mahali pa kusali, kutafakari na kukaa kimya!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Pango la Noeli ni Ishara ya Kushangaza kwa Wakristo

Pango la Noeli ni mahali pa kusimama, kutafakari na kusali katika ukimya. Kunahitajika kimya kikuu ili kuutafakari uzuri wa Uso wa Mtoto Yesu ambaye amelazwa kwenye hori ya kulishia wanyama. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai akazaliwa katika hali ya umaskini. Sala mbele ya Pango la Noeli ni kielelezo cha moyo wa shukrani na mshangao mkubwa mbele ya zawadi kubwa ya upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kutia saini kwenye Waraka wake wa Kitume “ADMIRABILE SIGNUM” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli”, akiwa kwenye Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio, Jumapili jioni, tarehe 1 Desemba 2019 wakati wa Liturujia ya Neno la Mungu, ametafakari kwa ufupi maana ya Pango la Noeli katika muktadha uliomzunguka Mtakatifu Francisko wa Assisi wakati ule. Jambo la kwanza, aligundua hali ya maisha ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, kiasi cha kupata mwamko wa kutengeneza mazingira yanayofanana na Pango la Bethlehemu, ili kwa kuona hekima ya Mungu kwa macho makavu, waamini waweze kupokea yale mambo msingi katika imani. Machoni pa waamini, Pango la Noeli linaonesha umuhimu wa maisha ambayo kwa bahati mbaya kutokana na changamoto mbali mbali yamekuwa kama “mchaka mchaka”.

Pango la Noeli ni mahali pa kusimama, kutafakari na kusali katika ukimya. Baba Mtakatifu anasema, kunahitajika kimya kikuu ili kuutafakari uzuri wa Uso wa Mtoto Yesu ambaye amelazwa kwenye hori ya kulishia wanyama. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai akazaliwa katika hali ya umaskini wa kutupwa. Sala mbele ya Pango la Noeli ni kielelezo cha moyo wa shukrani na mshangao mkubwa mbele ya zawadi kubwa ya upendo ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake. Katika Pango la Noeli, Ishara ya kushangaza, waamini wamejenga na kudumisha Ibada ambayo wameirithisha kwa kizazi baada ya kizazi. Ibada hii inakita mizizi yake katika: imani, matumaini na mapendo katika Fumbo la Umwilisho, ambalo ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu na kwa binadamu na maisha yake.

Mwenyezi Mungu katika busara na hekima yake ya Kibaba, ameamua kutembea bega kwa bega na watoto wake kwa njia ya uwepo wake, usionekana kwa macho makavu, lakini unaonekana kwa imani, katika nyakati za furaha au nyakati za mateso na machungu ya maisha. Yeye ni Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi! Kama ilivyokuwa kwa wachungaji kule kondeni mjini Bethelehemu, hata katika ulimwengu mamboleo, waamini wanahimizwa kuupokea wito na mwaliko wa kwenda mjini Bethelehemu kuona na kutambua “Signum” yaani “Ishara” ambayo wamepewa na Mwenyezi Mungu. Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu Francisko nyoyo za waamini zitaweza kusheheni furaha na hata kuweza kuipeleka mahali ambapo kuna majonzi;  kwani hapo patajazwa matumaini pamoja na kushirikiana na wale ambao wamepokonywa fadhila ya matumaini katika maisha yao.

Waamini waungane na Bikira Maria ili kumwona Mtoto Yesu akiwa amelazwa kwenye hori la kulishia wanyama, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Bikira Maria pamoja na Mtakatifu Yosefu, Mchumba wake mwaminifu, waamini wamwangalie Mtoto Yesu kwa ujasiri. Tabasamu lake la kukata na shoka linalopasua anga la usiku wa manane lifukuzie mbali tabia ya kutowajali wengine na hatimaye, kufungua nyoyo zinazobubujika kwa furaha kwa wale wanaohisi kwamba wanapendwa na Mwenyezi Mungu ambaye yuko mbinguni! Baba Mtakatifu mara baada ya tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, akiwa anasalimiana na Wafranciskani waliokuwa wamehudhuria Madhabahuni hapo, amewakumbusha changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Francisko wa Assisi watangaze na kushuhudia Injili ya Kristo kwa matendo yao adili na pale inapowezekana hata kwa maneno yao.

Uinjilishaji mpya unakita mizizi yake katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko na wala hakuna sababu ya kufanya wongofu wa shuruti. Kipaumbele cha kwanza ni kwa maskini na wadhambi wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu. Hii ni changamoto na mwaliko wa kutangaza na kushuhudia upendo wa Kristo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Huu ndio ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa Kristo Yesu: fukara, mtii, msafi kamili, kielelezo makini cha upendo usiokuwa na kipeo! Wakati huo huo, Wafranciskani wamemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea na kuwaenzi, wamemwahidia sala na sadaka zao, ili kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Papa: tafakari Pango la Noeli.
02 December 2019, 11:09