Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Pango la Noeli ni Ishara ya kushangaza na kustaajabisha sana, kwani hapa ni mahali alipozaliwa Mwana wa Mungu, Kristo Yesu! Papa Francisko: Pango la Noeli ni Ishara ya kushangaza na kustaajabisha sana, kwani hapa ni mahali alipozaliwa Mwana wa Mungu, Kristo Yesu! 

Papa Francisko: Pango la Noeli ni Ishara ya Kushangaza na Kustaajabisha

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 9 Desemba 2019 ametembelea Onesho la Mapango 100 ya Noeli kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anapenda kuwakumbusha waamini kwamba, Pango la Noeli ni ishara ya kushangaza na kustaajabisha; hapa panaonesha alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, alama hai ya Injili, mwaliko wa kutafakari Fumbo la Umwilisho

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “ADMIRABILE SIGNUM” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” anasema hiki ni kielelezo cha upendo wa Mungu; zawadi ya maisha inayokumbatia udugu na urafiki unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye pia ana uwezo wa kuwasamehe watu dhambi zao na kuwaweka huru! Injili na Pango la Noeli ni msaada mkubwa katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho, kwa kugusa nyoyo za watu na hivyo kuwazamisha katika historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. Huu ni mwaliko wa “kugusa na kuhisi umaskini wa Mwana wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, ili kuchuchumilia na kuambata njia ya unyenyekevu, ufukara na sadaka ili kufuata ile njia kutoka mjini Bethelehemu hadi mlimani Kalvari. Waamini wanaalikwa kukutana na kumhudumia Kristo Yesu anayejitambulisha na ndugu zake maskini na wahitaji zaidi.

Baba Mtakatifu katika tafakari yake, anagusia mazingira ya giza na kimya kikuu kinachotanda usiku wa manane, kielelezo cha watu wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti, kiasi cha kudhani kwamba, Mwenyezi Mungu, amewasahau waja wake na kwamba, maisha hayana tena thamani. Mwenyezi Mungu ndiye asili na hatima ya binadamu. Lakini mwanga utokao juu umewafikia na kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti. Mazingira ya Pango la Noeli yanaonesha magofu ya nyumba za kale kama ilivyokuwa kwa mji wa Bethlehemu uliogeuka kuwa ni makazi ya Familia Takatifu. Magofu haya ni utambulisho wa kuanguka kwa binadamu, kumezwa na malimengu na hatimaye, kujikuta akiwa amekata tamaa. Uwepo wa Kristo Yesu katika mazingira na hali kama hii unapania kupyaisha, kuganga na kutibu hali ya maisha ya binadamu ili yaweze kurejea tena katika mng’ao wake asilia. Ni mazingira yanayowaonesha wafugaji na mifugo yao, wanaofurahia kuzaliwa kwa Masiha, Mkombozi wa ulimwengu.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, akiwa ameongozana na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, Jumatatu, tarehe 9 Desemba 2019 ametembelea Onesho la Mapango 100 ya Noeli kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anapenda kuwakumbusha waamini kwamba, Pango la Noeli ni mahali ambapo panaonesha alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, alama hai ya Injili, mwaliko wa kutafakari Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwanadamu, ili kukutana na watu wote, ili kuwaonjesha upendo wake na hatimaye, waweze kuunganika pamoja naye. Kwa Waraka huu wa Kitume, Baba Mtakatifu anapenda kuwahamasisha waamini kuendeleza Mapokeo ya kuandaa Pango la Noeli kwenye familia, mahali pa kazi, shuleni, hospitalini, magerezani na kwenye maeneo ya wazi, kama kielelezo cha ibada katika Fumbo la Umwilisho. Mahali ambapo Ibada hii ilikuwa imeanza kufifia, Baba Mtakatifu anatoa mwaliko wa kuipyaisha tena.

Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kuweza kusalimiana na wasanii waliotengeneza Mapango ya Noeli kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakiwa wameambatana na familia zao. Waamini na mahujaji waliokuwepo katika eneo la tukio wametumbuizwa na kwaya ya Kodàly kutokaAmesali pamoja nao na hatimaye, akawapatia baraka yake ya kitume. Baadaye, Baba Mtakatifu amerejea kwenye Hosteli ya Santa Martha kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

Papa: Mapango ya Noeli
10 December 2019, 15:40