Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kurirhisha Ishara ya Kushangaza maana na umuhimu wa  Pango la Noeli Papa Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kurirhisha Ishara ya Kushangaza maana na umuhimu wa Pango la Noeli  (Vatican Media)

Papa Francisko: Warithisheni watoto: Umuhimu na maana ya Pango la Noeli

Pango la Noeli kwa Mwaka 2019 limetengenezwa kwa sehemu kubwa na mbao pamoja na vitu vyenye asili ya mikoa hii, vitakavyowasaidia watalii na mahujaji kugundua utajiri na maana ya Sherehe ya Kuzaliwa kwa Kristo. Vielelezo vilivyowekwa kwenye Pango la Noeli ni ushuhuda wa umaskini na udhaifu wa mwanadamu kama ilivyokuwa kwenye hori la kulishia wanyama mjini Bethlehemu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Pango la Noeli anasema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “ADMIRABILE SIGNUM” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” ni kielelezo cha upendo wa Mungu; zawadi ya maisha inayokumbatia udugu na urafiki unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye pia ana uwezo wa kuwasamehe watu dhambi zao na kuwaweka huru! Injili na Pango la Noeli ni msaada mkubwa katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho, kwa kugusa nyoyo za watu na hivyo kuwazamisha katika historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. Huu ni mwaliko wa “kugusa na kuhisi umaskini wa Mwana wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, ili kuchuchumilia na kuambata njia ya unyenyekevu, ufukara na sadaka ili kufuata ile njia kutoka mjini Bethelehemu hadi mlimani Kalvari. Waamini wanaalikwa kukutana na kumhudumia Kristo Yesu anayejitambulisha na ndugu zake maskini na wahitaji zaidi.

Ni katika muktadha huu wa Kipindi cha Majilio, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 5 Desemba 2019 amekutana na kuzungumza na watu wa Mungu kutoka Majimbo ya Trento, Vicenza, Treviso, Trento, Padua pamoja na Vittorio Veneto waliofadhili Mti wa Noeli utakaopambwa kwenye Pango la Noeli ambalo limejengwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatia shime kusonga mbele kwa imani na matumaini baada ya maeneo haya mwaka 2018 kukumbwa na majanga asilia, changamoto na mwaliko wa kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Taa kwenye Pango la Noeli zitawaka kipindi chote cha Sherehe za Noeli na waamini pamoja na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watakaofika kuhiji kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wataweza kushuhudia zawadi hii. Baba Mtakatifu amewashukuru pia kwa zawadi ya miche ya miti itakayopandwa kwenye Bustani ya Vatican na kwamba, yale maeneo yaliyoathirika kwa majanga asilia, yatapandwa tena miti ili kuendeleza uzuri wa kazi ya uumbaji.

Pango la Noeli kwa Mwaka 2019 limetengenezwa kwa sehemu kubwa na mbao pamoja na vitu vyenye asili ya mikoa hii, vitakavyowasaidia watalii na mahujaji kugundua utajiri na maana ya Sherehe ya Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Vielelezo vilivyowekwa kwenye Pango la Noeli ni ushuhuda wa umaskini na udhaifu wa mwanadamu kama ilivyokuwa kwenye hori la kulishia wanyama mjini Bethlehemu. Pango la Noeli lililowekwa pembeni mwa Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI, litawasaidia waamini na watalii kusimama, kutafakari na kusali mahali alipozaliwa na Mtoto Yesu. Baba Mtakatifu anasema, Jumapili ya kwanza ya Majilio, tarehe 1 Desemba 2019 akiwa kwenye Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio, Rieti, Mkoani Lazio, nchini Italia, Pango la kwanza kabisa la Noeli lililotengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi ametia mkwaju kwenye Waraka wa Kitume wake wa Kitume: “ADMIRABILE SIGNUM” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli”.

Baba Mtakatifu anasema, utamaduni wa kutengeneza Pango la Noeli unapaswa kuendelezwa na kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya. Kipindi cha Noeli kisipokwe na wafanyabiashara wanaotaka kuuza bidhaa zao kwa kuweka alama zao na kusahau maana ya Ishara ya kushangaza yaani Pango la Noeli. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuadhimisha Sherehe ya Noeli katika hali ya umoja, udugu, upendo na mshikamano wa dhati na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Papa: Pango la Noeli
05 December 2019, 15:41