Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa ajili ya Siku ya 53 ya Kuombea Amani Duniani tarehe 1 Januari 2020: Amani ni safari ya matumaini: Majadiliano, Upatanisho na Wongofu wa kiekolojia. Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa ajili ya Siku ya 53 ya Kuombea Amani Duniani tarehe 1 Januari 2020: Amani ni safari ya matumaini: Majadiliano, Upatanisho na Wongofu wa kiekolojia.  (Vatican Media)

UJUMBE WA PAPA FRANCISKO WA KUOMBEA AMANI DUNIANI MWAKA 2020

Baba Mtakatifu anazungumzia amani, kama safari ya matumaini inayokabiliana na vizingiti na majaribu. Amani ni safari ya ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza unaosimikwa katika kumbu kumbu, mshikamano na udugu. Amani ni safari ya upatanisho katika umoja wa kidugu. Amani ni safari ya wongofu wa kiekolojia na kwamba, watu wataweza kupata yale yote wanayotumainia. Amani 2020!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 53 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2020 sanjari na Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu inayoadhimishwa tarehe Mosi Januari, yanaongozwa na kauli mbiu: Amani ni safari ya matumaini: Majadiliano, Upatanisho na Wongofu wa kiekolojia. Amani na utulivu wa Jumuiya ya Kimataifa, hauwezi kamwe kujengeka katika msingi wa vitisho na hofu ya maagamizi, kumbe, kuna haja ya kuvunjilia mbali mawazo ya vitisho na hofu. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anapembua kwa kina na mapana amani, kama safari ya matumaini inayokabiliana na vizingiti pamoja na majaribu. Amani ni safari ya ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza unaosimikwa katika kumbu kumbu, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Amani ni safari ya upatanisho katika umoja wa kidugu. Amani ni safari ya wongofu wa kiekolojia na kwamba, watu wataweza kupata yale yote wanayotumainia.

Baba Mtakatifu anasema, amani ni tunu azizi na lengo la matumaini ya familia ya binadamu ingawa inakabiliwa na vikwazo vingi. Matumaini yanawatia moyo waamini kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu hata kama vizingiti vilivyoko mbele yao vinaonekana kuwashinda nguvu. Maisha ya mwanadamu bado yana makovu ya vita na misigano; yanakabiliwa na mnyororo wa unyonyaji, rushwa na ufisadi unaochochea chuki na vita. Matokeo yake watu wengi wananyimwa: utu, uhuru, mshikamano na matumaini kwa siku za mbeleni. Wengi wao wanageuka kuwa ni wahanga wa nyanyaso na ubaguzi na hatimaye, kutumbukizwa katika machungu, vitendo vinavyowakosesha haki pamoja na mashambulizi dhidi ya ndugu na jamaa zao. Matukio yote haya yanaacha chapa ya kudumu katika moyo wa mwanadamu. Ikumbukwe kwamba, vita ni kielelezo cha mauaji ya watu na inakwamisha mchakato wa ujenzi wa udugu.

Vita ni matokeo ya watu kutokukubaliana katika tofauti zao, tabia ya baadhi ya watu “kujimwambafai” kutokana na kumezwa na ubinafsi na kiburi, kwa kutaka kuwatenga au kuwafyekelea mbali wengine. Vita inachochewa na mahusiano tenge, uchu wa mali na madaraka, tabia ya kuwaogopa wengine kwa kudhani kwamba, tofauti zao msingi ni kizingiti. Na matokeo yake, vita inapamba moto na kusambaa kwa kasi kama “moto wa mbugani”. Amani na utulivu wa Jumuiya ya Kimataifa, hauwezi kamwe kujengeka katika msingi wa vitisho na hofu ya maagamizi, kumbe, kuna haja ya kuvunjilia mbali mawazo ya vitisho na hofu. Amani ya kweli inafumbata: kanuni maadili ya mshikamano na ushirikiano kwa ajili ya huduma inayokita mizizi yake katika uwajibikaji wa familia nzima ya binadamu kwa sasa na kwa siku za mbeleni.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, vitisho vinajenga mazingira ya watu kutokuaminiana na hivyo kujihami; ni tabia inayovuruga mahusiano na mafungamano ya watu kiasi kwamba, inakuwa ni vigumu kujenga misingi ya amani. Hofu, utengenezaji, ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia na utandawazi usioguswa wala kujali mahangaiko ya wengine, matokeo yake ni maamuzi ya kiuchumi yanayofanywa bila kuzingatia utu na mahitaji msingi ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kurejea tena katika asili ya binadamu kwa kujadiliana na kuaminiana. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, amani ni tamanio la ndani kabisa katika moyo wa mwanadamu na wala hakuna sababu ya kukata tamaa kutafuta amani duniani. Baba Mtakatifu anasema, amani ni safari ya ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza unaosimikwa katika kumbu kumbu, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Hibakusha, yaani wahanga wa mabomu ya atomiki yaliyorushwa huko Hiroshima na Nagasaki ni mashuhuda ya mateso ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kunako mwaka 1945. Hawa ni wahanga na kumbu kumbu endelevu ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya maangamizi, changamoto na mwaliko wa kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na udugu. Kumbu kumbu hii iwe ni fundisho kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya maamuzi mazito yatakayosaidia kudumisha amani duniani, kwa kuendelea kuwa na matumaini; kwa kujenga mshikamano na hatimaye, kufanya maamuzi mazito yanayoibua “cheche” za matumaini miongoni mwa watu. Kuna haja ya kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii kwa kujikita katika kanuni maadili inayomwilishwa katika utashi wa kisiasa, ili kuwaunganisha na kuwapatishana watu wanaotofautiana na kusigana.

Baba Mtakatifu anakazia kuhusu majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pamoja na kuheshimu utawala wa sheria. Kwa kujenga utamaduni wa kusikilizana, kutasaidia kuondoa maamuzi mbele ya kuwaona wengine kuwa ni maadui na badala yake kuanza kuwaangalia kama ndugu wamoja. Safari ya amani ni dumifu na inayohitaji fadhila ya uvumilivu ili kutafuta ukweli na haki sanjari na matumaini badala ya kutaka kulipiza kisasi. Nchi inayoheshimu utawala wa sheria na demokrasia ya kweli inaweza kusaidia mchakato wa haki pamoja na kuwalinda wanyonge ili hata wao waweze pia kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ili kuweza kufikia lengo hili kuna haja ya kukuza na kuimarisha demokrasia na elimu ili kuwawezesha watu kutambua haki, wajibu na mipaka ya uhuru wao.

Sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu, isaidie kubomoa mipasuko na migawanyiko ya kijamii na pengo kati ya matajiri na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Nguvu ya ukweli na uwazi isaidie jamii kutafuta na kuambata ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuendelea kurutubisha matumaini kwa ajili ya amani huku wakisaidiwa na tunu msingi za maisha ya Kikristo, kanuni maadili pamoja na mchango wa Kanisa katika medani mbali mbali za maisha. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya 53 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2020 anasema, amani ni safari ya upatanisho katika umoja wa kidugu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na uchu wa madaraka ya kutaka kuwatala wengine na badala yake, watu wajisikie kuwa ni ndugu wamoja, kwa kuheshimiana na kuthaminiana ili hatimaye, kuondokana na mnyororo wa kutaka kulipizana kisasi; kwa kusamehe na kusahau na hivyo kutambuana kama ndugu.

Nguvu ya msamaha inawawezesha watu kuwa ni mashuhuda wa amani katika masuala ya kisiasa na kiuchumi kwa sababu amani inakita mizizi yake katika medani mbali mbali za maisha ya kawaida. Baba Mtakatifu Mstaafu Beneditko XVI anasema amani ya kweli inafumbatwa katika mfumo wa uchumi unaozingatia haki, kwa kuondokana na mambo yale ambayo yanakwamisha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, amani ni safari ya wongofu wa kiekolojia, kwa kuwa na matumizi bora ya rasilimali za dunia badala ya kutumia utajiri wa dunia kwa vita na vitendo vya uvunjifu wa haki kiasi cha kushindwa kulinda na kuendeleza kazi ya uumbaji. Uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka vinapelekea watu kushindwa kuthamini jumuiya asilia, kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kulinda mafao ya wengi.

Ni kutokana na muktadha huu, kuna haja ya kufanya wongofu wa kiekolojia; kwa kujenga mazingira bora zaidi kati ya wananchi asilia na ardhi yao; kati ya nyakati zilizopita, mang’amuzi pamoja na matumaini kwa siku za mbeleni. Safari hii ya upatanisho inawataka walimwengu kusikiliza na kuitafakari dunia ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu ili aitunze kama nyumba ya wote. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kurithishwa mazingira bora zaidi, changamoto inayowashirikisha watu wote bila ubaguzi. Kumbe, kuna umuhimu wa kubadili mawazo na kujenga utamaduni wa kukutana na kuwapokea wengine jinsi walivyo sanjari na kuheshimu zawadi ya kazi ya uumbaji inayoakisi uzuri na hekima ya Mungu Muumbaji. Watu watathubutu kuwa na mtazamo mpya wa maisha, kuheshimu na kukubali tofauti msingi; kwa kuthamini, kusherehekea na kushirikishana zawadi ya maisha pamoja na kuendeleza mafao ya wengi kwa ajili ya ustawi wa familia kubwa ya binadamu.

Wongofu wa kiekolojia uwawezeshe watu kutambua umuhimu wa zawadi ya maisha; mahusiano na maendeleo fungamani ya binadamu na kwamba, hii ni fursa pia kama waamini ya kukutana na Kristo Yesu mintarafu mazingira yanayowazunguka na wanamoishi. Baba Mtakatifu anasema, watu wataweza kupata yale yote wanayotumainia kwa sababu safari hii ya upatanisho inahitaji uvumilivu na uaminifu, ili kupata amani ambayo watu wanaitamani sana kutoka katika sakafu ya nyoyo zao. Watu wawe na imani kwamba, amani inaweza kupatikana kwa sababu upendo wa Mungu unaokoa, hauna mipaka, unatolewa bure na wala hauchakai hata kidogo. Hofu ni chanzo kikuu cha vita na mipasuko ya kijamii, kumbe, kuna haja ya kuondokana na hofu kwa kutambua kwamba, binadamu wote ni watoto na wanapendwa na Mwenyezi Mungu. Utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi, unafeyekelea mbali kinzani na hivyo kutoa nafasi kwa watu kuonja upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, kwa kuishi na kujenga udugu wa kibinadamu.

Amani ni safari ya upatanisho na kwa waamini wanapaswa kuenzi jitihada hizi kwa kukimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, yaani Sakramenti ya Upatanisho inayopyaisha tena maisha yao kwa kumwangalia Kristo Yesu aliyepatanisha mbingu na dunia kwa njia ya Damu yake azizi. Huu ni mwaliko wa kuondokana na mawazo, maneno na vitendo dhidi ya Mwenyezi Mungu, jirani na mazingira nyumba ya wote, kwa kudumisha upendo mkamilifu. Msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu anasema Baba Mtakatifu, iwe ni sadaka itakayowawezesha kuwa ni vyombo na wajenzi wa haki na amani kwa msaada na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Bikira Maria Mama wa Mfalme wa Amani na Mama wa wote, awasindikize hatua kwa hatua katika safari ya upatanisho, ili watu wote wa Mungu waweze kuonja amani na kupata maendeleo ya kweli, ili upendo wa Mungu uweze kukaa ndani mwao!

Papa: Amani Duniani 2020

 

26 December 2019, 10:14