Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe kwa washiriki wa mkutano wa COP25 akiwahimiza kushughulikia changamoto za athari za tabianchi kwa ushirikiano. Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe kwa washiriki wa mkutano wa COP25 akiwahimiza kushughulikia changamoto za athari za tabianchi kwa ushirikiano.  (AFP OR LICENSORS)

Ujumbe wa Papa Francisko kwa wajumbe wa Mkutano wa COP25, Madrid, Hispania.

Baba Mtakatifu Francisko anasema inasikitisha kuona kwamba, miaka minne imekwisha kuyoyoma tayari, lakini utambuzi wa athari za mabadiliko ya tabianchi bado ni duni sana, kiasi cha kushindwa kujibu kikamilifu changamoto zinazotolewa na tafiti za kisayansi kama zile zilizobainishwa na Taarifa Maalum ya Jopo la Wataalam wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, IPCC. Ushirikiano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya ongezeko la joto duniani linalohatarisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ni kati ya changamoto kubwa zinazovaliwa njuga kwa sasa na Umoja wa Mataifa. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinatishia sana maisha ya watu wengi duniani: magonjwa ya mlipuko, umaskini na maafa makubwa kwa watu na mali zao.  Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuhakikisha kwamba, inashikamana kwa dhati ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza kwa vitendo Makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015. Jumuiya ya Kimataifa ilipitisha mkataba mpya wa Paris ambao umeweka historia mpya kwa nchi 195 kukubali kushirikiana katika kushughulikia athari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kupitisha mkataba mpya wa kisheria unaozijumuisha nchi zote katika mchakato wa kupunguza gesi joto duniani.

Kuanzia tarehe 2-13 Desemba 2019, Umoja wa Mataifa unafanya Mkutano wa 25, COP25 chini ya uongozi wa Mrs. Carolina Schmidt, Waziri wa Mazingira kutoka Chile ambaye pia ndiye Rais wa Mkutano wa 25, COP25 kuhusu mazingira unaoendelea mjini Madrid, nchini Hispania. Mkutano huu unawajumuisha wataalam wa mazingira kutoka katika nchi 196 na unahudhuriwa na wajumbe 29, 000. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwatumia ujumbe washiriki wa mkutano huu unaopania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inatekeleza Makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliopitishwa mjini Paris kunako tarehe 12 Desemba 2015. Utekelezaji huu ni mwaliko kwa wadau wote kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, malengo yaliyowekwa yanafikiwa ili kukabiliana na changamoto kubwa ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Jumuiya ya Kimataifa inatambua fika athari za mabadiliko ya tabianchi kama kikwazo kikubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Jambo la msingi kwa wakati huu ni Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa pamoja ili kujenga na kutunza mazingira nyumba ya wote. Inasikitisha kuona kwamba, miaka minne imekwisha kuyoyoma tayari, lakini utambuzi wa athari za mabadiliko ya tabianchi bado ni duni sana, kiasi cha kushindwa kujibu kikamilifu changamoto zinazotolewa na tafiti za kisayansi kama zile zilizobainishwa na Taarifa Maalum ya Jopo la Wataalam wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, IPCC. Taarifa hii inabainisha mapungufu yanayoikabili Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kama ilivyokubaliwa kunako mwaka 2015 huko mjini Paris, Ufaransa. Kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa maendeleo kimataifa, kwa kuhamasisha mshikamano pamoja na kuunganisha nguvu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na umaskini. Utekelezaji huu unapaswa kuvaliwa njuga na watu wote wa Mungu bila ubaguzi.

Muda uliobakia ni mchache wakati gharama za kupambana na athari hizi zinaendelea kuongezeka maradufu. Jambo msingi la kujiuliza ni ikiwa kama kuna wanasiasa wenye utashi wa kisiasa ambao wanapenda kutoa kwa uaminifu, uwajibikaji na ujasiri ili kuchangia kutoa rasilimali watu, fedha na teknolojia ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na kuwasaidia maskini pamoja na nchi maskini zaidi duniani zinazoendelea kuteseka kutokana na athari hizi. Baba Mtakatifu anasema, tafiti mbali mbali za kisayansi zimeonesha jinsi ambavyo Jumuiya ya Kimataifa inaweza kudhibiti ongezeko la joto duniani. Hapa kikubwa zaidi ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajielekeza zaidi kwa kuwekeza katika raslimali fedha na vitega uchumi vitakavyoboresha afya ya watu ili dunia hii iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa leo na kesho yenye matumaini. Hapa mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni pamoja na watu kuwa makini katika mfumo mzima wa uzalishaji, ulaji na elimu ili kukidhi utu na heshima ya binadamu.

Changamoto kubwa ni kujenga ustaarabu utakaosaidia kulinda mafao ya wengi na kwamba, utu na heshima ya binadamu vinapaswa kuwa ni sehemu ya mchakato huu. Umefika wakati wa kutumia fursa adhimu zilizobakia kwa kutekeleza dhamana zinazowajibisha katika masula ya uchumi, maendeleo ya sayansi na teknolojia, masuala ya kijamii bila kusahau sekta ya elimu; kwani mambo yote haya yanategemeana na kukamilishana. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, matatizo changamani yanapaswa kushughulikiwa kama dharura, bila kukitishwa mzigo kizazi kijacho, bali kuyavalia njuga matatizo haya na kuyapatia suluhu inayoonesha: uaminifu, uwajibikaji, ujasiri na utambuzi wa changamoto hizi; mambo msingi yanayotakiwa kutekelezwa kwa ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Jumuiya ya Kimataifa inao wajibu wa kuwaachia vijana wa kizazi kipya sababu ya kuwa na matumaini na kufanya kazi katika utu wema kwa siku za usoni. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na wajumbe wa Mkutano wa 25, COP25 kuhusu mazingira nyumba ya wote.

Papa: CO25
04 December 2019, 17:01