Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopata Daraja Takatifu ya Upadre amezidnua pia Makao makuu ya Taasisi ya Kipapa ya Scholas Occurrentes, Roma. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopata Daraja Takatifu ya Upadre amezidnua pia Makao makuu ya Taasisi ya Kipapa ya Scholas Occurrentes, Roma.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Mchakato wa mfumo mpya wa elimu kimataifa!

Baba Mtakatifu amezindua mpango mkakati wa mwaka 2020, tukio la kimataifa litakaloadhimishwa hapo tarehe 14 Mei 2020, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mabadiliko ya mfumo wa elimu kimataifa”. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti, kwa kujikita katika elimu fungamanishi inayowataka vijana kuwa wasikivu, wajenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu katika usawa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 baada ya uzoefu na mang'amuzi yake huko nchini Argentina, kwa sasa inapania pamoja na mambo mengine kuendelea kuwa mahali pa vijana kutambua na kushuhudia Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo. Kukuza elimu na kudumisha malezi bora kwa kujenga na kudumisha madaraja na utamaduni wa watu kukutana; kwa kuthamini na kuheshimu tofauti zao msingi sanjari na kila mtu akiwa na utambulisho wake makini. Tarehe 13 Desemba 2019 kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya tano ametembelea na kuzindua makao makuu mapya ya Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes". Katika tukio hili adhimu, Baba Mtakatifu ameweza kuzungumza mubashara kutoka Vatican na wanafunzi waliokuwa kwenye Kituo cha Haiti na Los Angeles, Marekani.

Wanafunzi kutoka Japan, Argentina, Marekani, Haiti, Israeli, Msumbiji, Mexico, Colombia na Italia, wameshiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 13 Desemba 1969. Baadhi ya wanawake wa Marais kutoka Amerika ya Kusini wanaounga mkono juhudi hizi za elimu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote wameshiriki. Jicho la Mama Kanisa kwa wakati huu ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuzindua mpango mkakati wa mwaka 2020, tukio la kimataifa litakaloadhimishwa hapo tarehe 14 Mei 2020, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mabadiliko ya mfumo wa elimu kimataifa”. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti, kwa kujikita katika elimu fungamanishi inayowataka vijana kuwa wasikivu, wajenzi wa majadiliano pamoja na kuongeza jitihada za kufahamiana, changamoto mamboleo, ili kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano ya kijamii kwa ajili ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa elimu itakayosaidia kuleta mfumo mpya wa uchumi duniani unaojikita katika wongofu wa kiekolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ndio mwelekeo pia wa tukio la "Economy of Francesco" yaani "Uchumi wa Francisko” litakalotimua vumbi huko mjini Assisi kuanzia tarehe 26-28 Machi 2020. Baba Mtakatifu anataka kuzama zaidi katika uchumi unaouhisha na wala si ule unaowatumbukiza watu katika kifo. Uchumi fungamani unaojikita katika tunu msingi za utu na heshima ya binadamu; uchumi unaokita mizizi yake katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anasema, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu hali ambayo imesababisha hata kinzani na mabadiliko si tu katika masuala ya kitamaduni bali pia kuhusiana na elimu ya binadamu, kwa kuunda lugha mpya ambayo inawatenga watu na kudhohofisha dhana ya elimu ya jadi.

Leo hii kuna kile kinachoitwa mchakato wa mwendokasi wa elimu unaofumbatwa katika kasi kubwa ya teknolojia na matumizi ya komputa yanayokinzana na kasi ndogo ya mabadiliko ya kibaiolojia. Kimsingi mchakato wa mabadiliko katika elimu unapaswa kuwahusisha watu wote ili kuunda “kijiji cha elimu”, mahali ambapo watu wote kadiri ya dhamana zao wanashiriki wajibu wa kuunda mtandao ambao ni wazi kwa ajili ya ujenzi wa mafungamano ya kibinadamu, kwani kila mtu anakuwa na wajibu wa kuchangia katika mchakato wa elimu. Kuna umuhimu wa kuanzisha kijiji cha elimu kabla ya kuanza kutoa elimu, kwa kuandaa mazingira ya udugu wa kibinadamu pamoja na kuondokana na ubaguzi. Kijiji cha elimu anasema Baba Mtakatifu ni jukwaa ambalo inakuwa rahisi kuweza kufikia muafaka wa elimu fungamani inayomheshimu binadamu na kuunganisha masomo na hali halisi ya maisha kati ya wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, michezo, siasa, biashara na wenyeji wote wa nyumba ya wote.

Ili kuweza kufikia ujenzi wa kijiji cha elimu, kwanza kabisa binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kukazia mifumo rasmi na isiyo rasmi ya elimu, ili kuwa na mwelekeo wa pamoja kuhusu: elimu ya binadamu, uchumi, siasa, ukuaji na maendeleo fungamani. Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" ina shule 450 katika nchi 190. Hizi ni shule za Serikali na binafsi zinazomilikiwa na kuendeshwa na dini mbali mbali duniani! Ndoto kubwa ya Baba Mtakatifu ni kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, hasa maskini zaidi duniani, kwa kuwajengea uwezo wa kusimama kidete kujenga, kulinda na kutetea amani, ustawi na mafao ya wengi.  Baba Mtakatifu anawataka vijana kujisadaka bila ya kujibakiza ili kutengeneza mtandao utakaowawezesha kushirikishana: ujuzi, elimu, maarifa, weledi pamoja na kipaji cha ugunduzi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, udugu na majadiliano, tayari kupandikiza mbegu hizi, ili ziweze kukua na kukomaa, kwa njia ya uongozi makini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Vijana wanakumbushwa kwamba wao ni leo ya Mungu, wanayopaswa kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao; kwa kushirikiana na wengine ili kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi.

Papa: Elimu
15 December 2019, 12:46