Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete dhidi ya rushwa na ufisadi duniani kwa kukazia kanuni maadili na utu wema. Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete dhidi ya rushwa na ufisadi duniani kwa kukazia kanuni maadili na utu wema.  (AFP or licensors)

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa na Ufisadi 2019

Rushwa inasigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni ugonjwa unaowaelemea watu wenye uchu wa madaraka, mali na utajiri wa haraka haraka. Baba Mtakatifu aliwahi kusema kwamba, kiini cha utumwa mamboleo, ukosefu wa fursa za ajira, uharibifu wa mazingira, ukwapuaji wa rasilimali na utajiri wa maliasili ni saratani ya rushwa inayorutubishwa na utamaduni wa kifo! RUSHWA!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Umoja wa Mataifa kunako tarehe 31 Oktoba 2003 ulianzisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa pamoja na Ufisadi, inayoadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 9 Desemba. Kwa mwaka 2019, Umoja wa Mataifa unawataka watu wa Mungu kuwasikiliza vijana ili kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu zinaendelezwa na kudumishwa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres anasema, Jumuiya ya Kimataifa ina lazima na wajibu wa kuwasikiliza vijana wanaoendelea kudai uwajibikaji na haki kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya saratani ya rushwa na ufisadi duniani. Vijana wanataka kuona shughuli mbali mbali zinatekelezwa kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi, uaminifu na uadilifu. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu kusimama kidete ili kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi, ili kweli rasilimali na utajiri wa nchi husika viweze kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya saratani ya rushwa duniani kwa njia ya vitendo, kwani maneno matupu hayavunji mfupa! Rushwa inasigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni ugonjwa unaowaelemea watu wenye uchu wa madaraka, mali na utajiri wa haraka haraka, lakini matokeo yake ni kuendelea kuwatumbukiza watu wengi zaidi katika umaskini wa hali na kipato! Baba Mtakatifu aliwahi kusema kwamba, kiini cha utumwa mamboleo, ukosefu wa fursa za ajira, uharibifu wa mazingira, ukwapuaji wa rasilimali na utajiri wa maliasili ni saratani ya rushwa inayorutubishwa na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika uchu wa mali na madaraka. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujitokeza kifua mbele kupambana na rushwa pamoja na kung’oa mizizi yake, ili kweli huruma iweze kutawala na uzuri kumwilishwa katika maisha ya watu ili kuondokana na utupu wa maisha.

Rushwa ni tatizo na changamoto kubwa katika maisha ya binadamu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka, mambo yanayochangia kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya, utumwa mamboleo na mikataba ya kimataifa! Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanasali ili kweli saratani ya rushwa iweze kutokomezwa kutoka kwenye uso wa dunia! Rushwa ni hatari sana katika medani mbali mbali za maisha. Umoja wa Afrika katika mkutano wake wa thelathini uliomaliza huko Addis Ababa ulitangaza kwamba, Mwaka 2018 ulikuwa ni Mwaka wa Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika. Kardinali Peter Turkson amefanikiwa kuchimbua mizizi ya maeneo yanayoweza kuchochea kishawishi cha rushwa na ufisadi. Ameanza katika maisha ya kiroho, yaani kutoka katika undani wa mtu mwenyewe na kupanua wigo huu katika maisha ya kijamii, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi sanjari na kuelezea dhamana na wajibu wa Mama Kanisa katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, saratani inayopekenyua maisha ya mataifa mengi duniani, kiasi cha kukwamisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Hii ni changamoto pevu katika maisha, utume na utambulisho wa Kanisa, ndivyo anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji ya kitabu kuhusu “Rushwa” kilichoandikwa na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu baada ya kufanya mahojiano maalum na Bwana Vittorio V. Albert. Kardinali Turkson anasema, Kanisa halina budi kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; uhalifu wa magenge kitaifa na kimataifa. Ili kufanikisha mapambano haya, rushwa haina budi kushughulikiwa kama “chuma chakavu” ndani ya Kanisa kwa kujikita katika: kanuni maadili, utu wema sanjari na kuambata tunu msingi za Kiinjili. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kuongoza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Lakini kwanza kabisa, Kanisa halina budi kuwa safi pasi na mawaa wala makunyanzi ya rushwa na ufisadi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, rushwa ni mchakato unaoharibu na kuvunjilia mbali kabisa mafungamano, upendo na mshikamano wa binadamu, demokrasia na maendeleo endelevu ya binadamu.

Rushwa inatia doa uhusiano kati ya binadamu, Mwenyezi Mungu na kazi ya uumbaji. Lakini kinyume cha rushwa ni: Uaminifu, uadilifu, utu wema, upole na unyofu wa moyo mambo yanayopania kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa inaonesha maisha ya mwanadamu asiyekuwa na dira wala mwelekeo sahihi wa maisha, hali inayoharibu sana mafungamano ya kijamii. Matokeo yake ni kukomaa kwa ubinafsi usiokuwa na mvuto wala mashiko; tabia ya kutowajali wengine. Rushwa inaonesha ile roho ya korosho, roho ya kwa nini; roho ya kutu, roho iliyovunda na kuanza kutoa harufu mbaya. Rushwa ni kikwazo katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa inapelekea kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Ni chanzo kikuu cha kuibuka na kusambaa kwa magenge ya kihalifu, kitaifa na kimataifa; magenge yanayochochea utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ili kupambana na rushwa pamoja na ufisadi kuna haja ya kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi, kimaadili, kitamaduni na kiutu!

Hii inatokana na ukweli kwamba, rushwa inapata chimbuko lake katika moyo wa mwanadamu! Rushwa ina tabia ya kujigeuza geuza kadiri ya mazingira na vionjo vya mtu, kumbe, hakuna anayeweza kujidai kwamba, rushwa ameipatia kisogo! Jambo la msingi ni kuwa macho na makini; kwa kukesha na kusali, ili kutokutumbukia majaribuni! Kanisa ni mama na mwalimu wa tabia ya kimaadili na utu wema. Ni sauti ya kinabii inayotetea haki, kupinga na kukemea mambo yasiyo ya haki. Kanisa linahimiza umuhimu wa kumwilisha Injili ya huruma, upendo, mshikamano na udugu kwa watu wote. Kanisa linapenda kusimama kidete, kulinda na kuwatetea maskini, wajane, yatima na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha. Kwa namna ya pekee, Kanisa linaitwa kujenga na kuimarisha Ufalme wa Mungu hapa duniani kwa kusaidia kuunga mkono sera za kiuchumi, kisiasa na kijamii zinazokuza na kudumisha: haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Sera na mikakati inayopania kulinda utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; mambo ambayo yanapata mwanga wake katika Maandiko Matakatifu na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Kimsingi, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanafumbatwa katika utu wa binadamu, ustawi, maendeleo fungamani na mafao ya wengi; udugu na mshikamano; ushiriki wa watu katika kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati mintarafu mustakabali wa maisha yao kwa kuzingatia kanuni auni! Ni mafundisho yanayojikita hasa katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kuzingatia pia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama sehemu ya mchalato wa mwendelezo wa kazi ya Uumbaji ambayo binadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu. Huu ndio mwongozo rasmi wa maisha na utume wa Kanisa katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata katika masuala ya kidini! Rushwa ni saratani inayokwamisha na kukatisha tamaa mchakato na jitihada za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo endelevu ya binadamu. Rushwa inawajengea watu uchu wa mali na madaraka kwa njia za mkato, inachafua na kudhohofisha kabisa mafungamano ya kijamii kwa kuunda matabaka ya watu wanaothaminiwa kutokana na uwezo wao wa kifedha na wale wanaodharauliwa kwa sababu si “mali kitu”.

Hapa utu na heshima ya binadamu vinapimwa si kutokana utu na heshima yake kwa vile ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu bali kwa ni kwa sababu anayo fedha na madaraka! Watu wawe na ujasiri wa kukemea na kupambana na rushwa si tu kwa maneno bali kwa matendo, ili kuondoa uovu ndani ya jamii na hatimaye, kudumisha haki, amani, upendo, mshikamano na demokrasia ya kweli. Huu ni ujasiri wa kutaka kukuza na kudumisha kanuni maadili, miiko ya kazi na utu wema; kwa kukuza sheria, nidhamu na misingi ya utawala bora. Rushwa ina madhara makubwa katika maisha ya wananchi kwani inapunguza umaarufu wa viongozi kiasi hata cha wananchi kukosa imani kwa viongozi wao. Rushwa inapelekea wananchi kujenga hasira dhidi ya serikali yao na haya ndiyo yanayoendelea kujitokeza kwa maandamano na migomo isiyokoma sehemu mbali mbali za dunia. Rushwa inashusha kiwango cha maadili, hali ya kuaminiana, inapotosha utu na heshima ya binadamu, inakuza na kudumisha ubinafsi, uchu wa fedha, tamaa ya mali na madaraka!

Siku ya Rushwa Duniani 2019

 

11 December 2019, 16:14