Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Shule ya Utakatifu wa maisha! Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Shule ya Utakatifu wa maisha! 

Sherehe ya Familia Takatifu: Yesu, Maria na Yosefu: Shule ya Utakatifu

Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mpango wa Mungu kwa mwanadamu sanjari na Mafundisho tanzu ya Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika maadhimisho ya Sherehe ya Familia takatifu linasema, familia ni shule ya utakatifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Mama Kanisa katika maisha na utume wake anapenda kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii inayotaka kugeuzia kisogo utakatifu wa maisha ya ndoa. Kanisa linatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbali mbali za Kikristo, kiutu na kijamii! Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Waamini wanakumbushwa kwamba, Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mpango wa Mungu kwa mwanadamu sanjari na Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika maadhimisho ya Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu hapo tarehe 29 Desemba 2019 linasema, familia ni shule ya utakatifu. Hapa ni mahali ambapo watu wa ndoa na familia wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kujichotea upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mwaliko kwa waamini kujichotea tena amana na utajiri uliofichika kwenye Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko“Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” kwa kuhakikisha kwamba, wanajitahidil kupyaisha upendo wao kila kukicha. Huu ni upendo unaofumbata sifa zile ambazo zimefafanuliwa kwa kina na mapana na Mtakatifu Paulo katika Waraka wake 1Kor. 13:4-7. Yaani upendo huvumilia, uko tayari kuwatumikia wengine, hautakabari, haujivuni, haukosi adabu. Upendo ni mkarimu, hauna hasira na kamwe haukati tamaa, husamehe, hufurahi pamoja na wengine, huvumilia yote, huamini, hutumaini na hustahimili yote. Huu ndio utajiri mkubwa unaofumbatwa katika upendo ndani ya familia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linawataka wanandoa kuheshimiana na kuthamini tofauti zao msingi kama utajiri unaokita mizizi yake katika ukarimu, msamaha na upendo wa dhati. Wanandoa wajifunze pia kupokea changamoto zinazojitokeza katika maisha kwa mfano magonjwa na misukosuko ya maisha ya ndoa na familia kama sehemu ya umwilishaji wa Heri za Mlimani kama muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Heri hizi ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya ndoa na familia! Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu iwe ni mfano bora wa kuigwa, kwa kuziwezesha familia zao kuwa ni mahali pa upendo na mshikamano; Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa sala na shule makini ya uinjilishaji wa kina unaozingatia mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili!

Furaha ya Upendo ndani ya familia “Amoris laetitia” “AL” ni Wosia wa Kitume ambao umetolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu Injili ya familia na kuchapishwa rasmi tarehe 19 Machi 2016, Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu mume wake Bikira Maria sanjari na kumbu kumbu ya miaka mitatau tangu Baba Mtakatifu Francisko alipoanza utume wake rasmi kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wosia huu wa Kitume ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia zilizoadhimishwa kunako mwaka 2014 na mwaka 2015. Sura ya tatu ya Wosia huu inatoa: Mwelekeo kwa Yesu: Wito wa Familia. Baba Mtakatifu Francisko katika sura hii anatoa muhtasari wa mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia. Hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayojikita katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi na ina mwelekeo wa kudumu ambayo ni zawadi.

Ndoa ni kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu, chemchemi ya upendo wa kweli wa wanandoa na wito mahususi wa kuishi kama bwana na bibi. Ndoa ni Sakramenti na zawadi inayowawezesha wanandoa kujikita katika mchakato wa utakatifu na wokovu wa wanandoa wenyewe. Kwa mwelekeo huu tendo la ndoa ndani ya familia, lililotakatifuzwa kwa Sakramenti ni njia ya kukua na kukomaa katika neema na Fumbo la maisha ya ndoa, mwaliko kwa wanandoa kumwomba Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili aweze kuibariki Ndoa yao. Kanisa halina budi kuwasaidia wanandoa wanaoishi “uchumba sugu” wale waliofunga ndoa ya Serikali; wanandoa wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha ya ndoa kwa baada ya kuoa au kuolewa  na kuachika na baadaye kuamua kuoa au kuolewa tena. Viongozi wanapaswa kuwashughulikia watu hawa kwa kuongozwa na ukweli wa upendo; wawafafanulie kwa kina na mapana mafundisho ya Kanisa na kwamba, hakuna majibu ya mkato, bali kila kesi inapaswa kushughulikiwa kikamilifu.

Viongozi wawe na hekima ya kutambua unyeti wa masuala wanayoshughulikia. Kwa wanandoa ambao hawakubahatika kupata watoto kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanahamasishwa kuridhika kwa kujikita katika utu wema na Ukristo, kwani watoto kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa mara nyingine tena tunu msingi ya maisha ya binadamu na haki ya mtu kuishi tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi kifo cha kawaida kinaqpomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu! Wafanyakazi katika sekta ya afya wanayo dhamana ya kimaadili kwa kukuza dhamiri nyofu ili kuendeleza zawadi ya uhai kwa kutojiingiza kwenye vitendo vya kifo laini au tiba za ghali sana. Kanisa linapinga adhabu ya kifo. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, kuna mahusiano muhimu sana kati ya Familia na Kanisa, kwani ikiwa kama Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, Kanisa ni familia ya familia na kwamba, upendo unaomwilishwa kwenye familia ni nguvu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Sherehe Familia Takatifu
26 December 2019, 16:38