Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ametembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la B.Maria Mkuu pamoja na Uwanja wa Spagna. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ametembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la B.Maria Mkuu pamoja na Uwanja wa Spagna. 

Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili: Sala kwa B. Maria

Bikira Maria ndiye binadamu pekee aliyekingiwa dhambi ya asili, kama Mama wa Yesu, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu. Upendeleo huu kwa Bikira Maria ni kwa ajili ya mafao ya watoto wake wote, kielelezo cha ushindi wa Kristo na Mungu dhidi ya dhambi. Mahali pale ambapo dhambi imeongezeka na hapo neema imeongezeka maradufu kwa nguvu ya Damu Azizi

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba mwaka 1854 katika Waraka wake wa Kitume “Ineffabilis Deus”, alitangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria!  Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 8 Desemba 2019 kabla ya kwenda kwenye Uwanja wa Spagna, kutoa heshima na kusali mbele ya Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Baba Mtakatifu amekwenda kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma. Maadhimisho haya yamehudhuriwa na umati mkubwa wa wagonjwa waliosindikizwa na Chama cha Kitaifa cha Kuwahudumia Wagonjwa nchini Italia, UNITALSI, ili kutoa heshima yao kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Wamepata fursa ya kusalimiana na Baba Mtakatifu Francisko ambaye katika maisha na utume wake, anaendelea kuwapatia wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kipaumbele cha kwanza. Kimsingi, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili inapania kuwa ni Siku ya sala, tafakari na mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya kijamii. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kusali na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupewa zawadi ya Mama Bikira Maria, Mkingiwa Dhambi ya asili, hata kama watoto wake bado wanaogelea kwenye dimbwi la dhambi. Bikira Maria ndiye binadamu pekee aliyekingiwa dhambi ya asili, kama Mama wa Yesu, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu. Upendeleo huu kwa Bikira Maria anasema Baba Mtakatifu ni kwa ajili ya mafao ya watoto wake wote, kielelezo cha ushindi wa Kristo na ushindi wa Mungu dhidi ya dhambi.

Mahali pale ambapo dhambi imeongezeka, yaani katika moyo wa mwanadamu, hapo neema imeongezeka maradufu kwa njia ya nguvu ya Damu Azizi ya Yesu. Bikira Maria anawakumbusha watoto wake kwamba wao ni wadhambi lakini hawapaswi kuwa tena ni watumwa wa dhambi kwa sababu kwa njia ya sadaka na mateso ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, amevunjilia mbali mnyororo wa dhambi na kuushinda ulimwengu. Huu ndio ujumbe unaosimuliwa na vizazi vyote kuhusu Moyo Safi wa Bikira Maria, huko mbinguni ambako mawimbi yote yametawanyika. Kuna utofauti kati ya kuwa mdhambi na fisadi na mla rushwa. Kwa sababu mdhambi anaanguka dhambini na anaweza kusimama tena kwa msaada wa neema na huruma ya Mungu akatubu na kumwongokea Mungu. Rushwa na ufisadi ni kielelezo makini cha unafiki na moyo ulioelemewa kwa uzito wa dhambi, kwa nje mtu anaonekana kuwa kweli ni mchamungu, lakini ndani mwake, kumejaa mawazo mabaya, ubinafsi na uchoyo.

Moyo Safi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni mwaliko kwa waamini kukuza ndani mwao ukweli, uwazi na unyofu wa maisha. Watoto wa Kanisa wanalo hitaji kubwa la kutaka kuokolewa kutoka katika dimbwi la rushwa na ufisadi ambalo linaelemea nyoyo za watu wa Mungu. Hili ni jambo ambalo linaonekana kwa macho ya kibinadamu kwamba, haliwezekani, lakini, waamini wakithubutu kuinua macho yao mbinguni, wataweza kukutana na tabasamu la “kata na shoka” kutoka kwa Mama Bikira Maria asiye na doa, ili kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa ajili ya mafao na upendo kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni katika muktadha huu anapenda kuwaweka watu wote walioko ndani ya mji wa Roma na ulimwengu katika ujumla wake, watu wanaonyanyasika kwa kukosa imani; waliokata tamaa kwa sababu ya dhambi, kiasi cha kudhani kwamba, dhambi zao ni kubwa sana kiasi cha kudhani kwamba, Mwenyezi Mungu hana nafasi tena kwa ajili yao. Wote hawa anawaweka chini ya ulinzi na tunza yake ya kimama, ili wasisite kamwe kuwapenda watoto wake.

Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, amejaa neema kiasi kwamba, anaweza kuwasaidia watoto wake kufukuza giza na ubaya wa moyo kwa mwanga wa Kristo Mfufuka ambaye ana uwezo na nguvu za kuvunjilia mbali minyororo ya utumwa wa dhambi. Ana uwezo wa kuwafungulia wahalifu wa kutupwa na kuwalainisha wale wenye mioyo migumu kama jiwe, ikiwa kama yote haya yapata chimbuko lake kutoka katika undani wa maisha yao na kwa njia hii sura ya mji wa Roma itaweza kubadilika. Baba Mtakatifu katika sala yake anasema, haya yote yanapaswa kumwilishwa katika matendo madogo madogo yanayotekelezwa kila siku. Kwa njia hii, kutakuwepo na maboresho makubwa ya maisha na kwamba, hali ya kijamii itakuwa na mwelekeo mpya zaidi. Baba Mtakatifu anamshukuru Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ambaye bado anawakumbusha kwamba,  upendo wa Kristo umewakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti na wala hawapaswi tena kuwa ni watumwa wa dhambi, bali watu huru, wenye uwezo wa kupenda na kupendwa, kwa kusaidiana kama ndugu wamoja licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza kati yao.

Baba Mtakatifu anamshukuru Bikira Maria ambaye kwa njia ya matendo yake anawatia shime kutenda mema na kuuonea ubaya aibu. Anamwomba Bikira Maria awasaidie kumweka mbali Shetani, Ibilisi, anayewashawishi na kuwavuta watu kwake na matokeo yake, wanaonja cha mtema kuni, yaani kifo kinawakodolea macho! Bikira Maria awakumbushe waamini kwamba, wao ni watoto wa Mungu Baba mwingi wa huruma na upendo, chemchemi ya maisha ya uzima wa milele, wema na uzuri. Amina!

Papa: Bikira Maria
09 December 2019, 11:52