Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili: Kioo cha imani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, hapo tarehe 8 Desemba 2019 anatarajiwa kwenda kwenye Uwanja wa Spagna, kutoa heshima zake kwa Sanamu ya Bikira Maria inayoheshimiwa sana na familia ya Mungu mjini Roma. Tukio hili litatanguliwa na Kikosi cha Zima moto kuweka shada la maua kwenye Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kama walivyofanya tarehe 8 Desemba 1857 mnara huu ulipozinduliwa rasmi kwa heshima ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Tangu mwaka 1953, viongozi wakuu wa Kanisa wamekuwa wakienda kutoa heshima zao kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Kabla ya kwenda kwenye Uwanja wa Spagna, Baba Mtakatifu Francisko atakwenda kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma.
Bikira Maria alipata upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyemkirimia karama na neema nyingi ili aweze kuwa ni Mama wa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Karne kwa karne Mama Kanisa ametambua kwamba, Bikira Maria aliyejazwa neema na Mwenyezi Mungu, alikombolewa tangu mwanzo alipotungwa mimba! Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kuwasaidia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kielelezo cha imani tendaji!
Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani, matumaini na mapendo, kwani amediriki kuwa ni mfuasi wa kwanza wa Kristo Yesu na chombo cha huduma makini kwa jirani zake; mtindo na mfumo wa maisha unaopaswa kutekelezwa na Mapadre kama sehemu ya majiundo yao ya awali na endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa watu wanaomkimbilia katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo ambaye pia ni ukweli na uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu.