Papa Francisko awaombea waathirika wa shambulizi la kigaidi jijini Moagadishu Somalia lililotokea tarehe 28 Desemba 2019 Papa Francisko awaombea waathirika wa shambulizi la kigaidi jijini Moagadishu Somalia lililotokea tarehe 28 Desemba 2019 

Sala ya Papa kwa ajili ya waathirika wa shambulizi la kigaidi jijini Mogadishu

Shambulio la kutisha la kigaidi limetokea jijini Mogadishu nchini Somalia Jumamosi tarehe 28 Desemba 2019 ambapo Papa Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Dominika 29 Desemba amewakumbuka katika sala waathirika zaidi ya 70 na majeruhi kadhaa.Waathirika hao ni pamoja na watoto wachanga na wanafunzi.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Papa  Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 29 Desemba 2019 wakati Familia ya Mungu inaadhimisha Sikukuu ya Familia Takatifu ambayo hufanyika Jumapili inayofuata mara baada ya Siku ya Kuzaliwa kwa Bwana ambapo ameomba waamini wote kusali kwa ajili ya waathirika wa shambulizi baya la kigaidi nchini Somalia. Papa amesema:  “Tusali kwa Bwana kwa ajili ya waathirika wa mashumbulizi mabaya  jana huko Mogadishu nchini Somalia mahali ambapo mabomu yalilipuka na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 70. Niko karibu na familia zote na wale wote wanaoomboleza kwa ajili ya wapendwa wao.

Papa Francisko akiendelea na salam pia amewakumbuka mahujaji wote wa Roma, makundi ya maparokia, vyama na vijana. Kwa namna ya pekee salam ni kwa ajili ya familia zote waliokuwapo katika uwanja wa Mtakatifu Petro na wale ambao kwa njia ya televisheni na radio walikuwa wanafuatilia! Papa amesema: "Familia ni tunu yenye thamani. Ni lazima na daima kuisadia na kulinda". Kwa wote amewatakia Jumapili njema na  matashi mema ya mwanzo wa mwaka mpya wa amani.

Ni tangu mwaka 1992 ambapo nchini Somalia inaendelea na vita hadi kudumu kwa miaka hii na misiba ya mikubwa kwa raia, kwa mujibu wa taarifa kutoka  Jumuiya ya Mtakatifu Egidio. Na hii wanasema, ni migogoro ambayo imesahulika na mahali ambapo maisha ya binadamu hayahesabiki tena. Haipiti hata wiki moja bila kuwa na waathirika katika mashambulizi ya kigaidi kama hayo! Aidha wanasema kuwa nchi imegawanywa bila kuwa na viongozi wa Somalia kupata mwafaka kati yao juu ya Katiba yao na utaratibu wa taasisi. Majaribio mengi yameshindwa katika miaka ya hivi karibuni na mikoa ya Somalia imejitenga kati yao kana kwamba kila mmoja anataka ajiokoe kadiri awezavyo kwa sababu ya kuachwa na kukataliwa na taasisi za kimataifa.

Hata hivyo kufuatia na tukio hili taarifa nyingine kutoka Jumuiya ya Umoja wa Mataifa inalaani vikali shambulio la kigaidi lililouwa watu zaidi ya 70 Jumamosi tarehe 28 Desemba 2019 mjini Moghadishu nchini Somalia. Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana  Antonio Guterres ametoa pole na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza Maisha katika tukio hilo na kuwatakia majeruhi wote ahuweni ya haraka. Amesisitiza kwamba wahusika wote wa ukatili na unyama huo ni lazima wafikishwe mbele ya sheria.

Kwa mujibu wa duru za habari, takriban watu 79 wameuawa na wengine 149 wamejeruhiwa baada ya bomu lililotegwa kwenye gari kulipuka kwenye eneo lililokuwa limejaa watu wengi nje kidogo ya mji mkuu Moghadishu saa za asubuhi za Somalia. Msemaji wa serikali ya Somalia Ismael Mukhtar amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa gaidi aliendesha gari lake lililokuwa na mabomu hadi kwenye kituo cha zamani cha ukaguzi cha Afgoye ambacho ni makutano maarufu yanayo  unganisha sehemu ya Kusini mwa Somalia na mji mkuu Moghadishu. Bwana Mukhtar ameongeza kusema kuwa miongoni mwa waliokufa katika shambulio hilo  ni wanafunzi wa chuo kikuu, raia na askari.

Hakuna kinachohalalisha ugaidi: Katibu Mkuu amerejea kusitiza ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia watu na serikali ya Somalia katika mchakato wao wa kusaka amani ya kudumu na maendeleo. Naye mwakilishi wa umoja wa Mataifa nchini Somalia na mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNSOM, Bwana, James Swan kupitia ukurasa wake wa Twitter anaalani vikali shambulio hilo la kikatili na kigaidi dhidi ya raia wasio na hatia akisisitiza kwamba wote waliohusika wanapaswa kufikishwa mbele ya mkono wa sheria na kuwajibishwa.

29 December 2019, 13:47