Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, amana ya imani "Fidei Depositum" inahifadhiwa na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, amana ya imani "Fidei Depositum" inahifadhiwa na Mama Kanisa.   (Vatican Media)

Safari ya Injili Duniani: Amana ya Imani inahifadhiwa na Kanisa!

Haiwezekani kumwamini Kristo na wakati huo huo kukimbilia na kujificha kwenye imani za kishirikina. Hata leo hii, licha ya kuenea kwa utamaduni na Mapokeo ya Kikristo, Baba Mtakatifu anasema bado kuna watu wanaoamini na kujishughilisha kwenye imani za kishirikina: kwa kupiga ramli na kwa kusomewa nyota. Tabia hii ni kwenda kinyume kabisa cha imani na matumaini kwa Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mzunguko wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume ni fursa ya kupembua: mchango wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa la Mwanzo na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji unaoendelea kutekelezwa na Mama Kanisa hata katika ulimwengu mamboleo kwa kukazia ushuhuda kama kielelezo cha imani tendaji. Mtakatifu Paulo Mtume, alipokuwa anawaaga wazee wa Efeso aliwataka kutunza nafsi zao na lile kundi lote ambalo Kristo Yesu amelinunua kwa Damu yake Azizi. Mtakatifu Paulo akawaweka katika mikono ya Mwenyezi Mungu, na kwa neno la neema kama sehemu ya urithi wao wa imani. Anawakumbusha kwamba, alifanya kazi kwa mikono yake mwenyewe ili kujipatia mahitaji yake msingi pamoja na kuwasaidia wanyonge daima wakikumbuka kwamba, “Ni heri kutoa kuliko kupokea”. Mdo. 20:32-35.

Katika safari hii, Mtakatifu Paulo anatoa Sakramenti ya Ubatizo kwa wakatekumeni kumi na wawili na wao pia wakampokea Roho Mtakatifu. Kwa jina la Yesu, Mitume wakatenda miujiza mbali mbali, wakawaponya wagonjwa na pepo wachafu wakawatoka. Mitume wa Yesu wakawa ni chemchemi ya maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na kwa njia hii wanafanana kabisa na Mwalimu wao. Kama kawaida Waswahili wanasema kwenye kundi la Mamba, Kenge hawakosekani. Hata wakati wa Paulo kulijitokeza kundi la Wayahudi wenye kutangatanga ambao walikuwa wanapunga pepo, wakajaribu kutumia jina la Yesu na Mtakatifu Paulo, lakini pepo wachafu wakawatoa mbio! Hofu ikawaingia Wayahudi na Wayunani na Jina la Yesu likaendelea kutukuzwa!

Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe  4 Desemba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Imani inamwezesha mwamini kujiachilia na kujiaminisha kwenye huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuokoa. Haiwezekani kumwamini Kristo na wakati huo huo kukimbilia na kujificha kwenye imani za kishirikina. Hata leo hii, licha ya kuenea kwa utamaduni na Mapokeo ya Kikristo, Baba Mtakatifu anasema bado kuna watu wanaoamini na kujishughilisha kwenye imani za kishirikina: kwa kupiga ramli na kwa kusomewa nyota. Tabia hii ni kwenda kinyume kabisa cha imani na matumaini kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kujiaminisha na kujisalimisha katika neema, huruma na upendo wa Kristo Mfufuka, ambaye atawakirimia kadiri anavyoona inafaa. Waamini wajielekeze zaidi katika sala kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu.

Safari ya Injili Duniani huko mjini Efeso inaharibu kabisa biashara ya waganga wa kienyeji na wapiga ramli waliokuwa wanajitajirisha kwa kutumia magonjwa, hofu na wasi wasi ya watu wa Mungu. Matokeo yake, kundi hili la waganga likajipanga na kuanza kumshutumu Mtakatifu Paulo kwa kuwaharibia biashara na mapato yao huko Efeso na kwamba, utajiri wao ulikuwa unapatikana kwa kazi hii na kwamba, kwa sasa si mali kitu tena. Ikamlazimu Mtakatifu Paulo mtume kuondoka kutoka Efeso mpaka Troa kwa kupitia Uyunani na Makedonia na huko Mileto, Mtume Paulo anawaaga wazee wa Efeso na kuwakabidhi “Mikoba ya shughuli za kichungaji”, ili kumtumikia Mungu kwa unyenyekevu, kwa kutangaza, kushuhudia na kufundisha Neno la Mungu katika ukweli na uwazi, kwa kusimama kidete kuwalinda wale waliomwongokea Kristo Yesu katika maisha yao.

Mtakatifu Paulo akawataka kukesha na kusali na mwishowe, akawaweka katika mikono ya Mwenyezi Mungu na kwa neno na neema yake ili kuwajenga na kuwapatia urithi wa imani Baba Mtakatifu anasema hii ni sehemu muhimu sana ya Kitabu cha Matendo ya Mitume inayoonesha jinsi ambavyo Wakristo wanapaswa kujiandaa kuaga na kuagana. Mtakatifu Paulo Mtume, anaitaka Jumuiya ya Wakristo kuwajibika kwa kukesha na kuwalinda watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema hiki ni kiini cha shughuli za kichungaji ambazo viongozi wa Kanisa wamekabidhiwa na Mama Kanisa. Waamini wanapaswa kukesha na kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani mwao. Maaskofu wanapaswa kusimama kidete kulinda kundi la waamini wao, kwa kuwa karibu nao.

Hatimaye, Mtakatifu Paulo naye akajikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Baba wa milele katika safari yake. Neno la Mungu ni chachu ya ukuaji na utakatifu wa maisha ya Kanisa. Waamini wanahimizwa kutekeleza vyema nyajibu zao pamoja na kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wahitaji zaidi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupyaisha upendo wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa kujichotea utajiri kutoka katika “Amana ya Imani: “Fidei Depositum” inayolindwa na kutunzwa ndani mwake. Waamini wajitahidi kulilinda, kuliendeleza pamoja na kuwaenzi wachungaji wao kwa njia ya sala na sadaka zao kama kielelezo cha ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Papa: Amana ya Imani
04 December 2019, 16:21