Tafuta

Waraka wa Kitume katika mfumo wa Barua Binafsi: "Motu Proprio": Dekano wa Baraza la Makardinali kuhudumia kwa muda wa miaka 5 tu, ingawa anaweza kurudia tena! Waraka wa Kitume katika mfumo wa Barua Binafsi: "Motu Proprio": Dekano wa Baraza la Makardinali kuhudumia kwa muda wa miaka 5 tu, ingawa anaweza kurudia tena! 

Papa Francisko:Waraka wa Kitume: Dekano wa Baraza la Makardinali

Baba Mtakatifu amechapisha Barua binafsi ya Kitume, yaani: “Motu proprio” kwa kutoa Sheria mpya zinazoratibu shughuli za Dekano wa Baraza la Makardinali kukaa madarakani. Baba Mtakatifu kwa kusoma alama za nyakati anasema Makardinali wanayo dhamana kubwa ya kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro sanjari na kumsaidia katika utume wake kwa ajili ya huduma ya Kanisa la Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Kardinali Angelo Sodano la kutaka kung’atuka kutoka madarakani kama Dekano wa Baraza la Makardinali, baada ya kutimiza umri wa miaka 92 tangu kuzaliwa na baada ya kuwaongoza Makardinali wenzake tangu mwaka 2005. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu amechapisha Barua binafsi ya Kitume, yaani: “Motu proprio” kwa kutoa Sheria, Kanuni na Taratibu mpya ambazo kuanzia sasa zitakuwa zinaratibu shughuli za Dekano wa Baraza la Makardinali. Baba Mtakatifu kwa kusoma alama za nyakati anasema Makardinali wanayo dhamana kubwa ya kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro sanjari na kumsaidia katika utume wake kwa ajili ya huduma ya Kanisa la Kristo. Kunako mwaka 1965, Mtakatifu Paulo VI alifanya marekebisho makubwa kwa kuwaingiza katika Baraza la Makardinali hata Mapatriaki kutoka katika Makanisa ya Mashariki waliokuwa wamepewa hadhi ya kuwa Makardinali.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mwaka 2018 alipanua Baraza la Makardinali kwa kuwaingiza pia Makardinali wakuu wa Mabaraza ya Kipapa pamoja na Mapatriaki wenye hadhi ya Ukardinali. Dekano wa Makardinali na Makamu wake, wamekuwa wakitekeleza dhamana na wajibu wao wa kidugu kati ya Makardinali wenzao ambao pia kisheria, ndio wenye uwezo wa kuwachagua kushika madaraka haya kwa ajili ya utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anampongeza Kardinali Angelo Sodano kwa kuongoza Baraza la Makardinali kwa takribani miaka 15 sasa. Kutokana na ongezeko la idadi ya Makardinali, dhamana na utume wa Dekano wa Makardinali umeendelea kuwa ni utume mzito. Dekano wa Baraza la Makardinali ataendelea kuchaguliwa na Makardinali wenzake mintarafu Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa namba 352§2 na ataendelea kuwemo madarakani kwa muda wa kipindi cha miaka mitano. Baada ya muda wake kumalizika, ataitwa Dekano Mstaafu. Dekano wa Baraza la Makardinali anaweza pia kuchaguliwa kuendelea kuongoza kwa awamu ya pili. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutumia fursa hii, kuwatakia heri na baraka Makardinali wote wa Kanisa Katoliki kwa huduma na msaada wanaopatia kwa ajili ya kuliongoza Kanisa Katoliki.

Dekano wa Makardinali
21 December 2019, 15:17