Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wasanii ambao wameamua kutumia karama zao ili kuchangia juhudi za maboresho ya elimu Ukanda wa Amazonia kwa mwaka 2019 Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wasanii ambao wameamua kutumia karama zao ili kuchangia juhudi za maboresho ya elimu Ukanda wa Amazonia kwa mwaka 2019 

Papa Francisko: Sanaa na Elimu vishirikiane na kushikamana!

Mama Kanisa anawahamasisha watu wote wa Mungu kujizatiti katika mchakato wa ujenzi wa dunia kama kijiji cha elimu, ili kuwawezesha wakazi wake wawe ni wajenzi wa mtandao wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu, dawa mchunguti inayoganga na kuponya mifumo yote ya ubaguzi na utengano. Katika kijiji hiki, elimu na sanaa ya maonesho vinakutana na kusaidiana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Mama Kanisa anawaalika watu wote wa Mungu kushikamana katika mchakato wa ujenzi wa dunia kama kijiji cha elimu, ili kuwawezesha wakazi wake wawe ni wajenzi wa mtandao wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu, dawa mchunguti inayoganga na kuponya mifumo yote ya ubaguzi na utengano. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 13 Desemba 2019, kwa wasanii wanaoshiriki katika Tamasha la 27 la Muziki wa Noeli kwa Mwaka 2019 hapa mjini Vatican ili kuchangia miradi ya elimu kwa watoto wanaoishi katika Ukanda wa Amazonia, kama kielelezo cha mshikamano wa upendo. Fedha itakayopatikana pamoja na mambo mengine, itaelekezwa zaidi katika mradi wa upandaji wa miti. Tamasha limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki Hizi ni juhudi zinazotekelezwa na Mfuko wa Utume wa Wasalesiani wa Don Bosco pamoja na Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" iliyoanzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 baada ya uzoefu na mang'amuzi yake huko nchini Argentina.

Kwa sasa inapania kuendelea kuwa ni mahali pa utambulisho wa vijana katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia: Injili ya maisha, kukuza elimu na kudumisha malezi bora kwa kujenga utamaduni wa watu tofauti kukutana na kusherekea zawadi ya uhai, kila mtu akiwa na utambulisho wake makini unaojionesha wazi, kwani maisha ni jambo zito. Kumbe, zoezi la upandaji wa miti ni sehemu ya mchakato wa wongofu wa kiekolojia ili kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamduni wa kifo! Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wakati huu wa Kipindi cha Majilio, kutafakari kuhusu kiu ya ndani ya nyoyo zao inayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, anayetaka kukutana na waja wake, ili hatimaye, kuzima kiu na matamanio yao halali. Mwenyezi Mungu anataka kuzima kiu ya haki, amani, uhuru na upendo kamili. Pango la Noeli anasema Baba Mtakatifu ni kielelezo cha upendo wa Mungu; zawadi ya maisha inayokumbatia udugu na urafiki unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye pia ana uwezo wa kuwasamehe watu dhambi zao na kuwaweka huru!

Injili na Pango la Noeli ni msaada mkubwa katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho, kwa kugusa nyoyo za watu na hivyo kuwazamisha katika historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu husika. Huu ni mwaliko wa “kugusa na kuhisi umaskini wa Mwana wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, ili kuchuchumilia na kuambata njia ya unyenyekevu, ufukara na sadaka ili kufuata ile njia kutoka mjini Bethelehemu hadi mlimani Kalvari. Waamini wanaalikwa kukutana na kumhudumia Kristo Yesu anayejitambulisha na ndugu zake maskini na wahitaji zaidi. Fumbo la Umwilisho linastaajabisha na kushangaza sana. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano. Walimwengu wanatamani kuona ushuhuda wa uzuri wa ukweli, chemchemi ya furaha ya kweli inayodumu na kuendelea kuuunganisha vizazi baada ya vizazi na hivyo kuwawezesha kushirikishana maajabu yanayoibuliwa ulimwenguni.

Ni katika mazingira haya, Mama Kanisa anawahamasisha watu wote wa Mungu kujizatiti katika mchakato wa ujenzi wa dunia kama kijiji cha elimu, ili kuwawezesha wakazi wake wawe ni wajenzi wa mtandao wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu, dawa mchunguti inayoganga na kuponya mifumo yote ya ubaguzi na utengano. Katika kijiji hiki, elimu na sanaa ya maonesho vinakutana na kukumbatiana kama kielelezo cha kipaji cha ubunifu wa kibinadamu ili kuunda njia zitakazodumisha udugu wa kibinadamu; majadiliano ya kidini na kiekumene. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" kwa kuendelea kujizatiti katika mchakato wa upandaji miti Ukanda wa Amazonia, kama kielelezo cha huduma. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia heri na baraka katika shughuli zao pamoja na mwendelezo mwema wa safari ya maisha ya kiroho, ili hatimaye, kukutana na Fumbo la Umwilisho, ili kuwashirikisha wasikilizaji wao huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.

Papa: Wasanii
14 December 2019, 16:26