Papa Francisko amekutana na Jumuiya ya Seminari ya Kipapa ya kanda ya  Flaminio Benedetto XV kutoka Bologna inayoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Papa Francisko amekutana na Jumuiya ya Seminari ya Kipapa ya kanda ya Flaminio Benedetto XV kutoka Bologna inayoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. 

Papa Francisko: Seminari ni nyumba ya sala, masomo na umoja

Baba Mtakatifu Francisko anasema hii ni fursa adhimu ya kutafakari juu ya uzuri na utakatifu wa wito na maisha ya Kipadre, kama wawakilishi wa Kristo Yesu mchungaji mwema, kati ya waja wake. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amepembua kuhusu umuhimu wa Seminari katika mambo makuu matatu; Maisha ya sala, nyumba ya masomo na nyumbe ya umoja na mshikamano wa dhati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri limechapisha mwongozo wa malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Sura ya Pili ya Mwongozo huu inapembua kwa kina na mapana kanuni msingi za maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre: Yaani wanapaswa kuunganika na Kristo ili kuwaongoza, kuwachunga na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wanapaswa kuungana na Kristo Yesu katika maisha, upendo na ukweli kwa ajili ya wokovu wa watu na kuendelea kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia. Dhamana ya Kanisa ni kulea, kusindikiza na kupalilia miito mitakatifu, lakini kwa namna ya pekee wito wa Daraja Takatifu. Seminari ndogo na nyumba za malezi ni mahali pa kulea na kuwasindikiza vijana katika maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Hapa waseminari wadogo wanapaswa kupewa malezi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kukazia majiundo ya kiakili, kiroho, kiutu na kimaadili.

Seminari ni mahali pa kukuza ukomavu, umoja na mshikamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Neno la Mungu na Mashauri ya Kiinjili. Walezi wawe kweli ni mashuhuda wa Injili ya Kristo! Mwongozo pia unaangalia wito kwa Daraja takatifu wa watu wenye umri mkubwa, wasaidiwe na kupatiwa malezi makini katika nyumba maalum, ili waweze hatimaye, kufanya maamuzi muhimu katika maisha yao! Kanisa linaangalia pia wito wa Kipadre unaoweza kuibuka miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji na jinsi ya kuwasaidia vijana wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 9 Desemba 2019 amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Seminari ya Kanda ya Flaminio kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Seminari hii chini ya uongozi wa Papa Pio X. Maadhimisho haya anasema Baba Mtakatifu ni fursa adhimu ya kutafakari juu ya uzuri na utakatifu wa wito na maisha ya Kipadre, zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama wawakilishi wa Kristo Yesu mchungaji mwema, kati ya waja wake.

Baba Mtakatifu katika hotuba kuhusu malezi na makuzi ya maisha na wito wa mapadre amegusia umuhimu wa Seminari katika mambo makuu matatu; Maisha ya sala, nyumba ya masomo na nyumbe ya umoja na mshikamano wa dhati. Waseminari watambue kwamba, wanaitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kati ya watu walioko kwenye Ukanda wao. Hawa ni watu wanaokabiliana na changamoto mbali mbali za maisha. Ni watu wanaosubiri kuimarishwa katika imani, matumaini na mapendo. Imani inajengwa na kuimarishwa katika sala ambayo ni chachu ya umoja na mshikamano wa mtu binafsi na Kristo Yesu. Kumbe, Seminari ni nyumba ya sala, ambamo Kristo Yesu anawaita na kuwaalika waja wake, kujitenga kidogo ili kuimarisha mkutano pamoja na kusikiliza kwa makini Neno lake. Waseminari watambue kwamba, wanaandaliwa ili kuwa ni walimu wa watu wa Mungu katika imani ili waweze kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ushupavu na mamlaka.

Wao ni kiungo kinachowaunganisha waamini katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa zinazowaongoza kuelekea kwenye wokovu sanjari na kuwadumisha katika umoja. Ni kutokana na mazingira haya, majandokasisi katika safari ya malezi yao ya kipadre, wanapaswa kutumia muda wa kutosha kwa ajili ya sala, ili kujenga utamaduni wa kumsikiliza Yesu, kukaa na kuonja uwepo wa daima katika tafakari, ili wote wawili waweze kufahamiana kwa kina. Lakini, jambo la msingi ni kukutana na Uso wa Kristo Yesu, anayejifunua na kujitambulisha kwa njia ya maskini. Hii ni sehemu fungamani ya malezi na majiundo ya majandokasisi katika maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, masomo ni sehemu muhimu sana kwa majandokasisi wanaojiandaa kupokea Daraja Takatifu ya Upadre, ili kuimarisha na kupyaisha imani yao. Kwa njia hii, imani yao inakuwa ni imani ya mchungaji mwema. Majandokasisi wanapaswa kujifunza hekima na sayansi mbali mbali ili kuimarisha msingi wa maisha na utume wao kwa siku za usoni.

Hii ni dhamana na wajibu wa mtu mmoja mmoja, lakini kwa kuzingatia kwamba, pembeni mwake, kuna wandani wa safari katika maisha, malezi na makuzi ya kipadre. Hii ni fursa ya kuwaandaa kuweza kujiunga na urika wa mapadre kwa siku za usoni. Majandokasisi watambue kwamba, wanao utume wa kusoma kwa pamoja ili kujichotea hekima, ujuzi na maarifa yanayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu, Taalimungu, Historia ya Kanisa, Sheria za Kanisa pamoja na masomo mbali mbali yanayowekwa mbele yao kama sehemu ya maandalizi kwa siku za usoni. Dhamana na utume huu anasema Baba Mtakatifu Francisko unatekelezwa kwa namna ya pekee na walimu na walezi seminarini. Walezi hawa wanapaswa kuwa  na upeo mpana, makini na huru bila kugubikwa na upendeleo wa aina yoyote ile! Mazingira kama haya ni mahali muafaka panapoweza kuwavutia majandokasisi kusoma kwa bidii, juhudi na maarifa!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Seminari ni nyumba ya ujenzi wa umoja na mshikamano katika misingi ya utu, ukweli na uwazi. Ni mahali ambapo, majandokasisi wanajifunza utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana; kujadiliana katika ukweli na uwazi; tayari kujenga mafungamano ya Kikanisa kumzunguka Askofu mahalia, ambaye amepewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Huu ni udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika utume katika majimbo kadiri ya utambulisho wa watu wa Mungu katika maeneo yao. Huu ni udugu unaoboreshwa kwa uwepo na ushuhuda wa watakatifu lakini zaidi Mapadre watakatifu kutoka katika Kanisa mahalia. Katika muktadha kama huu, Seminari inapata utambulisho wake kama safari ya kuwafunda majandokasisi ili kupima uwezo wao mintarafu Kristo Yesu ambaye ni Kuhani milele yote na mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, ushuhuda, umoja na mshikamano; mambo msingi yanayohitajika kwa ajili ya huduma makini katika Fumbo la Kanisa na utume wake ulimwenguni.

Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni mfano bora wa kuigwa kutokana na utii kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Ni Mama aliyeonesha unyenyekevu na ujasiri kwa mpango wa upendo ambao Mwenyezi Mungu alikuwa ameuweka mbele yake. Daima aliunganika na Kristo Yesu tangu alipotungwa mimba hadi pale alipoinamisha kichwa na kukata roho, Mlimani Kalvari. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awasaidie majandokasisi kila siku ya maisha yao, kugundua hazina iliyofichika, yaani Kristo Yesu na Ufalme wake, ili hatimaye, waweze kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa furaha ya Injili. Seminarini ni mahali pa kujifunza na kukuza Ibada kwa Bikira Maria, tayari kumpokea kama Mama kama alivyofanya Mtakatifu Yohane, Mtume.

Papa: Seminari

 

 

09 December 2019, 15:27