Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asema, Kristo Yesu ni neema na zawadi ya Mungu inayopaswa kupokelewa kwa moyo mkuu na shukrani. Baba Mtakatifu Francisko asema, Kristo Yesu ni neema na zawadi ya Mungu inayopaswa kupokelewa kwa moyo mkuu na shukrani.  (ANSA)

Papa Francisko: Mkesha wa Sherehe ya Noeli: Yesu ni neema na zawadi ya Mungu

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, Kesha la Noeli 2019 amejielekeza zaidi katika kufafanua kuhusu Neema ya Mungu, umuhimu wa waamini kuipokea neema hii kama zawadi, tayari kwa waamini kuonesha moyo wa shukrani ili hatimaye, hata wao wenyewe waweze kuwa ni zawadi ya Mungu kwa jirani zao. Kila mtu anayo zawadi kwa ajili ya kumpatia Mtoto Yesu! Neema na Zawadi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu na utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote. Hii ndiyo neema ya Mungu inayoleta chemchemi ya wokovu kwa watu wote na katika kesha la Sherehe ya Noeli, neema hii imewang’aria watu wote. Huu ndio upendo wa Mungu unaowafumbata na kuwaambata wote, kiasi cha kuwa ni chachu ya mabadiliko katika maisha, historia na kwamba, ni upendo unaowakomboa wanadamu kutoka katika dhambi na kuwakirimia amani na furaha ya kweli. Ni katika kesha la Noeli, Mwenyezi Mungu ameamua kujifunua kwa waja wake kwa njia ya Kristo Yesu. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Yesu amejinyenyekesha na kujifanya kuwa mdogo na kuzaliwa kama Mtoto, ili aweze kuwakumbatia watu wote kama kielelezo cha sadaka kuu inayobubujika kutoka katika mantiki ya Mwenyezi Mungu, kinyume kabisa na ufahamu wa binadamu. Hakuna chochote kile ambacho mwanadamu anaweza kutenda ili kulipia fidia ya gharama ya Fumbo la Umwilisho.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, katika Kesha la Noeli, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumanne, tarehe 24 Desemba 2019. Baba Mtakatifu katika tafakari yake amejielekeza zaidi katika kufafanua kuhusu Neema ya Mungu, umuhimu wa waamini kuipokea neema hii kama zawadi, tayari kwa waamini kuonesha moyo wa shukrani ili hatimaye, hata wao wenyewe waweze kuwa ni zawadi ya Mungu kwa jirani zao. Kila mtu anayo zawadi kwa ajili ya kumpatia Mtoto Yesu! Baba Mtakatifu anasema, neema hii ni upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye amekuja kukaa kati pamoja na waja wake, ili kuwaonjesha upendo wake wa daima. Mwenyezi Mungu anafahamu kupenda pasi na masharti kwa sababu kila mwanadamu ni wa pekee sana machoni pake.

Upendo wa Mungu hautegemei hali au utakatifu wa mtu, kwa sababu Mungu kwa hakika ni mwema. Hata katika hali ya ulegevu na kuanguka dhambini, Mwenyezi Mungu bado anabaki kuwa ni mwaminifu na mvumilivu. Sherehe ya Noeli ni fursa kwa waamini kutambua sadaka na wema wa Mungu katika maisha. Utukufu wa Mungu na uwepo wake mwanana si tishio kwa sababu ni kiini cha uwepo wao. Fumbo la Umwilisho ni kumbu kumbu ya upendo wake usiokuwa na kifani kiasi hata cha kuthubutu kuutwaa ubinadamu kwa milele yote! Neema ya Mungu ni sawa na uzuri wake unaowawezesha wanadamu kutambua kwamba kwa hakika wanapendwa na Mungu katika hali zao zote. Wakiwa wenye afya njema au wagonjwa; wenye furaha au huzuni moyoni, daima ni watu wanaopendeza mbele ya Mungu.

Wachungaji kondeni ambao kwa hakika hawakuwa watakatifu, walitangaziwa furaha kuu inayoendelea kuwaambata na kuwakumbatia waamini wa nyakati hizi hata katika udhaifu wao wa kibinadamu, kwa sababu tu, Mwenyezi Mungu anawapenda upeo na anataka kuwaambia kwamba, hawana sababu ya kuogopa. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha ujasiri, imani na matumaini na kwamba, kwa kupenda hakuna kinachoweza kupotea. Hii inatokana na sababu kwamba, upendo hushinda hofu; matumaini mapya yamefunuliwa kwa njia ya mwanga angavu wa Mungu ambaye ameshinda giza na kiburi cha mwanadamu. Baba Mtakatifu anawakumbusha watu kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda upeo ndiyo maana amefanyika mwili kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, ili kuambatana nao na hivyo kuwaondolea upweke!

Katika muktadha wa zawadi hii kubwa, waamini wanaalikwa kuipokea kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amepiga hatua ya kwanza kuwatafuta waja wake na wala si kwa nguvu na uwezo wao wa kibinadamu. Neema ya Mungu ambayo ni Kristo Yesu mwenyewe, ndiye Mkombozi wa Ulimwengu. Waamini wamwangalie Mtoto Yesu na kumwachia nafasi ili aweze kuwafunika kwa wema na upendo wake wa daima. Kwa njia hii, hawataweza kuwa tena na sababu za kuogopa kupendwa hata kama mambo yanakwenda kombo katika maisha; Kanisa hali inazorota na kile ambacho walimwengu wanapenda na kukishabikia hakitaweza tena kuhesabiwa haki. Yote, haya ni mambo ambayo yatawekwa kando, kwa sababu ya upendo wa Yesu ni chemchemi ya upole na inayoonesha ukaribu. Sherehe ya Noeli ni muda muafaka wa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili kuonja upendo wake usiokuwa na kifani; upendo uliomsukuma kuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, zawadi kubwa kama hii inahitaji kupokelewa kwa moyo wa shukrani; kwa kujikita katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kwa kutembelea mapango ya Noeli, Ishara ya kushangaza na kustaajabisha ili hatimaye, kumwambia Mwenyezi Mungu, asante sana. Kwa kumpokea Kristo Yesu kama zawadi, waamini nao wanahamasishwa kujisadaka, ili waweze hata wao kuwa ni zawadi kwa jirani zao, ili kutoa maana halisi ya maisha. Hii ndiyo njia muafaka ya kuweza kuleta mageuzi makubwa ulimwenguni. Waamini wanapofanya mabadiliko ya dhati katika maisha yao, Kanisa linabadilika, historia inapyaishwa kwa sababu chachu ya mageuzi inapaswa kuanza katika maisha ya mtu binafsi. Kristo Yesu ameweza kubadili historia ya ulimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya waja wake, changamoto na mwaliko hata kwa waamini pia.

Waamini kamwe wasisubiri kuona Kanisa ambalo ni kamilifu sana, ili kuweza kulipenda na wala jirani zake, kuwaona kuwa ni watu wanaostahili kuhudumiwa. Waamini wawe watu wa kwanza kupiga hatua kama kielelezo cha kumpokea Kristo Yesu kama zawadi kubwa inayohitaji kupewa shukrani. Na hii ndiyo chemchemi ya utakatifu wa maisha kwa kuendelea kuhifadhi zawadi hii ambayo ni sadaka kubwa! Katika Simulizi za kale kuhusiana na Sherehe ya Noeli zinaonesha kwamba, wachungaji kondeni, walipoguswa na ile furaha kubwa, kila mtu aliondoka kwa haraka na kuchukua zawadi kadiri ya kazi yake. Lakini kwa bahati mbaya, anasema Baba Mtakatifu, kati ya wale wachungaji wa kondeni, kulikuwepo na mchungaji ambaye hali yake ilikuwa mbaya sana kutokana umaskini, kiasi kwamba, alikuwa anaona haya kujichanganya na wafugaji wengine. Katika hali na mazingira haya, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walijikuta wakiwa katika hali ngumu ya kuweza kupokea zawadi zote kwa mkupuo.

Bikira Maria alipomwona yule mchungaji akiwa mikono mitupu, alimwita na kumkabidhi Mtoto Yesu mikononi mwake! Mchungaji yule akatambua moyoni mwake kwamba, amepokea zawadi kubwa ambayo kwa hakika kamwe hakustahili kupewa katika maisha na historia yake. Mikono yake iliyoonekana kuwa si mali kitu, ikageuka kuwa ni mahali pa faraja kwa Mtoto Yesu, akahisi moyoni mwake, kupendwa kupita kiasi. Na kutokana na furaha hii, akaanza kumwonesha Mtoto Yesu kwa wachungaji wengine. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, hata kama mikono ya waamini wengi inaonekana kuwa tupu, lakini Mwenyezi Mungu anaangalia moyo ambao unahitaji upendo wa dhati na hivyo kesha la Noeli linakuwa ni zawadi kwa watu kama hawa. Kwa sababu nuru kuu na utukufu wa Bwana umewang’aria ili hata wao waweze kung’ara katika maisha. Kumbe, waamini wakubali kumpokea Mtoto Yesu, ili waweze kung’ara kwa nuru ya Noeli.

Papa: Kesha la Noeli
25 December 2019, 15:51