Tafuta

Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali ametoa salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu kwa niaba ya Makardinali wote kwa Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre. Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali ametoa salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu kwa niaba ya Makardinali wote kwa Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre. 

Papa Francisko: Miaka 50 ya Daraja: Salam za Makardinali

Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali kwa niaba ya Makardinali, ameungana na Baba Mtakatifu Francisko kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani "Te Deum laudamus, Te Dominum confitemur!” kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe 13 Desemba 1969 mikononi mwa Hayati Askofu mkuu Ramón José Castellano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 13 Desemba 2019 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, kumbu kumbu ya Mtakatifu Lucia, Bikira na Shahidi, lakini hakutoa mahubiri katika Ibada hii ya Misa Takatifu. Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali kwa niaba ya Makardinali wote ameungana na Baba Mtakatifu Francisko kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani "Te Deum laudamus, Te Dominum confitemur!”  kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe 13 Desemba 1969 mikononi mwa Hayati Askofu mkuu Ramón José Castellano huku akiwa amezungukwa na umati mkubwa wa Wayesuit, wanashirika wenzake. Kama ilivyokuwa wakati ule, Makardinali wanaungana pamoja naye katika sala ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa neema, rehema na baraka ambazo amemkirimia Baba Mtakatifu.

Kunako mwaka 1992, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu, ushuhuda wa zawadi na fumbo la Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Daraja Takatifu ya Upadre ni fumbo ambalo linamwezesha Mwenyezi Mungu kuwateuwa baadhi ya waamini ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wakleri wanakumbushwa daima kwamba, si wao waliomchagua yeye, bali ni yeye aliyewachagua wao na kuwaweka kwenda kuzaa matunda, na matunda yao yapate kukaa. Makardinali wanampongeza Baba Mtakatifu kwa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini chemchemi ya dhamana hii ni wito wa Kipadre. Makardinali wanasema, wanaendelea kumsindikiza kwa sala na sadaka zao ili aweze kutekeleza vyema dhamana na utume wa kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, lakini zaidi kwa kuwaimaarisha katika imani. Wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Sodano
13 December 2019, 17:13