Tafuta

Vatican News
Katiba ya Kitume "Veritatis gaudium" yaani "Furaha ta ukweli" ilidhinishwa na Papa Francisko tarehe 8 Desemba 2017 na kuchapishwa tarehe 29 Januari 2019. Katiba ya Kitume "Veritatis gaudium" yaani "Furaha ta ukweli" ilidhinishwa na Papa Francisko tarehe 8 Desemba 2017 na kuchapishwa tarehe 29 Januari 2019. 

Katiba ya Kitume: Veritatis gaudium: Furaha ya ukweli!

Katiba hii ni mwongozo na mbinu mkakati katika mageuzi ya elimu inayopania kumpatia mwanadamu furaha ya ukweli unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu ambaye ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu; ni njia, ukweli na uzima. Ni kiungo muhimu cha umoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu kwani Roho Mtakatifu ni: Roho wa ukweli na upendo; uhuru, haki na umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” iliyoidhinishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Desemba 2017, na kuchapishwa rasmi tarehe 29 Januari 2018 ni mwongozo makini unaovihusu vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuongozwa na Kanisa Katoliki, kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa yanayowagusa na kuwaambata watu wa Mungu katika mwelekeo mzima wa utekelezaji wa utume wa uinjilishaji mpya. Hii ni dhamana inayojikita katika mang’amuzi, utakaso na mageuzi ya dhati yanayopania kupyaisha mfumo mzima wa elimu inayotolewa na Mama Kanisa katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu. Katiba hii ni mwongozo na mbinu mkakati katika mageuzi ya elimu inayopania kumpatia mwanadamu furaha ya ukweli katika maisha yake. Hii ni “Furaha ya ukweli” unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu ambaye ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu; ni njia, ukweli na uzima. Ni kiungo muhimu cha umoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na umoja kati ya watoto wa Mungu, kwani Roho Mtakatifu ni: Roho wa ukweli na upendo; uhuru, haki na umoja.

Uinjilishaji na utamadunisho ni chanda na pete katika maisha na utume wa Kanisa unaojikita pia katika majadiliano na tamaduni mbali mbali kwa kusoma alama za nyakati, ili kuliwezesha Kanisa kujipyaisha zaidi kama walivyokazia Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao wa “Optatam totius” yaani “Mwongozo wa Malezi ya Kipadre” kwa kuzingatia uhamasishaji wa miito na majiundo makini ya Mapadre, ili kuwawezesha kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa, kwa kumfuasa Kristo Mchungaji mwema anayewapatia: utambulisho, tasaufi na utume wanaopaswa kuutekeleza katika mwanga wa “Furaha ya ukweli”. Kuna matatizo na changamoto nyingi zinazowakumba wakleri na kwamba, Kanisa halina budi kusoma alama za nyakati, kwa kuibua mbinu na mikakati mipya itakayoliwezesha Kanisa kuendelea kuwa ulimwenguni pamoja na kutekeleza dhamana yake ya Uinjilishaji, katika misingi ya ukweli na uwazi. Kanisa linatambua kwamba, katika miaka ya hivi karibuni limetikiswa kwa kashfa mbali mbali, lakini bado limeendelea kusherehekea vipindi vya umoja na furaha, kwa kuonesha uzuri wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Katika mwanga wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1979, alichapisha Waraka wa Kitume “Sapientia christiana” yaani “Hekima ya Kikristo” ulioboresha kwa uangalifu mkubwa dhamana na utume wa Kanisa kwenye vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa ili kuweza kutekeleza kwa dhati kabisa utume wa uinjilishaji ambao kimsingi unafumbatwa katika ufunuo wa Kikristo. Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” imeyazingatia yote haya na kuyapyaisha zaidi ili kuliwezesha Kanisa kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii katika ulimwengu mamboleo na katika kutekeleza utume wake wa utangazaji na ushuhuda wa Furaha ya Injili unaotekelezwa na watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walikazia umuhimu wa kujifunza Maandiko Matakatifu kiini na msingi wa taalimungu, ushiriki mkamilifu wa Liturujia ya Kanisa, moyo wa maisha na utume wa Kanisa. Kanisa limeendelea kukazia pia umuhimu wa Katekesi makini kama sehemu ya majiundo ya awali na endelevu ya watu wa Mungu na kwamba, maendeleo endelevu ya watu ni sehemu muhimu sana wa maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Mtakatifu Yohane Paulo II, katika Waraka wake wa kitume “Fides et ratio” “akapigilia msumari tena” kwa kukazia umuhimu wa majadiliano ya kina kati ya masomo ya falsafa na taalimungu ili kuwawezesha watu wa Mungu kuwa na uelewa mpana zaidi kuhusu hekima ya Kikristo bila kusahau dhamana ya utamadunisho, ili “Furaha ya ukweli” iweze kuzama katika tamaduni, mila na desturi za watu kwa kusafisha yale yote yanayosigana na tunu msingi za Kiinjili! Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” anasema, nyaraka zote za kitume zilizotolewa na watangulizi wake, Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ni nyaraka zinazopania kuliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake katika ulimwengu mamboleo kwa kukazia utu na heshima ya binadamu; uhusiano, mafungamano pamoja na mshikamano wa kimataifa, ili kuwawezesha watu kulifahamu Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kanisa la Kristo Yesu ni alama na chombo cha kutangaza na kushuhudia ukweli huu. Kanisa linapenda kuunganisha hatua mbali mbali za uelewa wa binadamu, kitaalimungu, kifalsafa, kijamii na kisayansi, ili kukuza na kudumisha utamaduni wa upendo sanjari na kuwaandaa viongozi wabunifu watakaonesha dira na mwongozo wa kufuatwa hali inayohitaji ujasiri mkubwa wa mageuzi ya kitamaduni, changamoto inayoweza kutekelezwa na mtandao wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa sehemu mbali mbali za dunia mintarafu mwanga wa Injili na Mapokeo hai ya Kanisa. VIGEZO MUHIMU: Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” anatoa vigezo muhimu vinavyopaswa kuzingatiwa kwani lengo ni kujenga na kukuza umoja na udugu, upendo na mshikamano, daima maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza! Hii ndiyo dhamana ya umissionari wa Kanisa linatoka kifua mbele ili kuinjilisha na kutamadunisha mintarafu furaha ya ukweli wa Kikristo! Kigezo cha pili ni majadiliano katika ukweli na uwazi mintarafu mwanga wa Injili na Mafundisho ya Kanisa ili kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana.

Kigezo cha tatu ni mwingiliano makini wa masomo mbali mbali yanayotolewa na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu kwa kuzingatia ubunifu kadiri ya mwanga wa Ufunuo. Majiundo, tafiti, mbinu za ufundishaji na maudhui yanayotolewa yanapaswa kuzingatia Ufunuo na Utume wa Kanisa katika dhamana ya uinjilishaji. Mkazo unaotolewa na Mababa wa Kanisa katika mfumo wa elimu unajikita katika mambo makuu manne yaani: umoja wa kisayansi, mawasiliano ya utakatifu, maisha adili na umwilishaji wa upendo katika maisha ya watu mambo yanayobubujika kutoka katika Neno la Mungu, vinginevyo, sayansi haina mizizi na wala kamwe haiwezi kuacha kumbu kumbu hai katika akili na nyoyo za vijana wa kizazi kipya! Sayansi na utakatifu ni sawa na “uji kwa mgonjwa”. Kigezo cha nne ni kuunda mtandao wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ili kuweza kufanya upembuzi yakinifu katika shida, changamoto na hatimaye kuibua suluhu ya mambo yote haya mintarafu mwanga wa Injili, kwa kuwa na mradi wa pamoja unaotekelezwa na Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume! Lengo ni kufahamu matatizo haya na hatimaye, kuyapatia maana na ufumbuzi wake kadiri ya mwanga wa Injili, Mapokeo ya Kanisa Uinjilishaji na Utamadunisho. Maboresho yote haya yanapania kutangaza ukweli wa Injili bila kubezwa ukweli wa mambo na mafao yake kwa wengi.

Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zifanye tafiti katika medani mbali mbali za maisha ya watu: kiuchumi, kijamii, kitamaduni na kisayansi ili kuweza kuwa na maamuzi yanayowajibisha; kwa kutumia vyema rasilimali fedha na watu katika tafiti pamoja na kukuza majadiliano kati ya Kanisa na ulimwengu wa sayansi kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya watu wa Mungu, daima Kanisa likipania kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kupenyeza ukweli katika maisha ya watu binafsi na jamii katika ujumla wake! Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” anasema, changamoto mamboleo zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa zinajikita hasa zaidi katika tamaduni, maisha ya kiroho na katika mfumo mzima wa elimu unaohitaji kupyaishwa zaidi bila ya kukata tamaa kwa kuendelea kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu, mhimili mkuu wa utume na dhamana ya uinjilishaji ndani ya Kanisa.

SHERIA ZA JUMLA: Baba Mtakatifu anafafanua kuhusu: Asili na hatima ya Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu za Kanisa ambazo zinapaswa kusaidia mchakato wa uinjilishaji kwa njia ya tafiti ili kutangaza na kushuhudia furaha ya ukweli wa imani unaotamadunishwa katika mazingira mbali mbali ya maisha ya watu wa Mungu. Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yanayo dhamana ya kusimamia maisha na ukuaji wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu za Kikanisa kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na Vatican chini ya usimamizi na uratibu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa majaaalimu wenye sifa na wa kutosha katika vitivo mbali mbali kwa kuzingatia ufahamu na utajiri wao wa ujuzi na maarifa; ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo na Kikanisa, wawe ni watu wanao wajibika barabara. Majaalimu wawe na vyeti vinavyowawezesha kufundisha masomo hayo, kwa kuwa na viambata vya tafiti, machapisho mbali mbali na uwezo wa kufundisha na wanafunzi kuelewa! Majaalimu wawe waadilifu, makini katika Mafundisho Tanzu ya Kanisa, watu wanaoipenda taaluma yao, kiasi hata cha kujisadaka ili kuliwezesha Kanisa kutoa elimu makini.

Kanisa pia linaruhusu Majaalimu wasio Wakatoliki kufundisha masomo maalum kadiri ya weledi, ujuzi na maarifa yao. Pale ambapo majaalimu wanakosa sifa na vigezo, waondolewe mara moja kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu zilizopo. Majaalimu wanaofundisha imani na maadili watambue dhamana na wajibu wao na kwamba, wanapaswa kutekeleza utume huu kwa kuwa na muungano thabiti na Mafundisho ya Kanisa na umoja kamili na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya Kanisa ziko wazi kwa wanafunzi wote wenye sifa zinazohitajika na kwamba, mkazo wa elimu uwekwe kwenye Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican bila kusahau mchango unaotolewa na tafiti mbali mbali katika kukabiliana na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Mbinu, tafiti na ufundishaji lazima ziboreshwe mara kwa mara kwa kusoma alama za nyakati. Watafiti wapewe uhuru wa kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao, kwa kuzingatia ukweli, hekima pasi na haraka ili kuweka mlinganyo mzuri kati ya matokeo ya kisayansi na mahitaji ya kichungaji ya watu wa Mungu.

Taasisi za kitaalimungu zinao wajibu wa kutoa Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Ukweli mfunuliwa unaojikita katika imani na uelewa wa binadamu “faith and reason”, ili kuwasaidia watu wa Mungu kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya umoja katika kweli zote mintarafu falasafa na tamaduni za watu husika, daima imani ya Kikristo ipewe kipaumbele cha kwanza! Majadiliano ya kiekumene na kidini yafundishwe kwa uangalifu mkubwa, ili kukabiliana na ukanimungu unaojitokeza katika nyakati hizi. Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Amana na Utajiri wa Kanisa katika imani, Sheria za Kanisa, Falsafa na Taalimungu yatolewe kwa kuzingatia mzunguko wa masomo, ili hatimaye, kuweza kuwaandaa wanafunzi kufanya tafiti yakinifu katika masomo yao katika hali ya utulivu na ukomavu. Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” anatoa pia sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kufuatwa na kutekelezwa na vitivo mbali mbali, vyeti vinavyotolewa, usimamizi na uratibu wa rasilimali fedha; mbinu mkakati wa mipango na ushirikiano, uongozi na serikali za vyuo vikuu na taasisi za elimu ya Kanisa.

Sheria hizi zimeanza kutumika kati ya Mwaka 2018-2019 katika mwaka wa kwanza wa masomo kwa mwaka 2019, kwa kutegemeana na kalenda ya masomo ya vyuo vikuu na taasisi za elimu ya Kanisa. Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinapaswa kuwasilisha marekebisho ya Katiba na miongozo ya masomo kabla ya tarehe 8 Desemba 2019. Katiba hii imepitishwa “Ad Experimentum” na Baba Mtakatifu Francisko ili iweze kufanyiwa majaribio kwa muda wa miaka mitatu. Lakini, vyuo vikuu na taasisi za elimu ya Kanisa zinazoshirikiana na serikali mbali mbali zinaweza kupewa muda mrefu zaidi kwa kupata kibali kutoka kwenye Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki.

Veritatis Gaudium
09 December 2019, 15:49