Papa Francisko: Kanisa linawajibu na dhamana ya kushughulikia migogoro na kinzani za kifamilia kwa ajili ya ustawi na mafao ya familia husika. Papa Francisko: Kanisa linawajibu na dhamana ya kushughulikia migogoro na kinzani za kifamilia kwa ajili ya ustawi na mafao ya familia husika. 

Papa Francisko: Migogoro ya ndoa na familia! Kanisa linawajibika kuishughulikia!

Papa Francisko anasema, mbele ya wanandoa wanaoteseka kutokana na madonda ya maisha ya ndoa na familia Kanisa kama ilivyokuwa katika historia yake, halina budi kuonesha moyo wa upendo na mshikamano; kwa kuonja shida na magumu wanayokabiliana nayo, ili hatimaye, kuwawezesha kuzima kiu ya amani na furaha ya kweli kama mtu binafsi na kama wanandoa katika ujumla wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” umegawanyika katika sura tisa zenye utangulizi mfupi, kwa kuonesha mchango mkubwa uliotolewa na Mababa wa Sinodi ya familia, mchango ambao unapaswa kutunzwa kama amana na hazina ya Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, si majadiliano yote mintarafu Mafundisho tanzu ya Kanisa, maadili au shughuli za kichungaji yanapaswa kujadiliwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, bali mambo mengine yanahitaji kupatiwa ufumbuzi makini kadiri ya mila, tamaduni na changamoto mahalia. Hii inatokana na ukweli kwamba, mila na tamaduni za watu zinatofautiana, kumbe, hapa kuna haja ya kutamadunisha changamoto hizi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kadiri ya mwanga na tunu za kweli za Kiinjili. Wosia huu wa Kitume ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo.

Wosia huu wa Kitume unatoa mwelekeo wa Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Ni waraka unaokazia upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka na kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Anawataka wazazi na walezi kuimarisha elimu na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza, kung’amua na kuwasaidia wanafamilia wanaolegalega katika maisha na wito wao. Baba Mtakatifu anachambua kwa kina na mapana tasaufi ya maisha ya ndoa na familia! Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alikutana na kuzungumza na washiriki wa kozi maalum kuhusu: Utunzaji wa ndoa na huduma ya kichungaji kwa wanandoa waliojeruhiwa katika maisha na utume wao.

Katika kozi hii, washiriki walipata nafasi ya kupembua kwa kina na mapana taalimungu ya maisha ya ndoa na familia; sheria, taratibu na kanuni za maisha ya ndoa na famlia sanjari na maisha ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anasema, mbele ya wanandoa wanaoteseka kutokana na madonda ya maisha ya ndoa na familia, Kanisa kama ilivyokuwa katika historia yake, halina budi kuonesha moyo wa upendo na mshikamano; kwa kuonja shida na magumu wanayokabiliana nayo, ili hatimaye, kuwawezesha kuzima kiu ya amani, utulivu na furaha ya kweli kama mtu binafsi na kama wanandoa katika ujumla wao. Mipasuko na majeraha ya maisha ya ndoa na familia ni matokeo ya sababu mbali mbali katika maisha kwa mfano haya ni masuala: kisaikolojia, kimwili, kimazingira na kitamaduni na wakati mwingine ni matokeo ya binadamu kujifungia katika ubinafsi wake na kushindwa kupokea zawadi ya upendo.

Katika muktadha huu unaowaonesha wanandoa wakichuruzika damu kutokana na madonda ya ndoa na familia si rahisi kwa Kanisa kuweza kuwageuzia kisogo na kujifanya kana kwamba hakuna kinachoendelea. Mama Kanisa anapaswa kuonesha mshikamano wa dhati na wale wote wanaoteseka na kuomboleza kutokana na majeraha ya ndoa na familia zao. Katika mazingira kama haya, Kanisa litafute ukweli wa upendo wao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Kanisa, daima likitafuta mafao ya watu wa ndoa. Hii ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuwakirimia watoto wake. Katika ushuhuda wa kesi za watu wa ndoa zinazoendeshwa na Mama Kanisa, mashuhuda wanapaswa kwanza kabisa kujiaminisha chini ya ulinzi na maongozi ya Roho Mtakatifu, ili wasikilize kwa umakini sana, wapate vigezo muhimu, wafanye mang’amuzi na hatimaye, kutoa hukumu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, mchakato huu ni tete na wala si “maji kwa glasi”.

Kanisa linapaswa kuwa makini ili kuwasaidia wanandoa kudumisha maisha yao ya ndoa mintarafu Mafundisho ya Kanisa kama ambavyo Mtakatifu Paulo anavyofafanua uhusiano kati ya Kristo Yesu na mchumba wake Kanisa, ambaye amejisadaka hata kufa kwa ajili yake pale Msalabani. Kwa njia hii, mapenzi ya Mungu kwa ajili ya familia nzima ya binadamu yakatendeka. Maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa yanapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha. Huu ni mwaliko wa kutembea kwa pamoja na Kanisa ndani ya Kanisa kwa kujikita na kuambata njia ya utakatifu wa maisha. Ndoa kadiri ya Agano Jipya ni safari ya imani. Kumbe, familia  ya Kikristo inapata chimbuko lake katika maisha ya ndoa ambayo ni ushirikiano wa agano la upendo kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika hija hii ya maisha ya kiroho kuna haja kuwa na wachungaji watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasaidia wandoa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao.

Ndoa na familia ni utume unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ndoa; unapaswa kukita mizizi yake katika ari na mwamko wa kimisionari; ili kuwawezesha wanandoa kuwa wakarimu, tayari kupokea maisha mapya kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ili wanandoa waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao, wanapaswa kupata maandalizi makini yanayogusa masuala ya kisaikolojia, upendo wa dhati, mahusiano na mafungamano yao katika maisha ya unyumba ili kuwasaidia kupata ukomavu  na hatimaye udumifu katika maisha yao. Wanandoa na familia wanapaswa kukuza na kudumisha ndani mwao wito wa ndoa, ili hatimaye, kusimama kidete, kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya ndoa na familia katika mazingira ya kifamilia, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla wake. Wanandoa wanapaswa kutangaza na kushuhudua uzuri, utakatifu na ukuu wa maisha ya ndoa na familia kama kielelezo chenye mvuto na mashiko.

Maisha ya ndoa na familia ni ushuhuda wa ufunuo wa upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Mababa wa Mtaguso wa Pili wa Vatican wanabainisha umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya ndoa na familia, kwa kuwa na mwelekeo, ari na mwamko wa kimisionari. Ni katika muktadha huu, wanandoa wanapaswa kujizatiti katika sala, kwa kushiriki kikamilifu maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho; kwa kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa mwenzi wake wa ndoa katika ukweli, uwazi na uaminifu, ili kweli familia yao iweze kuwa ni shule ya utakatifu, haki na amani; kitovu cha uinjilishaji, maadili na utu wema. Parokia hazina budi kuwasaidia wanandoa kuishi vyema wito na utume wao ndani ya Kanisa. Mchakato huu wa maisha na utume wa wanandoa ni tete lakini unawezekana kutekelezwa. Baba Mtakifu anapenda kuwatia shime wakleri kujizatiti kuwasaidia, kuwaunga mkono na kuwasindikiza wanandoa ili kulisaidia Kanisa kupyaisha  maisha na utume wake, kwa kujenga na kudumisha mtandao wa jumuiya na familia ambazo ni mashuhuda na wamisionari wa Injili ya familia.

Papa: Rota Romana

10 December 2019, 16:15