Vatican News
Papa Francisko anasema, Machapisho ya Padre Miguel Angel Fiorito ni utajiri na amana kubwa kwa maisha na utume wa Kanisa zima! Papa Francisko anasema, Machapisho ya Padre Miguel Angel Fiorito ni utajiri na amana kubwa kwa maisha na utume wa Kanisa zima!  (Vatican Media)

Papa Francisko Miaka 50 ya Jubilei ya Upadre: Machapisho ya Padre Miguel Angel Fiorito 1916-2005

Baba Mtakatifu amegusia historia ya Padre Miguel Ángel Fiorito na mchango wake katika malezi na makuzi ya maisha yake ya kiroho. Ni Padre aliyekirimiwa karama ya machozi, kielelezo cha faraja ya maisha ya kiroho. Alikuwa ni mwalimu wa majadiliano, aliyetumia vyema karama yake ya kufundisha ili kuwafunda wafuasi mitume, wenye ari na mwamko wa kutangaza na kushuhudia Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, hapo tarehe 13 Desemba 2019 amezindua machapisho ya Padre Miguel Ángel Fiorito (1916-2005), ambaye alikuwa baba yake wa maisha ya kiroho na kwa miaka kadhaa alikuwa ni Mkurugenzi wa Jarida la “La Civilità Cattolica". Tukio hili limehudhuriwa na Wayesuit. Padre Arturo Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika la Wayesuit, Padre Antonio Spadaro, Mkurugenzi wa Jarida la "La Civilità Cattolica" pamoja na Padre José Luis Narvaja, aliyehariri Vitabu Vitano (Escritos) vya Padre Miguel Ángel Fiorito, wamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo na huduma yake makini kwa ajili ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amemtaja Padre Miguel Ángel Fiorito kuwa ni Baba wa majadiliano, asiyefahamika na wengi, lakini ni mtu mashuhuri sana kwa maisha na tafakari zake, zilizowawezesha wasikilizaji wake, kujitambua na hivyo kujitosa kikamilifu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Padre Fiorito aliwasaidia Wayesuit wengi kufanya mang’amuzi kuhusu maisha na wito wao, akajenga ari na mwamko wa shule, mahali pa kujenga umoja na mshikamano wa kijumuiya; kwa kukuza na kuendeleza karama na mapaji mbali mbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wake. Uwepo wake miongoni mwao anasema Baba Mtakatifu ni alama ya shukrani kwa yote ambayo Shirika limemtendea na angependa kubaki akiwa ni mtumishi mwaminifu pasi na makuu katika maisha yake yote! Machapisho ya Padre Miguel Ángel Fiorito  ni amana na utajiri mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa zima. Baba Mtakatifu amegusia historia ya Padre Miguel Ángel Fiorito na mchango wake katika malezi na makuzi ya maisha yake ya kiroho, pamoja na watu mbali mbali waliogusa na kumfunda kwa namna ya pekee katika maisha na utume wa Kipadre. Kwa hakika alikuwa ni Padre aliyekirimiwa karama ya machozi, kielelezo cha faraja ya maisha ya kiroho.

Padre Fiorito alikuwa ni mwalimu wa majadiliano, aliyetumia vyema karama yake ya kufundisha “Munus docendi” ili kuwafunda wafuasi mitume, wenye ari na mwamko wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Alikuwa ni chombo makini cha upendo na huruma ya Mungu, kutokana na uvumilivu wake akawasaidia vipofu wengi wa maisha ya kiroho, kuweza kuona njia tena kwa kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao. Alikuwa ni kiongozi ambaye hakupenda kujitambulisha na makundi ya kisiasa, lakini alipenda wasikilizaji wake kukuza na kudumisha dhamiri nyofu ili kuchagua jema la kufuata na baya la kuachana nalo! Alipenda kuimarisha majadiliano ya kijumuiya kwa kuwasaidia wanajumuiya wengi kushiriki katika majadiliano hayo. Alikuwa ni mtu wa sala iliyomwilishwa katika matendo. Alijenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kutafakari na kutafuta majibu kwa ajili ya kuganga kinzani na mipasuko ambayo ilijitokeza katika jumuiya.

Alitoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya ujenzi wa amani na utulivu wa ndani. Padre Miguel Ángel Fiorito alikuwa ni mtu mnyenyekevu na asiyependa makuu. Alikuwa ni kiongozi mwenye utaratibu katika masomo, sala na shughuli za kichungaji. Maktaba yake ilikuwa kama duka la dawa ya huruma na upendo wa Mungu. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu kwamba, Padre Miguel Ángel Fiorito alikuwa ni mtu mkarimu sana na kamwe hakuwa na haraka ya maisha. Alipenda kuwasaidia Wayesuit kufanya tathmini na upembuzi wa kina kuhusu matatizo, changamoto na fursa walizokuwa nazo mbele yao kabla ya kuwatwisha watu wengine lawama mambo aliyoyafanya kwa upole na upendo mkuu. Uvumilivu na upole vikawa ni vinasaba na utambulisho wa Padre Miguel Ángel Fiorito. Ni mfuasi misionari aliyeonesha ukomavu wa imani, matumaini na mapendo, akawa kama mwerezi wa Lebanoni uliopandwa kando ya maji ya utulivu na matunda yake yakazaa wafuasi wa mafungo ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Kumbe, Machapisho yake yataendelea kuzamisha mizizi na matunda yatapatikana kwa wakati wake.

Papa: Wayesuit
15 December 2019, 11:22