Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Desemba 2019 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Desemba 2019 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. 

Papa Francisko: Miaka 50 ya Daraja Takatifu: Huduma kwa Mungu na watu wake!

Tarehe 13 Desemba 2019, Papa Francisko anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre: 13 Desemba 1969 na chimbuko la wito wake ni Siku kuu ya Mtakatifu Mathayo, alipoonja kwa karibu zaidi huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake, kiasi cha kufanya maamuzi magumu ya kuacha yote na kuanza kumfuasa Kristo Yesu katika maisha na wito wa Kipadre.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Kumbu kumbu ya Mtakatifu Lucia, Bikira na Shahidi inaadhimishwa na Mama Kanisa Ijumaa, tarehe 13 Desemba 2019. Hiki ni kilele cha kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, yaani tarehe 13 Desemba 1969 na chimbuko la wito wake ni katika Siku kuu ya Mtakatifu Mathayo, alipoonja kwa namna ya pekee huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake, kiasi cha kufanya maamuzi magumu ya kuacha yote na kuanza kumfuasa Kristo Yesu katika maisha na wito wa Kipadre. Baba Mtakatifu katika wito na maisha yake ya Kipadre amekazia sana umuhimu wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu; Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa kwa sababu Kristo Yesu ndiye chemchemu ya upendo kwa waja wake.

Wakleri wanakumbushwa kwamba, kabla hata ya kuwekewa mikono na kuwa ni: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu,  wao kimsingi ni: waamini waliobatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu na kwamba, utambulisho wao wa kwanza ni waamini na wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa kuwekwa wakfu katika Sakramenti ya Daraja Takatifu wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Kwa namna ya pekee,  ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Huu ndio urithi unaojikita katika Mafundisho tanzu ya Mama Kanisa. Ni ukweli ambao wakleri wanapaswa kuumwilisha katika maisha na utume wao kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Padre daima anapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake na kwamba, Ibada kwa Bikira Maria inawawezesha wakleri kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria, ili kweli waweze kuwa wafuasi na mitume hodari wa Kristo Yesu kwa kusikiliza na kutenda kama alivyokuwa Bikira Maria. Daima amekumbusha kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, ni watu wanaopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Katika historia na maisha ya Kanisa kuna wakleri ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili yakutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili sehemu mbali mbali za dunia, lakini kutokana pia na udhaifu wa binadamu, kuna baadhi ya wakleri wametumbukia katika kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo na hivyo kuchafua maisha na utume wa Kanisa. Katika shida, mahangaiko na majaribu ya maisha, wakleri wakumbuke, ile siku ya kwanza kabisa walipokutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre ni muda wa kufanya toba na kuomba msamaha; kusifu, kushukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha na wito wa Kipadre, bila kusahau wema na ukarimu anaoendelea kuwatendea wahudumu wa Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma kwa waja wake. Yote haya yanadhihirisha wema na huruma ya Mungu kwa wakleri wake hata kama wakati mwingine wanaelemewa na udhaifu wao wa kibinadamu, lakini bado Mwenyezi Mungu anaendelea kubaki kuwa mwema na mwaminifu kwa ahadi zake. Wakleri watambue kwamba, wao kwanza kabisa wameguswa kwa wema na huruma ya Mungu katika wito na maisha yao, changamoto ya kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Upendo wa Mungu usaidie mchakato wa kupyaisha maisha ya kikasisi yanayoambata toba, wongofu wa ndani, utakatifu wa maisha, furaha, huruma na upendo kwa Mungu na jirani.

Wakleri kwa namna ya pekee wameitwa na kutumwa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kumbe, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya yanayovunjilia mbali ubinafsi ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema kwamba, anaguswa sana na mchoko pamoja na upweke wa Mapadre na kwamba, hawa ni wahudumu wa Injili ambao hawana mbadala! Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za Kanisa; ni viongozi wa Jumuiya ya waamini waliokabidhiwa kwao, lakini zaidi wanapaswa kuwa ni mwandani wa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anawapongeza Mapadre wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa; wanaoteseka na kuhangaika kutokana na sababu mbali mbali. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwasindikiza Mapadre wao kwa njia sala na majitoleo yao, ili kweli wajisikie kwamba, wanasaidiwa na kufarijika kutokana na urafiki wao wa dhati na Kristo Yesu pamoja na ndugu zao katika Kristo! Katika shida na mahangaiko yao ya ndani, Mapadre, wasipate kishawishi cha hofu kuhusu maisha na wito wao, bali watambue kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Daraja takatifu, wanashiriki Ukuhani wa Kristo! Kumbe, wao kimsingi ni watu wa Mungu na watumishi wa Kristo Yesu na Kanisa lake! Wao wanatenda kwa niaba ya Kristo “Agunt in persona Christi” kwa njia ya Roho Mtakatifu na hivyo, wanakuwa ni madaraja kati ya Mungu na binadamu kwa njia ya huduma ya Mafumbo ya Kanisa!

Wakleri ni watu wanaoishi si kwa ajili yao binafsi, bali kwa ajili ya jirani zao, lakini zaidi kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Mapadre ni vyombo na mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake, lakini wanapaswa kutambua kwamba, wito na maisha yao yamehifadhiwa katika vyombo vya udongo! “Habemus...thesaurum istum in vasis fictibus, ut sublimitas sit virtutis Dei et non ex nobis” (Rej. 2 Kor. 4:7). Tiba ya magonjwa ya kiroho katika maisha na utume wa Mapadre ni: Sala ya Kanisa ndio msingi wa majadiliano ya maisha ya kiroho kati ya Mapadre na Mwenyezi Mungu, ni nguvu ya maisha ya ndani inayojenga na kuimarisha utashi na dhamiri nyofu. Huu ni mwaliko wa kukuza na kudumisha usafi kamili kama sadaka na utimilifu wa upendo na huduma kwa Mungu, Kanisa sanjari na mpango wa Mungu wa wokovu kwa ulimwengu. Mapadre wakuze na kudumisha umoja, udugu, upendo na mshikamano katika maisha ya kijumuiya, kwani wanaitwa na kutumwa kama Jumuiya na wala si kama mtu binafsi!

Mapadre watambue udhaifu wao wa kibinadamu, karama na neema walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kuweza kuamua na kutenda kwa ukarimu. Mapadre waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, kwa sababu huruma ya Mungu yadumu milele. Moyo wa shukrani ni silaha madhubuti inayowawezesha kutafakari ukarimu wa Mungu katika maisha yao, mshikamano, msamaha, subira, uvumilivu na upendo, kiasi hata cha kuthubutu kusema kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi”, lakini Kristo Yesu akamwambia “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu” kwa sababu huruma yake yadumu milele! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu inayoongozwa na Roho Mtakatifu inayohitaji umoja na ushirikiano wa watoto wake wote! Waamini wote wawe na ujasiri wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kupyaisha maisha yao kwa kukabiliana na changamoto mamboleo kwa mwanga wa Injili.

Mapadre waendelee kujikita katika mchakato wa mageuzi ya Kiliturujia na kwamba, Kanisa liwe ni chombo makini cha huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa liendelee kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Liwe ni chombo cha amani na maridhiano kati ya watu kwa kujikita katika majadiliano ya kiekumene na kidini; ili kudumisha uhuru wa kidini, nguzo msingi ya haki za binadamu. Mapadre wakuze na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kuwafariji na kuwategemeza kwa ulinzi na tunza yake ya kimama!

Papa: Miaka 50 Daraja Takatifu
12 December 2019, 17:31