Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. 

Papa Francisko: Huruma ya Mungu ni vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa

Kanisa linatumwa kumwilisha huruma na upendo katika maisha yake. Kanisa ni chombo na shuhuda wa: furaha, huruma na msamaha. Katika maisha na utume wake, Kanisa kwa nyakati zote, limeendelea kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu, ili kuondokana na kishawishi cha watu kudhani kwamba, wanaweza kujiokoa wenyewe! Huruma ya Mungu ni chachu ya uinjilishaji mpya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Kanisa limeagizwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu inayopaswa kupenya katika sehemu mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Huruma ni daraja inayomkutanisha Mungu na waja wake, kiasi cha kuonja upendo wake usiokuwa na mipaka. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kupyaisha sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa ni shuhuda na mhudumu wa huruma ya Mungu katika maisha ya watu wa Mungu mintarafu Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu. Huruma ni msingi thabiti wa uhai na maisha ya Kanisa unaopaswa kujidhihirisha katika shughuli mbali mbali za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Kanisa linatumwa kumwilisha huruma na upendo katika maisha na vipaumbele vyake.

Kanisa ni chombo na shuhuda wa: furaha, huruma na msamaha wa Mungu kwa binadamu. Katika maisha na utume wake, Kanisa kwa nyakati zote, limeendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu, ili kuondokana na kishawishi cha watu kudhani kwamba, wanaweza kujiokoa wenyewe! Huruma ya Mungu ni chachu ya uinjilishaji mpya. Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 13 Desemba 2019 alipokutana na kuzungumza na mashirika na vyama vya kitume kutoka Ufaransa vinavyojihusisha na matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama sehemu ya mbinu mkakati wa kumwilisha Injili ya huruma kati ya watu. Kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, wanachama wa vyama vya kitume nchini Ufaransa wameendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia utamaduni wa Injili ya huruma ya Mungu, ili kuzima kiu ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Ili kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, waamini wanapaswa kuwa na amani na utulivu wa ndani unaobubujika kutokana na huduma wanayoitoa kwa ndugu, jirani na hasa maskini. Kwani hawa ni watu wanaopaswa kusikilizwa kwa makini, kuheshimiwa, kuthaminiwa na kupendwa, tayari kuwashika mkono na kuwainua kwa kuzingatia utu, heshima na haki zao msingi. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa ni mitume wa huruma ya Mungu kwa njia ya unyenyekevu pamoja na nia njema, mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika kipindi hiki cha Majilio, kuelekea katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, Baba Mtakatifu anawaalika kufanya tafakari ya kina kuhusu Pango kama ishara ya kushangaza na kustaajabisha kutokana na uwepo wa Mungu ambao ni chachu ya mabadiliko makubwa yanayoleta matumaini pamoja na kukuza utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Pango la Noeli anasema Baba Mtakatifu ni kielelezo cha upendo wa Mungu; zawadi ya maisha inayokumbatia udugu na urafiki unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye pia ana uwezo wa kuwasamehe watu dhambi zao na kuwaweka huru! Injili na Pango la Noeli ni msaada mkubwa katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho, kwa kugusa nyoyo za watu na hivyo kuwazamisha katika historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. Huu ni mwaliko wa “kugusa na kuhisi umaskini wa Mwana wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, ili kuchuchumilia na kuambata njia ya unyenyekevu, ufukara na sadaka ili kufuata ile njia kutoka mjini Bethelehemu hadi mlimani Kalvari. Waamini wanaalikwa kukutana na kumhudumia Kristo Yesu anayejitambulisha na ndugu zake maskini na wahitaji zaidi.

Papa: Ufaransa
13 December 2019, 16:53