Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anasema, wanawake walei wanayo dhamana na utume maalum kwa maisha ya Kanisa la Kristo! Papa Francisko anasema, wanawake walei wanayo dhamana na utume maalum kwa maisha ya Kanisa la Kristo!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Dhamana na utume wa wanawake walei ndani ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 14 Desemba 2019 amekutana na kuzungumza na Wanawake Wasaidizi Majimboni na wale wanaojisadaka katika shughuli za kichungaji na kitume kwenye Jimbo kuu la Milano, Padua na Treviso; utume ambao ulianzia Jimbo kuu la Milano wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Battista Montini, anayejulikana na wengi kama Mtakatifu Paulo VI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kuona kwamba, bado mfumo dume unaendelea kutawala na kuwanyanyasa wanawake kana kwamba, wao ni watu wa daraja la pili duniani! Kuna wanawake wengi ambao wanatumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Haya ni mambo yanayodhalilisha utu, heshima na haki zao msingi. Wanawake wanayo dhamana na utume katika jamii na Kanisa katika ujumla wake. Wana utajiri na karama nyingi zinazopaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Chuki, uhasama na mauaji ya wanawake ni mambo ambayo yamepitwa na wakati. Wanawake wana karama ya kuvumilia mateso kwa ajili ya ustawi wa watoto wao pamoja na kuendeleza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anasema kuna mifano ya wanawake wengi ambao wanaendelea kujisadaka kama vyombo na mashuhuda wa upendo kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake sehemu mbali mbali za duniani.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 14 Desemba 2019 amekutana na kuzungumza na Wanawake Wasaidizi Majimboni na wale wanaojisadaka katika shughuli za kichungaji na kitume kwenye Jimbo kuu la Milano, Padua na Treviso; utume ambao ulianzia Jimbo kuu la Milano wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Battista Montini, anayejulikana na wengi kama Mtakatifu Paulo VI. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia umuhimu wa waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kushirikiana na kufungamana na viongozi wa Kanisa na kwamba vyama vya kitume vina mchango mkubwa katika kuimarisha Jumuiya za Kikanisa. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, kati ya wafuasi wake wa karibu, walikuwepo pia wanawake waliofuatana naye katika mahubiri yake. Wanawake waliokuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa. Kati yao ni Mariamu aitwaye Magdalena aliyekuwa na imani na upendo mkuu kwa Kristo Yesu, kiasi cha kuwa ni mfuasi wa kwanza kushuhudia Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Akawa ni mtume kwa mitume wa Yesu ili kuwatangazia kwamba, Kristo Yesu, amefufuka. Ndiyo maana wanawake hawa wasaidizi majimboni na washiriki katika utekelezaji wa shughuli mbali mbali za kitume, wanaitwa “Wawanawake wa Ufufuko”.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, walei, ama kwa kujitolea kwa hiari ama kwa kualikwa kufanya kazi na kushirikiana moja kwa moja na utume wa kihierarkia, wanatenda kazi chini ya uongozi mkuu wa Hierarkia yenyewe, ambayo yaweza kuidhinisha ushirikiano huo kwa njia ya agizo rasmi “mandatum”. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanaonesha umuhimu wa kushirikiana na waamini walei katika shughuli mbali mbali za kitume, kichungaji na katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kazi hii ni nyeti na wakati mwingine ni ngumu sana. Roho Mtakatifu anawakirimia waamini karama mbali mbali kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, changamoto na mwaliko kwa wakleri kufanya mang’amuzi ya kina kama ilivyotokea kwa Jimbo kuu la Milano, Treviso, Padua na Vicenza. Huu ni utume na wala si ajira. Kumbe, viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa macho, kuwapokea, kuwatambua na kuwapatia mfumo wa utambulisho wao katika Jimbo husika, ili waweze kushirikiana kwa karibu zaidi na Askofu mahalia.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, utume ni uchu kwa ajili ya Kristo Yesu na watu wake, kwa kuona kina cha upendo wake unaowainua, kuwategemeza na kuwakumbatia wote. Kristo Yesu anataka kuwatumia waamini walei kuwavuta watu wake wote. Kristo anawachagua na kuwatuma kwa waja wake. Kumbe, huu ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya kutaka kujifungia katika ubinafsi; kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo Yesu ametumwa na Baba yake wa mbinguni ili kuwaokoa watu wa nyumba ya Israeli, kiasi cha kujisadaka kwa ajili ya Kondoo wake. Baba Mtakatifu anahitimisha kwa kusema kwamba, uaminifu una gharama zake, ni tete kama ulivyo Msalaba, lakini ni chemchemi ya maisha mapya kadiri ya mpango wa Mungu. Amewashukuru kwa ushuhuda wa maisha na utume wao na kuwataka kusonga mbele kwa imani na matumaini, huku wakishuhudia ile furaha ya mateso na ufufuko wa Kristo Yesu miongoni mwa ndugu zao.

Papa: Wanawake
14 December 2019, 16:49