Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawahimiza waamini kuwa ni mashuhuda amini wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Papa Francisko anawahimiza waamini kuwa ni mashuhuda amini wa Kristo Yesu na Kanisa lake.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Wakristo iweni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake!

tarehe 13 Septemba 2019 Kanisa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Lucia, Bikira na Shahidi. Hii itakuwa pia ni kilele cha kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, yaani tarehe 13 Desemba 1969 na chimbuko la wito wake ni katika Siku kuu ya Mtakatifu Mathayo, alipoonja kwa namna ya pekee huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake kuhusu safari ya Injili Duniani, Jumatano tarehe 11 Desemba 2019 ambamo amegusia ushuhuda wa imani ya Mtakatifu Paulo, Mtume aliyethubutu kuyaangalia mateso yake kwa mwanga wa imani, amewataka vijana wa kizazi kipya kuwa na jeuri kama hii katika maisha yao. Kipindi cha Majilio, iwe ni fursa makini kwa waamini kuweza kupyaisha tena imani yao kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Huyu ndiye Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu anayekuja kuwakomboa watu kutoka katika lindi la utumwa wa dhambi na mauti. Wajiaminishe daima kwa Kristo ili aweze kuwasaidia kuwa waaminifu kwa wito na maisha yao ya Kikristo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Mfufuka. Wakumbuke daima kwamba, kamwe, kifo, nyanyaso, dhuluma na mateso hayataweza kuwatenganisha na upendo wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo, kumbe wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Imani yao iwe ni mwanga angavu wa kuwaangazia wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao hapa duniani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwa ni kiongozi na dira ya maisha yao. Ijumaa, tarehe 13 Desemba 2019 Kanisa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Lucia, Bikira na Shahidi. Hii itakuwa pia ni kilele cha kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, yaani tarehe 13 Desemba 1969 na chimbuko la wito wake ni katika Siku kuu ya Mtakatifu Mathayo, alipoonja kwa namna ya pekee huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake, kiasi cha kufanya maamuzi magumu ya kuacha yote na kuanza kumfuasa Kristo Yesu katika maisha na wito wa Kipadre.

Papa: Mwaliko kwa waamini

 

 

11 December 2019, 15:39