Tafuta

Mwenyeheri James Alfred Miller, wa Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo awe ni chemchemi ya haki, amani na mshikamano nchini Guatemala Mwenyeheri James Alfred Miller, wa Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo awe ni chemchemi ya haki, amani na mshikamano nchini Guatemala 

Mwenyeheri James Alfred Miller: Shuhuda wa imani katika huduma!

Br. James Alfred Miller, wa Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo, FSC, ametangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo, FSC, linaadhimisha Jubilei ya Miaka 300 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle. Br. Miller alizaliwa mwaka 1944, huko, USA. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, akaweka nadhiri za daima kunako tarehe 12 Juni 1969.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 8 Desemba 2019, aliyaelekeza mawazo yake nchini Guatemala, ambako, Kardinali Josè Luis Lacunza Maestrojuàn Jumamosi, tarehe 7 Desemba 2019 kwa niaba ya Baba Mtakatifu amemtangaza Mtumishi wa Mungu Br. James Alfred Miller, wa Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo, FSC, kuwa ni Mwenyeheri. Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo, FSC, linaadhimisha Jubilei ya Miaka 300 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle. Br. Miller alizaliwa tarehe 21 Septemba 1944, huko Marekani. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, akaweka nadhiri za daima kunako tarehe 12 Juni 1969. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua dhamana na mchango wa Watawa hawa akautangaza Mwaka 2019 kuwa ni mwaka wa Jubilei ya Watawa wa Shule za Kikristo. Katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 300 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle, muasisi wa Shirika hili, wameendelea kuwa waaminifu kutekeleza dhamana na wito wao ndani ya Kanisa kwa: ukarimu na uaminifu wa Kiinjili.

Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle ana mchango mkubwa katika sekta ya elimu, kwani kwa mfano na ushuhuda wake, ameisaidia jamii kuzingatia mambo makuu matatu: Dhana ya shule; Uelewa wa mwalimu pamoja na Mbinu za ufundishaji. Huu ni mwaliko wa kujenga utamaduni wa watu kukutana, ili kuwashirikisha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, amana na utajiri wa Habari Njema ya Wokovu! Mwaka wa Jubilei ya miaka 300 imekuwa ni fursa ya kumwangalia tena na tena Kristo Yesu kama dira ya maisha, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini, kwa kutangaza Habari Njema kwa njia ya elimu inayomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili. Kwa mfano wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle pamoja na maongozi ya Roho Mtakatifu, wamefanikiwa kupyaisha ari yao kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa kugundua pia njia mpya za maisha na utume wao! Kumbe, kutangazwa kwa Br. James Alfred Miller  kuwa Mwenyeheri, ni ushuhuda wa imani tendaji, iliyompelekea hata kunako mwaka 1982 kuuwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Guatamela.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika ujana wake, Br. James Alfred Miller akayamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, chemchemi ya huduma makini kwa watu wa Mungu nchini Guatemala. Mwenyeheri Br. James Alfred Miller awe ni chemchemi ya haki, amani na mshikamano nchini Guatemala. Ni mtawa aliyejisadaka kuwafundisha vijana katakesi ya kina, kwa fedha ya ruzuku ya Serikali ya Guatemala, akafanikiwa kujenga shule 10 huko vijijini, ili kuwasaidia “watoto wa wakulima” kupata elimu, ujuzi na maarifa ya kuweza kupambana na hali pamoja na mazingira yake, kwa kuwahakikishia leo na kesho iliyo bora zaidi. Kutokana na wivu pamoja na kijicho kisichokuwa na mashiko kutoka ndani ya Shirika na Guatemala katika ujumla wake, Mwenyeheri Br. James Alfred Miller mwaka 1979 akalazimika kurejea nchini Marekani. Mwaka 1981 akatumwa tena nchini Guatemala, lakini hali ya kisiasa ilikuwa tete sana na huo ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyoacha ukakasi mkubwa hata katika maisha na utume wa Kanisa.

Akauwawa kikatili tarehe 13 Februari 1982 wakati alipokuwa akisimamia ujenzi wa shule. Licha ya hali ya wasi wasi na uchungu mkubwa, umati mkubwa wa waamini kutoka sehemu mbali mbali za Huehuetenango huko Guatemala wakahudhuria mazishi yake. Kwa upande wake, Bruda Robert Schieler, Mkuu wa Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo anasema, wako huru, kuvuka mipaka inayotenganisha nchi hata mipaka ya kijamii na kisiasa. Wamekuwa ni watangazaji na mashuhuda wa maisha ya wakfu kwa njia ya elimu inayokomboa; kwa kuwaendea wale walioko pembezoni mwa jamii; waliosahauliwa na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, ili wote hawa waweze kushiriki furaha ya Injili na matumaini kwa wale waliokata tamaa! Bruda Robert Schieler anasema, wanaendelea kufuata nyayo za muasisi wao wa kuambatana na maskini kwa ajili ya maskini kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaotekelezwa kwa njia ya elimu makini.

Katika utekelezaji wa huduma hii kwa watu wa Mungu, watawa hawa wanaendelea kushirikiana na watu mbali mbali wanaojisadaka kwa ukarimu na weledi ili kutekeleza utume huu katika sekta ya elimu. Ni watu wanaoshiriki pia amana na utajiri wa maisha ya kiroho, daima Kristo Yesu akipewa kipaumbele cha kwanza. Kwa njia hii, wanaendelea kuandika ukurasa mpya wa simulizi ya Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle. Wanaitwa na Kanisa pamoja na kusukumwa na tunu msingi za Kiinjili kugusa akili na nyoyo za watu, ili kuwaonjesha upendo hai wa Kristo Yesu kwa kuimarisha mafungamano kati ya mwalimu na mwanafunzi, ili kweli darasa liweze kuwa ni mahali pa ukombozi wa watu wa Mungu. Hii ni tasaufi inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu; huduma makini kwa jirani na mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, bila kuwasahau vijana wa kizazi kipya wanaohitaji msaada wao.

Lengo ni kutangaza na kushuhudia uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Uwepo wao katika sekta ya elimu ni kama Sakramenti ya ufunuo wa Mungu, mahali pa kukutana na Kristo Mfufuka kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Watawa hawa wanasukumwa kujibu kilio cha watu ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, kwa njia ya elimu wanaweza kuinuka na kusonga mbele kama watoto wa Mungu.

Papa: Mwenyeheri James

 

 

08 December 2019, 15:47