Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kilio, mateso na mahangaiko ya watoto wadogo sehemu mbali mbali za dunia yanamfikia Mungu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, kilio, mateso na mahangaiko ya watoto wadogo sehemu mbali mbali za dunia yanamfikia Mungu! 

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Desemba 2019: Kilio cha watoto wadogo kinafika mbinguni!

Kuzaliwa kwa Mtoto Yesu kuwakumbushe tena walimwengu kwamba, kila mtoto anayetengwa, kunyanyaswa na kuonewa; kila mtoto anayekosa elimu na huduma bora ya afya, ni kilio kinachomwelekea Mwenyezi Mungu. Katika mtandao kuna picha za video zinazoonesha jinsi ambavyo watoto sehemu mbali mbali za dunia wanavyokabiliana na shida na mahangaiko mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali na wanadiplomasia wakati wa hija yake ya kitume nchini Thailand alisema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa kwa Mwaka 2019 inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 30 ya Tamko la Haki ya Mtoto Duniani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za watoto; utu na heshima yao kama binadamu. Watoto wajengewe mazingira mazuri ya maisha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho, kimwili, kisaikolojia na kiakili. Matumaini ya kesho iliyo bora zaidi yanafumbatwa kwa namna ya pekee, katika huduma kwa watoto. Leo hii jamii inawahitaji wajenzi wa ukarimu, watu wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani katika familia ya binadamu kwa kuzama zaidi katika misingi ya haki, mshikamano, udugu wa kibinadamu na utulivu. Kila mmoja anapaswa kuchangia katika: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu katika salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” kwa Noeli ya Mwaka 2019, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwangalia na kumtafakari Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Anasema, kuna giza, kinzani na mipasuko ya kiuchumi, kijiografia na kiekolojia, lakini mwanga angavu wa Kristo Yesu bado unang’ara zaidi. Ni matamanio ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kristo Yesu, atakuwa ni mwanga angavu wa watoto wengi wanaoteseka kutokana na vita na kinzani huko Mashariki ya Kati na sehemu mbali mbali za dunia. Kila mtoto anayeteseka, ikumbukwe kwamba, kilio na mateso yake yanamfikia Mwenyezi Mungu. Hii ni sehemu ya Nia za Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwezi Desemba 2019. Nia zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha pekee kwa watoto, ili kuweza kuwaandalia leo na kesho yenye matumaini bora zaidi.

Nia hii ya Baba Mtakatifu inajikita zaidi katika mazingira ya Sherehe ya Noeli, yaani Kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, ili kuwakumbusha tena walimwengu kwamba, kila mtoto anayetengwa, kudhulumiwa, kunyanyaswa na kuonewa; kila mtoto anayekosa fursa ya elimu na huduma bora ya afya, ni kilio kinachomwelekea Mwenyezi Mungu. Katika mtandao huu, kuna picha za video zinazoonesha jinsi ambavyo watoto sehemu mbali mbali za dunia wanavyokabiliana na shida na mahangaiko mbali mbali. Baba Mtakatifu anasema, Mtoto Yesu aliyezaliwa Pangoni kule mjini Bethlehemu ni changamoto na mwaliko kwa kila Serikali na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, kutoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto hawa kwa kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Katika mateso na mahangaiko ya watoto sehemu mbali mbali za dunia, kati yao yuko Kristo Yesu anayeteseka pamoja nao!

Papa: Nia Desemba 2019
27 December 2019, 15:23