Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Baba Mtakatifu wakati wa sala ya Malaika wa Bwana Dominika ya tatu ya kipindi cha majilio! Tafakari ya Baba Mtakatifu wakati wa sala ya Malaika wa Bwana Dominika ya tatu ya kipindi cha majilio!  (ANSA)

Kuwa na furaha lakini na utambuzi wa vipindi vyenye mashaka!

Neno la Mungu linatoa mwaliko kwa upande mmoja kuwa na furaha na upande mwingine na utambuzi ya kwamba maisha yaambatana hata na vipindi vya kuwa na mashaka hadi kufikia kuwa na ugumu wa kuamini.Furaha na mashaka ni uzoefu ambao ni sehemu ya maisha yetu.Ni katika tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko kabla ya sala ya Malaika wa Bwana kwa mahujaji na waamini katika Dominika ya tatu ya Majilio 15 Desemba 2019.

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Tarehe 15 Desemba 2019 ikiwa ni Dominika ya tatu ya Majilio, Baba Mtakatifu Francisko ametoa tafakari yake kwa waamini na mahujaji wote waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro kushiriki naye katika sala ya alaika wa Bwana. Akianza tafakari hiyo anasema, “Katika Dominika ya Tatu ya Majilio ambayo inajulikana ya ‘furaha’, Neno la Mungu linatoa mwaliko kwa upande mwingine kuwa na furaha na upande mwingine kuwa na utambuzi kuwa maisha yanavyo ambatana hata na vipindi vya kuwa na mashaka hadi kufikia kuwa na ugumu wa kuamini. Furaha na mashaka, vyote viwili ni uzoefu ambao ni sehemu ya maisha yetu” amethibitisha Baba Mtakatifu.

Mwaliko wa Nabii Isaya ni kinyume na maneno ya Injili. Je  kwa namna gani?

Isaya anatoa mwaliko wa kuwa na  furaha hivyo kwa upande wa Nabii Isaya anasema “Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi”.(35,1). Hii inakwenda kinyume na Injili kutokana na kujitokeza wasiwasi wa Yohane Mbatizaji anayetuma kuuliza Yesu kama: “Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? (Mt 11,3).  Hata hivyo  Baba Mtakatifu Francisko anmebainisha  kuwa, kwa hakika Isaya anatazama upeo zaidi ya hali halisi, kwa maana mbele yake anao watu waliokata tamaa na ambao  anawambia “Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea. 35,3-4).  Hii ndiyo hali halisi ya kila wakati ambayo inatuweka katika majaribu ya imani yetu. Lakini mtu wa Mungu anatazama pia upeo zaidi  kwa maana Roho Mtakatifu anasikika katika moyo wake ile nguvu ya ahadi yake na kutangaza wokovu kwamba: “Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; (…) atakuja na kuwaokoa ninyi”. Na ndipo kila kitu kinabadilika kwa maana jangwa lina chanua maua, faraja na furaha vinatawala katika roho zilizokata tamaa, kiwete, kipofu, kiziwi, wote wanapona (Is 35 5-6).  Na ndicho kinachotimizwa na Yesu, kwa maana vipofu wanapata kuona, viweti wanatembea, wakoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuka na maskini wanatangaziwa Injili. (Mt 11,5).

Maelezo hayo yote yanaonesha wokovu unaomzunguka mwanadamu

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, katika maelezo hayo yote yanaonesha jinsi gani wokovu unamzunguka mwanadamu na kumuunda. Lakini kuzaliwa kwake kwa upya na furaha inayomsindikiza daima inahitaji kujisafisha sisi wenyewe kwa dhambi zilizomo ndani mwetu. Na kwa maana hiyo ndipo kuna haja ya kuwa na uongofu ambao ndiyo msingi wa mahubiri ya Yohane Mbatizaji na Yesu mwenyewe. Kwa namna ya pekee hasa katika hali ya kubadilisha mawazo yetu tuliyo nayo kuhusu Mungu. Ni kipindi sasa cha Majilio ambacho kinachangamotisha na kutoa chachu ya kujiuliza kama Yohane “ Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?”(Mt 11,3).

Tunaalikwa kutambua uso ambao Mungu ameuchagua kujifananisha katika Yesu Kristo

Baba Mtakatifu amewaomba wafikirie katika maisha yake yote, Yohane Mbatizaji alimsubiri Masiha; mtindo wake wa maisha na mwili wake wote ulikuwa umejiundia subira hiyo hiyo. Hata kwa upande wa Yesu, yanasikika maneno haya ya sifa kwake kwamba: “Amin, nawaambieni, Hajatokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye (Mt 11,11). Licha ya hayo Baba Mtakatifu Francisko anasema hata yeye alitakiwa kuongokea Yesu. Kama Yohane Mbatizaji, basi hata sisi tunaalikwa kutambua uso ambao Mungu ameuchagua kujifananisha katika Yesu Kristo, aliye mnyenyekevu na mwenye huruma. Majilio ni kipindi cha neema. Kuna maanisha kwamba haitoshi kuamini katika Mungu tu na badala yake ni lazima kila siku kujitakasa imani yetu.

Jiandae kumpokea japokuwa siyo mtu wa hadithi bali ni Mungu mwokozi

Baba Mtakatifu Francisko amesema kuwa ni kujiandaa  kumpokea japokuwa mapokezi hayo  si kumpokea mtu wa hadithi bali ni Mungu ambaye anatuchangamotisha, anatujumuisha na ambaye mbele yetu tunatakiwa kuwa na uchaguzi mmoja tu. Mtoto ambaye anayelala katika holi la Pango ana uso wa ndugu zetu, kaka na dada wenye kuhitaji, maskini ambao ndiyo fursa ya fumbo hilo  na ambao mara nyingi sehemu kubwa hawawezi kutambua uwepo wa Mungu kati yetu (Waraka Admirabile signum, 6). Bikira Maria atusaidie kwa sababu tunakaribia Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bwana na tusizuiwe na mambo ya kijujuu juu tu, bali tuweze kutoa nafasi ndani ya moyo kwa ajili ya  Yesu ambaye tayari amekwisha kuja na anataka kuja tena ili kuponesha magonjwa na kutupatia furaha yake.

16 December 2019, 15:26