Tafuta

Vatican News
Jarida la "Aggiornamenti Sociali" ni nyenzo muhimu ya majiundo makini ya waamini kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Jarida la "Aggiornamenti Sociali" ni nyenzo muhimu ya majiundo makini ya waamini kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Mafundisho Jamii ya Kanisa chachu ya utakatifu!

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakita mizizi yake katika misingi ya: haki, amani na maridhiano kati ya watu, kwa kuzingatia pia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa kazi ya Uumbaji. Huu ndio mwongozo rasmi wa maisha na utume wa Kanisa katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata katika masuala ya kidini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanafumbatwa katika utu wa binadamu, ustawi, maendeleo fungamani na mafao ya wengi; udugu na mshikamano; ushiriki wa watu katika kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati mintarafu mustakabali wa maisha yao kwa kuzingatia kanuni auni! Ni mafundisho yanayokita mizizi yake hasa katika misingi ya: haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kuzingatia pia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa kazi ya Uumbaji ambayo binadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu. Huu ndio mwongozo rasmi wa maisha na utume wa Kanisa katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata katika masuala ya kidini! Majadiliano hayana budi kuzingatia ukweli na uwazi bila ya kumezwa na kishawishi cha maamuzi mbele. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana; kwa kuheshimiana na kuthamianina hata katika tofauti msingi zinazoweza kujitokeza.

Kusikiliza ni sanaa inayomwezesha mtu kupata ukweli na kuufanyia kazi, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa katika maisha. Ukweli utawaweka watu huru. Kwa kusikiliza, watu wajenge na kuimarisha msingi wa majadiliano ili kupata suluhu ya kudumu katika matatizo na changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza kwa kutumia mwanga wa Injili. Kimsingi, kuna haja ya kufanya mang’amuzi, kuangalia ukweli na hali halisi iliyopo, kusali na kufanya maamuzi. Haya ni mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alipenda kuwashirikisha wafanyakazi wa Jarida la “Aggiornamenti Sociali” linalochapishwa nchini Italia. Anasema, hakuna sababu ya kukata wala kujikatia tamaa, bali kusikiliza kwa makini, kuangalia na hatimaye, kufanya hata wakati mwingine, maamuzi machungu. Hii pia ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha, ukweli na uwazi sanjari na unyenyekevu wa maisha.

Waamini wawe na ari na moyo wa kuthubutu na kamwe wasiogope “kutekeleza na kuanguka”. Ikiwa kama haya yatawapata, wawe na ujasiri wa kusimama na kusonga mbele kwa imani na matumaini, kwa sababu ni sehemu ya ubinadamu. Waamini wajenge utamaduni wa kujiweka wazi mbele ya Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwakirimia uhuru wa ndani ambao ni msingi wa ukweli wa maisha. Kwa upande wao, wafanyakazi wa Jarida la “Aggiornamenti Sociali” wamesisitizia umuhimu wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini. Jarida hili ni kielelezo makini cha uwekezaji unaofanywa na Wayesuit kwa kushirikiana na waamini walei katika maisha na utume wao. Hii ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wao katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Jarida hili lilianzishwa mara tu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kama sehemu ya utume wa Wayesuit katika mchakato wa kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Hii ni huduma inayopania kukuza na kudumisha mchakato wa uinjilishaji na Injili ya Haki kati ya watu wa Mataifa, kwa kujitahidi kuwa ni vyombo vya haki, amani na upatanisho. Jarida hili pamoja na mambo mengine, linaendelea kuragibisha umuhimu wa kumwilisha ekolojia fungamani  katika vipaumbele vya kijamii na kwamba, Waraka wake wa kitume “Laudato si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” umekuwa ni rejea na chachu muhimu katika maisha na utume wao. Lengo ni kukazia ekolojia fungamani inayopania: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jarida linafafanua mambo msingi ya maisha na utume wa Kanisa, linafanya tafiti makini za kisayansi na kumwilisha matokeo yake kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa la Kristo, chini ya usimamizi na uratibu wa Wayesuit. Jarida hili limewekeza kwa kiasi kikubwa katika mitandao ya kijamii kama nyenzo msingi ya malezi na majiundo makini kwa watu wa Mungu. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, Jarida limeendelea kuwekeza zaidi na zaidi katika mchakato wa tafiti pamoja na kuendelea kuwafunda wanasiasa misingi ya maadili na utu wema katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Papa: Jarida
11 December 2019, 14:58