Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Desemba 2019 ameadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe: Ni Mama na Mwombezi wa wote! Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Desemba 2019 ameadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe: Ni Mama na Mwombezi wa wote!  (Vatican Media)

Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe: Mama na mwombezi!

Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa, ambaye daima katika hija ya maisha yake, amekuwa tayari kusadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa jirani zake. Bikira Maria ni Mama wa wote; ni Mama wa Kanisa kwani Kanisa ni bikira na mama na linapaswa kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuuiga utakatifu wa Bikira Maria ili liweze kung'ara kwa utakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Mama Kanisa tarehe 12 Desemba 2019 ameadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, Msimamizi wa Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko, majira ya jioni, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka Amerika ya Kusini. Katika mahubiri yake, amekazia dhamana na utume wa Bikira Maria kama mtume hodari na mwaminifu, Mama na mwombezi wa watu wote, wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora hasa huko nchini Marekani. Kila mwaka, kuna mahujaji zaidi ya milioni 20 wanaofanya hija kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Guadalupe. Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Bikira Maria ni mtume hodari na mwaminifu wa Kristo Yesu, Mwanaye wa pekee na mkombozi wa ulimwengu. Ni Mama ambaye wala hakuwahi kujisikia kuwa ni mkombozi mwenza na Mwanaye Kristo Yesu.

Kumbe, kipaumbele cha kwanza kwa wanataalimungu ni kuweka uzito kwa Umama wa Bikira Maria pamoja na utume wake. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa, ambaye daima katika hija ya maisha yake, amekuwa tayari kusadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa jirani zake. Bikira Maria ni Mama wa wote; ni Mama wa Kanisa kwani Kanisa ni bikira na mama na linapaswa kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuuiga utakatifu wa Bikira Maria, kwa sababu anang’ara kwa fadhila na alibahatika kupenya ndani kabisa ya historia ya wokovu. Ni kielelezo cha upendo wa kimama ambao wanapaswa kuwa nao rohoni wale wote wanaoshiriki katika kazi ya utume wa Kanisa ili watu waweze kuzaliwa upya! Mababa wa Kanisa kwa kutambua ukuu na umama wa Bikira Maria wanafafanua pia umama wa Kanisa katika maisha na utume wake. Bikira Maria ni mfano mtimilifu wa Kanisa.

Bikira Maria ni Mama na mwombezi wa watu wote. Lakini, kamwe watu wasitake kumibinafsisha Bikira Maria ili kujibu matamanio binafsi au kwa kutaka upendeleo fulani. Bikira Maria ni mwombezi wa wote anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kumbe, kwa uwepo, maombezi na tunza yake ya daima, alisaidie Kanisa kuwa kweli ni Mama Mtakatifu, kama alivyo Bikira Maria wa Guadalupe ambaye amekuwa ni mwombezi na Mama wa wote aliyemchukua mimba na hatimaye akamzaa Kristo Yesu, Mungu kweli na mtu kweli. Ibada kwa Bikira Maria wa Guadalupe ilipata chimbuko lake kunako Karne ya XVI, yaani kati ya tarehe 9 – 12 Desemba 1531 Bikira Maria alimtokea Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoazin na huo ukawa ni mwanzo wa wongofu wa Wahindi Wekundu huko Amerika ya Kusini.

Papa: Guadalupe
13 December 2019, 15:56