Papa Francisko asikitishwa na maafa makubwa yaliyosababishwa na kimbunga cha Phanfone, maarufu kama Ursula nchini Ufilippini. Papa Francisko asikitishwa na maafa makubwa yaliyosababishwa na kimbunga cha Phanfone, maarufu kama Ursula nchini Ufilippini. 

Kimbunga cha Phanfone cha sababisha maafa nchini Ufilippini

Kimbunga Phanfone kikiwa kimeambatana na mvua kubwa pamoja upepo mkali, kimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao nchini Ufilippini. Hadi sasa zaidi ya watu 16 wamekwisha kupoteza maisha sanjari na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu ya barabara na majengo. Mawasiliano pamoja na usafiri nchini Ufilippini vimeathirika sana kwa wakati huu. Papa amewakumbuka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kimbunga Phanfone ambacho kwa wananchi wa Ufilippini kinajulikana kama Ursula, ambacho kilikuwa kimeambatana na mvua kubwa pamoja upepo mkali, kimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hadi sasa zaidi ya watu 16 wamekwisha kupoteza maisha sanjari na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu ya barabara na majengo. Mawasiliano pamoja na usafiri nchini Ufilippini vimeathirika sana kwa wakati huu. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Siku kuu ya Mtakatifu Stefano Shemasi na Shahidi, tarehe 26 Desemba 2019 akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameungana na wananchi wa Ufilippini ambao tarehe 25 Desemba 2019 wamekumbwa na kimbunga cha Phanfone. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka Mwaka 2013 kimbunga cha Haiyan kilipelekea zaidi ya watu 7,300 nchini Ufilippini kupoteza maisha.

Baba Mtakatifu amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwaombea wale wote walioathirika kutokana na maafa haya. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa waamini, mahujaji na wageni kutoka ndani na nje ya Italia na wote hawa amewatakia heri na baraka na kwamba, Sherehe ya Noeli ili chemchemi ya furaha, imani na matumaini kwa kuendelea kumtafakari Mtoto Yesu aliyezaliwa Pangoni, Ishara ya kushangaza na kustaajabisha sana. Tafakari hii, ilete msukumo wa kuwapenda na kumhudumia Kristo Yesu kwa njia ya ndugu zake maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wale wote waliomtumia salam na matashi mema ya Noeli na Mwaka Mpya 2020. Amekiri kwamba, si rahisi kuweza kuwajibu wote hawa, lakini anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea. Kwa namna ya pekee, anawashukuru wale wote wanaoendelea kumsindikiza katika maisha na utume kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa sala na sadaka zao. Anasema kwamba, kwa hakika anahitaji msada wa sala na sadaka zao kwa ajili ya maisha na utume wake.

Papa: Ufilippini: Maafa

 

26 December 2019, 15:44