Tafuta

Vatican News
Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Baraza la Makardinali ameng'atuka kutoka madarakani baada ya kuhudumia tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2019. Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Baraza la Makardinali ameng'atuka kutoka madarakani baada ya kuhudumia tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2019.  (Vatican Media)

Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali ang'atuka kutoka madarakani

Kardinali Angelo Sodano, Dekano mstaafu wa Baraza la Makardinali alizaliwa mwaka 1927. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 23 Septemba 1950. Akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Askofu na kuwekwa wakfu tarehe 15 Januari 1977. Tarehe 30 Novemba 1978 akateuliwa kuwa Askofu mkuu. Ilikuwa ni tarehe 28 Juni 1991 Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteuwa kuwa Kardinali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Kardinali Angelo Sodano la kutaka kung’atuka kutoka madarakani kama Dekano wa Baraza la Makardinali, baada ya kutimiza miaka 92 baada ya kuwaongoza Makardinali wenzake tangu mwaka 2005. Kardinali Angelo Sodano, Dekano mstaafu wa Baraza la Makardinali alizaliwa tarehe 23 Novemba 1927 huko Kisiwani Asti, nchini Italia.Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 23 Septemba 1950. Akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Askofu na kuwekwa wakfu tarehe 15 Januari 1977. Tarehe 30 Novemba 1978 Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu mkuu. Ilikuwa ni tarehe 28 Juni 1991 Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteuwa kuwa Kardinali. Katika maisha na utume wake, Kardinali Angelo Sodano amewahi pia kuwa ni Balozi wa Vatican kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 1990 alipoteuliwa kuwa Katibu mkuu wa Vatican, utume ambao ameutekeleza hadi mwaka 2005.

Kardinali Angelo Sodano, Dekano Mstaafu wa Baraza la Makardinali kwa niaba ya Makardinali wenzake pamoja na wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican, Jumamosi, tarehe 21 Desemba 2019 amemtakia heri na baraka Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli na Mwaka mpya 2020. Katika kipindi cha mwaka 2019, Baba Mtakatifu ameendelea “kuchanja mbuga” ili kutangaza na kushuhuduia furaha ya Injili inayowaambata na kuwakumbatia watu wote sehemu mbali mbali za dunia. Katika mchakato huu, Baba Mtakatifu ameonesha ujasiri na hatimaye, akavuta vikwazo vilivyokuwa mbele yake, akionesha daima ile furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Daima ameendelea kuwa ni chombo na shuhuda wa matumaini kwa kutembelea nchi kumi na moja.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu aliuanza mwaka 2019 kwa kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyonena” Lk. 1:38. Ilikuwa ni fursa ya kutafakari vipaumbele vya maisha na utume wa vijana, changamoto, matatizo na fursa walizo nazo kama mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili. Baba Mtakatifu ameufunga mwaka kwa kutembelea Thailand na Japan. Akiwa mjini Nagasaki, Baba Mtakatifu Francisko amepaaza sauti yake kwa ajili kudumisha amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Kwa hakika katika kipindi cha Mwaka 2019, Baba Mtakatifu amekuwa ni shuhuda na chombo cha amani duniani. Baraza la Makardinali pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatica itaendelea kushirikiana na kushikamana pamoja naye katika mchakato wa utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Mchungaji mwema.

Kardinali Sodano

 

 

21 December 2019, 14:59