Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 22 Desemba 2019 amekutana na kuzungumza na watoto wanaotibiwa kwenye Zahanati ya "Santa Marta" amekazia: Matumaini, Mapendo na Amani. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 22 Desemba 2019 amekutana na kuzungumza na watoto wanaotibiwa kwenye Zahanati ya "Santa Marta" amekazia: Matumaini, Mapendo na Amani.  (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Francisko kwa watoto: Matumaini, Mapendo na Amani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali walimtolea Mtoto Yesu zawadi kubwa tatu: Matumaini, Mapendo na Amani na kwa hakika neno vita halikuwemo. Watoto wanasema, vita inauwa, inaleta maafa makubwa kwa watu na mali zao; vita inasababisha majonzi na huzuni maishani. Watoto wamempongeza Papa kwa kuadhimisha Miaka 83 ya kuzaliwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 22 Desemba 2019 amekutana na watoto, wazazi, wauguzi na wahudumu wa Zahanati ya “Santa Marta”  iliyoko mjini Vatican, kwenye Ukumbi wa Paulo VI,  ili kuwatakia heri na baraka kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa mwaka 2019. Na kwa upande mwingine, familia ya Zahanati ya “Santa Marta”, ambayo inaundwa na zaidi ya watu 800, imetumia fursa hii, kumtakia heri na baraka, amani, utulivu na afya njema, Baba Mtakatifu Francisko anapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 83 tangu kuzaliwa kwake na Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja takatifu ya Upadre, hapo tarehe 13 Desemba 1969. Zahanati ya “Santa Marta” ilianzishwa na Papa Pio XVI kunako mwaka 1922 na iko jirani sana na Hosteli ya Mtakatifu Martha, ambayo kwa sasa ni makazi ya Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni Zahanati inayotoa huduma ya afya kwa watoto wadogo wanaotoka kwenye familia zenye kipato cha chini zaidi kutoka ndani na nje ya Italia.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza watoto waliomwimbia kwa ustadi mkubwa pamoja na zawadi ya Keki ya Kumbu kumbu ya miaka 83 ya kuzaliwa kwake. Amewashukuru wazazi, wauguzi na wafanyakazi wa kujitolea kwa kuwasindikiza pamoja na kuwa karibu na watoto wao, kwa sababu kwa njia hii wanawatia shime na matumaini ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Watoto ni watakatifu wa Mungu na ahadi ya Mungu na mambo mazuri kwa siku za mbeleni. Baba Mtakatifu anasema, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali walimtolea Mtoto Yesu zawadi kubwa tatu: Matumaini, Mapendo na Amani na kwa hakika neno vita halikuwemo. Watoto wanasema, vita inauwa, inaleta maafa makubwa kwa watu na mali zao; vita inasababisha majonzi na huzuni maishani. Ili kufyekelea mbali dhana ya vita, kuna haja ya kujikita katika ujenzi wa fadhila ya upendo kwa sababu: Matumaini, Amani na Mapendo ni sawa na chanda na pete kwani ni fadhila zinazotegemeana na kukamilishana.

Kumbe, Baba Mtakatifu amekazia: Matumaini, Upendo na Amani. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wale wote waliofanikisha hafla hii! Baada ya hapo, Baba Mtakatifu alikwenda moja kwa moja kusali na kutoa tafakari kwenye Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Zahanati: St. Marta

 

23 December 2019, 09:08