Tafuta

Vituo vya Michezo Roma vinaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipoanza kutoa baraka kwa ajili ya Sanamu za Mtoto Yesu kwa ajili ya Mapango ya Noeli Roma. Vituo vya Michezo Roma vinaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipoanza kutoa baraka kwa ajili ya Sanamu za Mtoto Yesu kwa ajili ya Mapango ya Noeli Roma. 

Jubilei ya Miaka 50 ya Baraka za Pango la Noeli Roma: 1969-2019

Kwa mara ya kwanza, Mtakatifu Paulo VI alibariki Sanamu za Mtoto Yesu kwa ajili ya Mapango ya Noeli, Jimbo kuu la Roma tarehe 21 Desemba 1969. Maadhimisho ya Mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Hata hapa ni Noeli ya Bwana”. Waamini wanakumbushwa kwamba, Yesu anaweza kuzaliwa mahali popote pale. Lakini zaidi anazaliwa katika hali ya umaskini, ukimya na unyenyekevu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio mwaka A wa Kanisa, tarehe 15 Desemba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amebariki Sanamu za Mtoto Yesu zitakazowekwa kwenye Mapango ya Noeli yaliyoandaliwa na watoto kutoka Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu katikaWaraka wa Kitume “ADMIRABILE SIGNUM” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” anafafanua kwamba,  Pango la Noeli ni mahali ambapo panaonesha alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, alama hai ya Injili, mwaliko wa kutafakari Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwanadamu, ili kukutana na watu wote, ili kuwaonjesha upendo wake na hatimaye, waweze kuunganika pamoja naye.

Vituo vya Michezo vya Roma “Centro Oratori Romani”, Jumapili tarehe 15 Desemba 2019 vimeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu watoto waanze mchakato wa kuomba baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu kwa ajili ya Mapango ya Noeli nyumbani kwao. Kwa mara ya kwanza, Mtakatifu Paulo VI alibariki Sanamu za Mtoto Yesu kwa ajili ya Mapango ya Noeli, Jimbo kuu la Roma tarehe 21 Desemba 1969. Maadhimisho ya Mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Hata hapa ni Noeli ya Bwana”. Waamini wanakumbushwa kwamba, Yesu anaweza kuzaliwa mahali popote pale. Lakini zaidi anazaliwa katika hali ya umaskini na kimyaa kikuu; mahali ambapo wengi wamepageuzia kisogo, mwaliko kwa waamini kujinyenyekesha ili waweze kumpokea na kukaribisha Kristo Yesu anayezaliwa upya katika historia na maisha yao.

Jubilei hii imezinduliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio maarufu kama Jumapili ya furaha “Dominica Gaudete”, watoto kutoka Parokia mbali mbali za Jimbo kuu la Roma walikusanyika kusali na kusherehekea Fumbo la Umwilisho, huku wakiwa waumeungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa sala kama kielelezo cha kumtukuza Mwenyezi Mungu ambaye ameua kuambatana na waja wake kwa njia uwepo angavu wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili! Injili zinatoa ufafanuzi wa Pango la Noeli kwa kusema kwamba, Bikira Maria, alimzaa Mwanaye, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe,  kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.

Yesu alilazwa kwenye “Praesepium” yaani “Pango la Noeli”. Hiki kikawa ni kitanda chake cha kwanza, Kristo Yesu ambaye alijifunua kama “Mkate ulioshuka kutoka mbinguni”, akalazwa Pangoni ili awe ni “chakula cha wasafiri”. Pango la Noeli limesheheni utajiri na amana ya Mafumbo ya maisha ya Kristo Yesu, ambayo yako karibu sana na maisha ya watu wa kawaida. Itakumbukwa kwamba, Pango la kwanza la Noeli lilitengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kunako tarehe 29 Novemba 1223 baada ya Papa Honorius III kupitisha Katiba ya Shirika lake. Pango hili la Noeli ni matokeo ya hija ya kiroho iliyofanywa na Mtakatifu Francisko wa Assisi mjini Bethlehemu pamoja na picha alizowahi kuona kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Alilitengeneza Pango la Noeli, Siku 15 kabla ya Sherehe ya Noeli kama kumbu kumbu endelevu ya Fumbo la Umwilisho.

Pango la Noeli

 

 

16 December 2019, 12:20