Papa Francisko anawataka wanafunzi kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Papa Francisko anawataka wanafunzi kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! 

Wanafunzi wawe mstari wa mbele katika utunzaji bora wa mazingira

Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato Si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, unaopembua kwa na kina mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Wanafunzi wanawapaswa kuwajibika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Taasisi zinazojihusisha na Sekta ya Elimu nchini Italia, FIDAE yaani “Federazione Istituti di Attività Educative” kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki linaendelesha mradi ujulikao kama “I Can” yaani “Hata mimi ninaweza” mintarafu Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato Si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”,  unaopembua kwa na kina mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika katika usawa na kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote duniani. Kwa upande wa Shirikisho la Taasisi zinazojihusisha na Sekta ya Elimu nchini Italia mkazo mkubwa hapa unawekwa kwa wanafunzi, ili wao wenyewe waweze kuwa ni chachu ya mageuzi makubwa katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira kwa kuvukwa mifumo ya elimu ambayo imeonesha ukasisi katika malezi na makuzi ya wanafunzi.

Kimsingi mfumo huu wa elimu umepata chimbuko lake nchini India kutokana na mawazo ya Kiran Bir Sethi. Wanafunzi wanaohusika na mradi huu kuanzia tarehe 27-30 Novemba 2019 wamekuwa wakifanya mikutano mbali mbali na hatima ya yote haya, wakaweza kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Roma, hapo tarehe 29 Novemba 2019. Baba Mtakatifu amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wanafunzi wenye umri kati ya miaka 6-16 walipata nafasi ya kukutana na Baba Mtakatifu mubashara, huku wakiwa wamesindikizwa na wazazi, walezi pamoja na waalimu wao kutoka katika nchi 60 na Italia ikiwa ni nchi mwenyeji! Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu aliwaangalisha wanafunzi kuwa makini dhidi ya mifumo mbali mbali ya ubaguzi, matumizi ya nguvu na “Cyberbullying” yaani unyanyasaji na uonevu wa kimtandao. Mafundisho ya dini mbali mbali duniani yanakazia kuhusu uzuri na wema kama ambavyo unashuhudiwa kwenye simulizi la kazi ya uumbaji katika Kitabu cha Mwanzo alivyoweza kutenganisha nuru na giza, maji na nchi kavu, jua na mwezi, binadamu na wanyama wa mwituni; mwanaume na mwamake.

Mwenyezi Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Kazi ya uumbaji anasema Baba Mtakatifu Francisko inachapa ya uzuri na wema wa Mungu na kwamba, binadamu anayo dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, analinda na kuiendeleza kazi hii kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Kuna uhusiano mkubwa kati ya kitu chema na kizuri kwa ajili ya huduma kwa jirani kama ambavyo Mwenyezi Mungu alinuia tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Kwa hakika mwanadamu hawezi kufidia uzuri asilia kwa vitu anavyovitengeneza yeye mwenyewe, kwa kutaka kujifananisha na Mungu kama ilivyokuwa kwa Prometeo. Mwanadamu anataka “kujimwambafai” kwa kujikweza na kuwa ni kiini cha mambo yote hiki ni kishawishi cha hatari sana. Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kushirikiana na kushikamana na wengine ili kuitengeneza dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Wanafunzi kwa kushirikiana na kushikamana na walimu, wazazi na walezi wao, wanaitwa na kuhamasishwa kujenga ulimwengu ambao utakua kama kijiji cha elimu, kwa kujenga na kudumisha mtandao wa ushirikiano na mafungamano ya kibinadamu, dawa mchunguti dhidi ya mifumo mbali mbali ya ubaguzi, matumizi ya nguvu na “Cyberbullying” yaani unyanyasaji na uonevu wa kimtandao. Kwa njia hii mfumo wa elimu utasaidia kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu sanjari na amani kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia; kwa kujikita katika mchakato unaosimikwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene katika ukweli na uwazi. Wanafunzi wakishirikiana na wazazi wao katika mradi mzima wa elimu, wanapaswa kuonesha tabia ya udadisi kwa kile ambacho watoto wao wanajifunza shuleni, kwa kuendelea kuangalia upya unaojitokeza ili kwa pamoja waweze kusaidiana kufanya upembuzi yakinifu.

Wazazi waoneshe tabia ya uvumilivu na waendelee kuchangia katika ukuzaji wa mfumo mpya wa elimu. Baba Mtakatifu anawakumbusha walimu, wazazi na walezi kwamba, vijana wanapenda kuchota kutoka kwao imani na ujasiri wa kutekeleza mambo kama chachu inayopania kupyaisha mazingira na jamii katika ujumla wake. Ushiriki wao mkamilifu unaweza kuacha alama ya kudumu katika sekta ya elimu. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa ubunifu wao kiasi kwamba, mradi huu unatumia pia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ili kuwafikia walengwa. Wanafunzi hawa wameonesha kwamba, matumizi pekee ya akili bandia yanahitaji vuguvugu na joto la binadamu. Baba Mtakatifu anakumbuka jinsi ambavyo watoto wawili wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia walivyo elezea mradi huu mkubwa hatua kwa hatua.

Baba Mtakatifu anawashukuru wanafunzi hawa ambao wameamua kujikita katika mchakato wa umoja na mshikamano wa dhati, kwa kufanya kazi kwa pamoja na kuwajibika kikamilifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Haya ni matunda ya mfumo wa elimu unaowawezesha wanafunzi kutumia vyema akili, mikono na nyoyo zao kwa kutambua kwamba, yote haya yameungana kwa pamoja. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna heri zaidi kutoa kuliko kupokea! Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko akawaalika kusali katika ukimya na hatimaye, akawapatia baraka yake ya kitume, wanafunzi wakaondoka wakiwa wamefurahi kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mubashara!

Papa: Vijana na Mazingira
28 December 2019, 15:23