Tafuta

Sekretarieti ya Haki Jamii na Ekolojia ya Shirika la Wayesuit inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1969. Sekretarieti ya Haki Jamii na Ekolojia ya Shirika la Wayesuit inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1969. 

Jubilei ya Miaka 50 ya Sekretarieti ya Haki Jamii na Ekolojia!

Sekretarieti ya Haki Jamii na Ekolojia, “Sjes” iliyoanzishwa kunako mwaka 1969 ni msingi wa maisha na utume wa Shirika la Wayesuit sehemu mbali mbali za dunia. Kauli mbiu: “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini: Ni muda kwa Wayesuit kusikiliza na kujibu; haki na upatanisho, kumbu kumbu ya miaka 50 ya Sekretarieti ya Haki Jamii na Ekolojia, mang’amuzi ya jinsi ya kuendeleza utume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sekretarieti ya Haki Jamii na Ekolojia, “SJES” iliyoanzishwa kunako mwaka 1969 ni msingi wa maisha na utume wa Shirika la Wayesuit sehemu mbali mbali za dunia. Katika kipindi cha Mwaka 2019, Sekretarieti hii inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini: Ni muda kwa Wayesuit kusikiliza na kujibu; haki na upatanisho, kumbu kumbu ya miaka 50 ya Sekretarieti ya Haki Jamii na Ekolojia, mang’amuzi ya jinsi ya kuendeleza utume huu kwa siku za usoni. Lengo lilikuwa ni kukuza na kuimarisha utume wa Wayesuit sehemu mbali mbali za dunia kama kielelezo cha imani tendaji. Wayesuit kwa kusoma alama za nyakati, wakaendelea kusimama kidete katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Kumbe, katika kipindi cha miaka 50 Wayesuit wameendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya haki na utamadunisho katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Masuala ya haki jamii na utunzaji bora wa mazingira yakaendelea kupewa msukumo wa pekee katika maisha na utume wa Wayesuit, ili kujenga na kudumisha sera na mikakati ya uchumi fungamani, unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2019 hadi mwaka 2029 Wayesuit wameamua kujielekeza zaidi kwa kutembea na kushikamana na maskini; watu wanaotelekezwa na kusukumiziwa pembezoni mwa jamii. Ni muda wa kushikamana na wale ambao wamejeruhiwa katika undani wa maisha na utu wao. Wajesuit wanapenda kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upatanisho, haki na amani. Wayesuit katika maisha na utume wao wanataka kuendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Ili kutekeleza yote haya kuna haja ya watu kuwa na haki ya kupata elimu juu ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote.

Rasilimali fedha na watu inahitajika kwa ajili ya kudhibiti matumizi ya raslimali na utajiri wa dunia; wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Jubilei ya Miaka 50 Sekretarieti ya Haki Jamii na Ekolojia, “SJES” inawashirikisha Wayesuit, wataalam mabingwa na wakereketwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Maisha na utume wa Wayesuit unaweza kueleweka katika mazingira ya haki jamii. Katika kipindi hiki cha miaka 50 kuna Wayesuit mbao wameyamimina maisha yao kwa ajili ya kulinda na kutetea haki jamii sehemu mbali mbali za dunia. Ni watu waliosimama kidete kutetea: utu, heshima, usawa na haki msingi za binadamu. Changamoto endelevu kwa Wayesuit ni kuendelea kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na maskini wanosukumizwa pembezoni mwa jamii. Haki Jamii na Ekolojia inawawezesha Wayesuit kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji; mambo msingi yanayofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Maadhimisho haya ni sehemu ya mchakato wa kupyaisha na kuimarisha imani inayokita mizizi yake katika haki na majadiliano ya kitamaduni, ili kuambata ekolojia na maendeleo fungamani ya binadamu! Katika maadhimisho haya, Wayesuit wanapenda kukiri makosa na mapungufu yaliyojitokeza wakati wanatekeleza dhamana na wajibu wao katika kutekeleza haki jamii na ekolojia, ili kuanzia sasa waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 7 Novemba 2019 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na wajumbe wanaosherehekea Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Sekretarieti ya Haki Jamii na Ekolojia. Huu ni utume ambao unapata chimbuko lake tangu mwanzo wa Shirika kunako mwaka 1550, wakajipambanua kuwa ni walinzi na watetezi wa Mafundisho ya Kanisa; kwa kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, chemchemi ya faraja na utume wa Wayesuit.

Kwa njia ya huduma ya huruma na upendo, Wayesuit walipania kumwona Mwenyezi Mungu kati ya watu waliokuwa wanateseka na kuzama katika unyonge na utupu wa maisha yao; watu waliokuwa wananyanyaswa na kubezwa ndani ya jamii. Padre Pedro Arupe, alitaka kuona kwamba, maisha na utume wa Wayesuit unakita mizizi yake katika misingi ya haki jamii, kwani kwake, maskini ni mahali muafaka pa kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu. Hii ni zawadi wanayopaswa kuipokea kwa mikono miwili kama kielelezo cha imani tendaji. Ikumbukwe kwamba maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, wao ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, imani inakuwa ni sehemu ya Fumbo la Pasaka, kwa kuonesha huruma, wema na fadhila na kwamba huduma kwa maskini ni faraja kubwa kwa wale wanaohudumia.

Hii ni sehemu ya mchakato unaopania kuwapatia wafuasi wa Kristo toba na wongofu wa ndani, kwa kumwangalia na kumtafakari Kristo Yesu anaendelea kusulubiwa. Anawaalika kuwa pamoja naye chini ya Msalaba kwa kushikamana na maskini, ili kujenga madaraja yanayowakutanisha watu. Wafuasi wa Kristo waendelee kupata utambulisho wao chini Msalaba, ili kujizatiti zaidi katika kumfuasa kwenye Njia ya Msalaba na katika huduma makini. Leo hii kuna Vita ya Tatu ya Dunia inayotekelezwa sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya wahalifu, mauaji ya kimbari pamoja na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu. Kuna umati mkubwa wa watu wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; kuna watu wanaoteseka kutokana na chuki dhidi ya wageni “Xenophobia”. Katika orodha hii, kuna watu wanaotaka “kujimwambafai” kwa kukumbatia utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko na kwamba, kumekuwepo na pengo kubwa kati ya “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” na kundi la watu wachache ambao ni matajiri wa kutupwa, wanaoendelea kula “bata kwa mirija”.

Baba Mtakatifu anasema, kuna uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote unaoendelea kuwatumbukiza watu wa Mungu katika umaskini wa hali na kipato. Matukio yote haya ni mwaliko kwa Wayesuit kuyatafakari na kuyapatia majina yake halisi bila kupepesa pepesa macho! Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kufanya mapinduzi ya kitamaduni, ili kuwaokoa watu wanaoteseka na kukata tamaa ya maisha. Kumbe, kuna haja ya kukazia ushiriki wa majadiliano katika hatua mbali mbali za kupanga na kutekeleza maamuzi yanayofikiwa. Ni wajibu wao kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na huduma makini za kijamii. Wayesuit waendelee kushirikiana na taasisi nyingine katika huduma kwa maskini katika ulimwengu wa utandawazi. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Wayesuit. Mwaka 2019, Wayesuit wanaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu Wayesuit waliokuwa wanafanya utume wao kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha El Salvador walipouwawa kikatili. Maisha na kifodini ni chanda na pete kwa Wayesuit, chemchemi ya Injili ya matumaini.

Katika muktadha wa hatari za maisha, Wayesuit hawana sababu ya kukata tamaa, bali waendelee kujiaminisha katika Injili ya matumaini, kwa kuwa ni mashuhuda wanyenyekevu kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuwa ni wadau wa mustakabali wa maisha yao. Wayesuit waendelee kuwa ni mashuhuda wa matumaini ya Kikristo, ili kuwasaidia watu kukua na kukomaa; sanjari na kuwa na ujasiri wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Ili kufanikisha yote haya, Wayesuit lazima wajenge moyo wa sala na ibada; wapanzi wa mbegu ya matumaini pamoja na kutembea bega kwa bega na maskini na wale wote wanaoteseka kwa kukosa matumaini na furaha ya kweli!

Papa: Haki Jamii

 

07 November 2019, 14:28