Tafuta

Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya III ya Maskini Duniani 2019: Kauli mbiu: Matumaini ya wanyonge hayatapotea kamwe! Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya III ya Maskini Duniani 2019: Kauli mbiu: Matumaini ya wanyonge hayatapotea kamwe! 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku III ya Maskini Duniani 2019

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya siku ya III ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2019 unaongozwa na kauli mbi: "Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele" (Rej. Zab. 9:19). Mzaburi anaonesha imani na matumaini yake kwa Mwenyezi Mungu licha ya ukosefu wa haki, mateso na kukosa uhakika wa maisha. Kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 17 Novemba 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani ni changamoto inayotolewa na Mama Kanisa kwa Jumuiya ya Kimataifa, kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wa nyakati hizi wanaoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia. Maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu na kwamba, bado kilio cha maskini hakijasikilizwa hata kidogo, kwani hata leo hii, kuna watu wanataka “kuwashikisha adabu maskini, ili wafunge midomo yao na kamwe wasiendelee kuleta kero duniani”. Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya III ya Maskini Duniani ni tarehe 17 Novemba 2019 yaani Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya siku ya III ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2019 unaongozwa na kauli mbiu: "Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele" (Rej. Zab. 9:19). Mzaburi anaonesha imani na matumaini yake kwa Mwenyezi Mungu licha ya ukosefu wa haki, mateso pamoja na kukosa uhakika wa maisha.

Mzaburi anasimulia udhalimu wa mwenye kiburi, anamwomba Mwenyezi Mungu atoe hukumu ya haki, kwa sababu maskini na mnyonge amejidhaminisha mikononi mwake kwa sababu Mungu ndiye msaada na kimbilio lake la daima. Pengo kubwa kati ya maskini na matajiri ni changamoto ambayo imekuwepo katika maisha na historia ya mwanadamu. Zaburi hii ilitungwa anasema Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maendeleo na ustawi wa kiuchumi, hali ambayo ilipelekea mipasuko na ukosefu mkubwa wa haki jamii. Kukaibuka kundi la matajiri wachache ndani ya jamii na kwa upande mwingine, umati mkubwa wa maskini, hao ndio “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Katika kipindi hiki wadhalimu walikuwa na jeuri sana, kiasi hata cha kuwanyanyasa na kuwadhulumu maskini, hali ambayo inaendelea kutokea hata leo hii. Kuna watu wachache sana ambao wamejikusanyia utajiri wa kutupwa, lakini mitaani kuna jeshi kubwa la maskini wanaokosa hata mahitaji msingi katika maisha yao, hata wakati mwingine wanadhulumiwa na kunyanyaswa kama “Mbwa koko”.

Matajiri wanajiona kana kwamba, hawana haja na kitu chochote, lakini wanakumbushwa na Maandiko Matakatifu kwamba, wao ni: wanyonge, watu wenye mashaka, maskini, vipofu na watu walio uchi. Kwa bahati mbaya hali hii bado inaendelea na binadamu kamwe hajajifunza kutokana na historia na kwamba, maneno ya Mzaburi yanaonesha hali halisi kwa watu wa nyakati hizi, ambao wanapaswa kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu ili wahukumiwe. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, hata katika ulimwengu mamboleo kuna maskini ambao wametumbukizwa katika mifumo mbali mbali ya umaskini duniani. Kuna wakimbizi na wahamiaji; kuna watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Kuna vijana wa kizazi kipya wanaotafuta fursa za ajira. Kuna watu wanaotumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Kuna maskini wanaoishi katika hali ngumu kiasi kwamba, wanatamani kujishibisha kwa makombo ya chakula kinachotupwa kwenye mapipa ya takataka mijini na matokeo yake maskini kama hawa wanatelekezwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ndiyo kashfa inayoendelea kushuhudiwa ulimwenguni.

Kwa sababu ya umaskini wao, wanahukumiwa na jamii kuwa ni watu hatari sana. Katika mahangaiko yao ya ndani, wamekuwa ni watu wa kurandaranda mitaani wakitafuta fursa za ajira, makazi na mahali ambapo wanaweza kuonja upendo wa dhati. Hawa ni watu ambao wamenyimwa haki zao msingi; wanadhulumiwa na kunyanyasika. Wanafanyishwa kazi za suluba, katika mazingira magumu na hatarishi kwa ujira kiduchu pengine hata bila ya kuwa na fursa ya kushirikiana na wengine. Hawana haki ya kupata mafao wala mapumziko ya ugonjwa. Mzaburi anasema, mdhalimu anataka kumkamata mnyonge, ili amvute wavuni mwake. Maskini ni watu wanaowindwa, ili wakamatwe na kutumbukizwa kwenye utumwa mamboleo; leo hii kuna umati wa maskini wanaoendelea kulalama barabarani, lakini hakuna wa kusikiliza na kujibu kilio chao; ni watu ambao wamegeuka kuwa ni tishio hata kwa majirani zao. Mzaburi anasikitika kuona ukosefu wa haki na mateso yanayowakabili maskini wanaomtumainia Mungu ambaye kamwe hatawageuzia kisogo, kwani Mwenyezi Mungu anafahamu hali halisi, kwa sababu anawapenda na anataka kujenga mahusiano na mafungamano ya dhati pamoja nao.

Mwenyezi Mungu anasikiliza na kujibu kilio cha maskini; anawapatia msaada kwa wakati wake; anawalinda na kuwaokoa. Maskini mbele ya Mwenyezi Mungu, wanao uhakika kwamba, iko siku atawatendea haki na kuwapatia msaada. Siku ya Bwana itakapowadia, hapo kutakuwa na “mshike mshike” kwani kuta zote za utengano kati ya Mataifa zitabomolewa na wadhalimu watakiona “cha mtema kumi”. Mateso na mahangaiko ya maskini hayadumu milele yote bila ya kushughulikiwa, kwani kilio cha maskini daima kitaendelea kusikika na kwamba, maskini ni sawa na moto wa kuotea mbali, iko siku watalipuka! Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya III ya Maskini Duniani, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujiandaa kukabiliana na Siku ya Mwisho, kwa kujitahidi kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma kwa sababu Kristo Yesu katika Injili anajitambulisha na ndugu zake walio wadogo. (Rej. Mt. 25:40).

Huu ndio ujumbe wa Injili unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Mwenyezi Mungu, kwa njia ya Kristo Yesu amejifunua kuwa ni Baba mkarimu, mwingi wa huruma, mapendo na neema. Ni chemchemi ya matumaini kwa wale waliokata tamaa kwa kesho iliyo bora zaidi. Waamini wanaalika kutafakari Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, kwani anatoa kipaumbele kwa maskini, wanaoendelea kudidimizwa zaidi na zaidi katika umaskini. Katika Ufalme wa Mungu, maskini wanao upendeleo wa pekee na ni dhamana na wajibu wa wafuasi wa Kristo kuwapatia maskini imani na matumaini. Huu ni wajibu ambao jumuiya ya Kikristo inapaswa kuuvalia njuga kama sehemu ya ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili. Ni mwaliko wa kushikamana na maskini kwa sababu ni sehemu ya Fumbo wa mwili wa Kristo na kwamba, huduma kwa maskini ni kiini cha uinjilishaji na ushuhuda wa imani tendaji unaogusa uhalisia wa maisha ya watu.

Baba Mtakatifu anamkumbuka kwa namna ya pekee, Jean Vanier, mwamini mlei, aliyejisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini; akawaonesha upendo na mshikamano wa dhati, wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Alijiundia kundi la watu waliosaidiana naye kwa ajili ya kuwahudumia maskini, kiasi cha kuwaletea mabadiliko makubwa katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kilio cha maskini kikasikilizwa na hatimaye, wakapatiwa matumaini yaliyokuwa yanabubujika kutoka katika upendo unaopaswa kushuhudiwa hata katika ulimwengu mamboleo. Upendeleo kwa maskini ni kati ya vipaumbele vya Kanisa. Hapa ni mahali ambapo, upendo unamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa sababu maskini ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Huduma makini kwa maskini iwe ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Kanisa katika maisha na utume wake, na hasa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya, unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha.

Baba Mtakatifu anawasifu na kuwapongeza wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kutambua mahitaji ya kweli kwa maskini hawa na wala wasiridhike na hatimaye kuishia kwa kuwatimizia mahitaji ya mwili peke yake, bali mahitaji yao ya ndani kabisa na huo ni mwanzo wa majadiliano ya kidugu. Wajitahidi kuweka kando mambo ya sera na misimamo ya kisiasa kwa kujikita katika kuangalia mambo msingi ya maisha ya kiroho. Hakuna ubaguzi mkubwa kama kumnyima maskini mahitaji ya maisha ya kiroho. Maskini katika hija ya maisha yao, wanahitaji kwanza uwepo wa Mungu unaoshuhudiwa na watakatifu ambao ni majirani wanaoishi karibu nao; wakristo wanaoshuhudia nguvu ya upendo. Maskini wanahitaji uwepo endelevu wa jirani zao na wala si mahitaji ya chakula peke yake. Wanahitaji kuungwa mkono, kunyanyuliwa na kusaidiwa ili waweze kupyaisha maisha yao na hatimaye, kuvunjilia mbali upweke hasi.

Kwa maneno mafupi, maskini wanahitaji upendo! Wanahitaji kusikilizwa na kupewa tabasamu la “kukata na shoka”. Kwa njia ya maskini, waamini wanaweza kukutana Uso wa Kristo Yesu. Maskini ni watu wanaoonesha ile hekima ya Mungu inayo okoa. Katika hija ya maisha ya hapa duniani, waamini wajitahidi kutubu na kumwongokea Mungu, wawatambue maskini kati yao na kuwapenda kwa moyo wa dhati! Mwenyezi Mungu kamwe hatakisahau kilio cha wanyonge, awatasikiliza na kuwajibu kwa wakati wake. Maskini wanatambua kwamba, kwa hakika wanapendwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, kamwe umaskini hauwezi kuwapokonya utu na heshima yao. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya matumaini ya maskini, atasikiliza tamaa ya wanyonge, ataitengeneza nyoyo yao na kuwategea sikio. Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini na faraja kwa maskini. Maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani, iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kwa ajili ya huduma kwa maskini. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kusema, kwa wale wote wanaolicha jina la Mungu, jua la haki na lenye kuponya litawazukia.

Papa: Ujumbe Maskini 2019

 

13 November 2019, 16:32