Tafuta

Vatican News
Papa Francisko tarehe 4 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Kimataifa, FIUC/IFCU: Umuhimu wa elimu bora! Papa Francisko tarehe 4 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Kimataifa, FIUC/IFCU: Umuhimu wa elimu bora!  (Vatican Media)

Elimu makini inafumbatwa katika: Maadili, Mtu na Mazingira yake!

Vyuo Vikuu vya Kikatoliki vinapaswa kuwa ni vituo vinavyowawezesha watu kupata majibu makini katika ngazi ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake, kwa kujikita katika mshikamano, udumifu, weledi pamoja na kuzingatia mambo yenye kugusa zaidi mafao ya wengi. Matatizo ya kale na mapya yanapaswa kupembuliwa kwa kuzingatia mwono wa mtu binafsi na ule wa kiulimwengu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Kimataifa, FIUC/IFCU. “The International Federation of Catholic Universities” kuanzia tarehe 4-5 Novemba 2019 linaadhimisha mkutano unaoongozwa na kauli mbiu “Mipaka mipya kwa ajili ya viongozi wa vyuo vikuu: Matarajio ya Afya na Ekolojia ya Vyuo vikuu”. Shirikisho hili limejikita katika masomo na tafiti mbali mbali kama sehemu ya mpango mkakati wa kuwaandaa wanazuoni wa baadaye. Mfumo wa vyuo vikuu unakabiliwa na changamoto pevu kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi pamoja na uvumbuzi wa teknolojia mpya bila kusahau mahitaji msingi ya jamii, ambayo taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vinahitaji kuwajibika barabara. Changamoto za kijamii na kiuchumi; kisiasa na utamaduni wa kudumisha Injili ya uhai ni changamoto katika utume wa vyuo vikuu, katika muktadha wa kufundisha, kufanya tafiti pamoja na kuwaandaa wasomi na wanazuoni wa baadaye, si tu katika masuala ya weledi na nidhamu, bali hata katika mchakato wa kujikita ili kusimamia mafao ya wengi katika hali ya ubinifu, ili hatimaye, vyuo vikuu viweze kuwa ni vitalu vya kuwaunda na kuwafunda viongozi wa kada mbali mbali wenye mwono sahihi kuhusu binadamu na ulimwengu unaomzunguka.

Vyuo vikuu havina budi kuangalia jinsi ambavyo vinaweza kuchangia katika maboresho ya huduma fungamani ya afya bila kusahau ekolojia fungamani. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 4 Novemba 2019 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Kimataifa na kuwataka kuhakikisha kwamba, Vyuo Vikuu vya Kikatoliki vinakuwa ni vituo ambamo watu wanaweza kupata majibu ya kiraia na maendeleo ya kitamaduni katika ngazi ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake, kwa kujikita katika mshikamano, udumifu, weledi pamoja na kuzingatia mambo yenye kugusa zaidi mafao ya wengi. Matatizo ya kale na mapya yanapaswa kupembuliwa kwa dhati kabisa, kwa kuzingatia mwono wa mtu binafsi na ulimwengu katika ujumla wake, ili matunda ya tafiti hizi yaweze kuwanufaisha watu wengi zaidi. Maendeleo makubwa ya sayansi ya teknolojia yanaonekana kuwa na ushawishi mkubwa katika maisha ya watu kimwili na kisaikolojia, hali ambayo inaathiri pia mbinu na mchakato wa masomo ya vyuo vikuu. Kumbe, kuna haja kwa wasomi kujiuliza, Je, ni kwa nini haya yanatendeka kama msingi wa masomo mbali mbali kwenye vyuo vikuu.

Elimu makini anasema Baba Mtakatifu Francisko inafumbatwa katika nidhamu, maadili na utu wema na kwamba, elimu haina budi kujibu maswali msingi yanayomsumbua mwanadamu kwa kuwa na mwono sahihi wa binadamu na ulimwengu unaomzunguka. Hiki ndicho kiini cha elimu kinachounganisha lengo na mchango wa masomo yanayotolewa yaani mfumo wa uelewa binafsi “forma mentis; kanuni za ushawishi, makundi, ubunifu pamoja na uzoefu kutoka nje ni mambo msingi katika kufanikisha maendeleo ya kisayansi. Ni katika muktadha huu, Chuo kikuu kinaweza kuwajibika katika akili pamoja na kuzingatia kanuni maadili yanayowawajibisha wahusika kwa ajili ya mafao ya jumuiya ya binadamu. Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Kimataifa linapaswa kujizatiti katika wajibu wa kimaadili kwa kuunganisha jumuiya ya wasomi; kwa kuendelea kua aminifu kwa sababu msingi zilizopelekea kuanzishwa kwa vyuo hivi; kwa kuunda na kuimarisha mtandao wa vyuo vikuu vya zamani na vile vinavyoanzishwa wakati huu, ili kujenga ari na mwamko wa kikatoliki sanjari na maboresho ya tamaduni za maisha ya watu.

Ekolojia ya chuo kikuu inajengeka pale ambapo kila mwanajumuiya anamwangalia mtu mzima, anajitahidi kuyafahamu mazingira yake anamoishi na kukua, ili kusaidia mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Vyuo vikuu vitaweza kufanikiwa kuwaunda na kuwafunda viongozi, ikiwa kama majiundo haya yatazingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kukuza dhamiri safi pamoja na kuwawezesha wanafunzi wao kutenda kadiri ya uwezo wao. Nadharia na vitendo ni mambo yanayopaswa kuunganishwa katika maisha ya wasomi na watafiti, ili ujuzi na maarifa yaliyopatikana yaweze kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Wanasayansi wanao wajibu mkubwa wa kutoa huduma bora zaidi, kwa sababu wamebahatika kuwa na ujuzi na maarifa, kama ilivyo hata kwa Jumuiya ya chuo kikuu na hasa kama ni vyuo vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa. Wasayansi wawe makini kuhusu ekolojia, ili kuziwezesha taasisi hizi kujibu changamoto mamboleo kwa weledi mkubwa. Ni katika muktadha huu, Kanisa Katoliki pamoja na Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Kimataifa, FIUC/IFCU, wataendelea kusimama kidete katika elimu bila kuogopa maarifa, kwani linataka kuyatakasa na kukuza asili ya binadamu katika ujumla wake: kiroho na kimwili.

Papa: Elimu

 

05 November 2019, 14:28