Vatican News
Papa Francisko anawaalika waamini kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu unaowakirimia toba, wongofu wa ndani na malipizi ya dhambi. Papa Francisko anawaalika waamini kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu unaowakirimia toba, wongofu wa ndani na malipizi ya dhambi.  (ANSA)

Papa Francisko: Zakayo mtoza ushuru na Jicho la huruma ya Mungu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kitendo cha kuwadharau na kuwatenga wadhambi kunawaongezea “usugu” wa kutenda mabaya zaidi na kuwa na moyo mgumu hata dhidi ya jumuiya. Mwenyezi Mungu analaani dhambi zinazotendwa na mdhambi, lakini anajitahidi kuhakikisha kwamba, mdhambi anaokolewa na kurejeshwa tena kwenye njia ya haki. Muhimu: Toba, Wongofu na Malipizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya 31 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa Inaelezea simulizi la Zakayo: Mkuu wa watoza ushuru aliyekuwa anaifanya kazi hii kwa ajili ya utawala wa Kirumi. Alikuwa ni tajiri wa kutupwa kwa sababu alipenda na kukumbatia sana rushwa katika maisha yake, lakini kwa bahati mbaya alikuwa ni mfupi wa kimo, hali iliyomfanya kudharauriwa na jamii iliyokuwa inamzunguka. Lakini alikuwa ni mtu aliyekuwa na kiu ya kutaka kumwona Yesu ambaye alisikia sana kuhusu habari zake. Kwa sababu ya ufupi wa kimo alipanda juu ya mti wa mkuyu ili Yesu anapopita yeye apate kumwona. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 3 Novemba 2019. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, naye Yesu alipomwona akamwambia ashuke na akaenda naye hadi nyumbani kwake.

Katika muktadha huu, Kristo Yesu, anaonesha utashi wa kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni, kama ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, wadhambi na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kristo Yesu, hakuona sababu ya kutoa “mahubiri wala kumkaripia” Zakayo mtoza ushuru licha ya manung’uniko ya watu, lakini Kristo Yesu akaamua kushinda nyumbani mwa Zakayo mtoza ushuru. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, hata leo hii, pengine, waamini wengi wangeliona tukio hili kuwa ni kashfa ya mwaka. Lakini ikumbukwe kwamba, kitendo cha kuwadharau na kuwatenga wadhambi kinawaongezea “usugu” wa kutenda mabaya zaidi na kuwa na moyo mgumu hata dhidi ya jumuiya. Mwenyezi Mungu analaani dhambi zinazotendwa na mdhambi, lakini anajitahidi usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, mdhambi anaokolewa na kurejeshwa tena kwenye njia ya haki.

Kwa mtu ambaye katika hija ya maisha yake hapa duniani, anadhani kwamba, hajawahi kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake, inakuwa ni vigumu kuweza kufahamu ukuu wa tendo hili na maneno yanayotolewa na Kristo Yesu kwa Zakayo mtoza ushuru. Moyo wa ukarimu, upendo na hali ya kujali pamoja na kuguswa na mahangaiko ya Zakayo mtoza ushuru yanasaidia kuleta toba, wongofu wa ndani na malipizi ya dhambi zake. Uwepo wa Kristo Yesu nyumbani mwa Zakayo mtoza ushuru, kuna mwezesha kuona historia na matukio mbali mbali ya maisha yake katika mwanga mpya, lakini zaidi kutokana na jicho la upendo kutoka kwa Kristo Yesu ambalo lilipenyeza hadi katika “sakafu ya undani wa maisha yake”. Akaongoka na kuwa mtu mpya, akawa na mwelekeo tofauti kabisa wa jinsi ya kutumia fedha na mali, badala ya kumezwa na uchu wa fedha, mali na utajiri wa haraka haraka, Zakayo anagundua njia mpya ya kuwasaidia maskini.

Ni katika muktadha huu, Zakayo mtoza ushuru anaamua kutoa nusu ya mali yake na kuwapatia maskini na ikiwa kama alikuwa amemnyang’anya mtu kitu kwa hila atamrudishia mara nne, matendo makuu ya Mungu kwa wadhambi, wanaotubu na kumwongokea Mungu. Zakayo mtoza ushuru anaonesha ile njia ya upendo wa dhati pasi na “ndoana” yaani: upendo wa nipe nikupe! Zakayo mtoza ushuru aliyekuwa “amemezwa na kusiginwa” na malimwengu kwa uchu wa mali na fedha ya rushwa na ufisadi, anageuka kuwa mkarimu na mgawaji wa mapaji na utajiri ambao Mwenyezi Mungu amemkirimia katika maisha yake, kiasi hata cha kufurahia ukarimu huu unaobubujika kutoka katika undani wa moyo wake, ulioonja huruma na upendo wa Mungu. Anatambua kwamba, anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu licha ya “ufupi wake” na dhambi zote alizowahi kutenda katika maisha, anageuka kuwa ni shuhuda na chombo cha upendo kwa maskini kwa kutumia fedha na utajiri wake kama alama ya umoja na mshikamano wa upendo.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwa kuwaalika waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwasaidia kuona ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu, ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu na kumpokea Kristo Yesu katika maisha yao, Yesu ambaye amekuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea!

Papa: Zakayo Mtoza Ushuru
03 November 2019, 10:40