Baba Mtakatifu Francisko anawaambia vijana kwamba, wao ni leo ya Mungu ambayo wanapaswa changia katika utekelezaji wake. Baba Mtakatifu Francisko anawaambia vijana kwamba, wao ni leo ya Mungu ambayo wanapaswa changia katika utekelezaji wake. 

Papa Francisko Wosia wa Kitume "Christus Vivit": Sura ya III: Leo ya Mungu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, vijana ni "Leo ya Mungu" ambayo wanapaswa kuchangia katika utekelezaji wake. Kanisa halina budi kuwasikiliza kwa makini badala ya kuorodhesha litania ya matatizo na mapungufu ya vijana wa kizazi kipya, matokeo yake ni vijana, “kuwageuzia kibao”! Viongozi wa Kanisa wanaitwa na kutumwa kama: mababa, wachungaji na viongozi wa kiroho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wosia wa kitume kutoka kwa Baba Francisko “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”, umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, iliyoadhimishwa mwezi Oktoba 2018, kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Vijana, Mang’amuzi na Miito”. Katika sura ya kwanza, Baba Mtakatifu anakita tafakari yake kwenye Neno la Mungu kuhusu vijana katika Maandiko Matakatifu, yaani: tangu katika Agano la Kale hadi Agano Jipya. Katika Sura ya Pili, Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu ni kijana milele yote. 

Katika Sura ya tatu, Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwamba, wao ni Leo ya Mungu ambayo wanapaswa kuchangia katika utekelezaji wake. Ndiyo maana Kanisa halina budi kuwasikiliza kwa makini badala ya kuorodhesha litania ya matatizo na mapungufu ya vijana wa kizazi kipya, matokeo yake ni vijana, “kuwageuzia kibao”! Viongozi wa Kanisa wanaitwa na kutumwa kama: mababa, wachungaji na viongozi wa kiroho, ili kuvunjilia mbali kuta za utengano na jicho linalotazama hatari peke yake katika maisha ya vijana! Viongozi wa Kanisa wawe na jicho la kuona ile mbegu njema iliyopandikizwa mioyoni mwa vijana kwa kutambua kwamba, moyo wao ni eneo takatifu! Ulimwengu wa vijana unafumbata nyuso mbali mbali! Kuna vijana wanaoishi katika maeneo ya vita, nyanyaso na kinzani za aina mbali mbali: Kuna kundi kubwa la vijana linalotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo! Matokeo yake ni baadhi ya vijana kujikuta wakimezwa na ubinafsi, uadui pamoja kudhaniana vibaya, kiasi cha hata kuwa ni wahanga wa matukio yanayokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, kuna sera na mikakati ya kisiasa na kiuchumi ambayo si rafiki sana kwa maisha ya vijana. Kuna vijana wanaotengwa na kusukumiziwa pembezoni mwa jamii kutokana na: dini, kabila na hali yao ya kiuchumi. Kuna vijana wanaopata ujauzito katika umri mdogo; vijana wanao ambukizwa virusi vya ugonjwa wa UKIMWI pamoja na kutumbukizwa katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, ikiwa ni pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya, michezo ya kamari na upatu pamoja na picha za ngono. Wapo vijana wanaotumbukizwa kwenye utamaduni wa kifo, kwa kukumbatia sera za utoaji mimba; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi! Kwa hali na mazingira yote haya, Mama Kanisa anawalilia watoto wake na anataka kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi! Baba Mtakatifu anawaalika vijana kulia na kuwaombolezea vijana wenzao wanaoishi katika hali na mazingira magumu na hatarishi. Kuna vijana wanaoishi katika umaskini wa hali na kipato. Kuna mashirika ya kimataifa na nchi tajiri zinazotoa misaada inayofumbatwa katika ukoloni wa kiitikadi ambao waathirika wakubwa ni vijana.

Haya ndiyo yale mambo yanayojionesha katika masuala ya kujamiana, ndoa, maisha na haki jamii. Vijana wanapendwa na mashirika ya biashara kimataifa kwa ajili ya matangazo ya biashara, wanataka kupoka uzuri na utajiri wa ujana kwa mafao yao binafsi! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kuhusu tamaa, madonda na tafiti zitakazosaidia kukuza na kudumisha utu, heshima na utakatifu wa maisha ya ujana. Maendeleo ya sayansi, teknolojia na tiba ya binadamu yanataka kuwasahaulisha vijana kwamba, maisha ni zawadi na kwamba, wameumbwa na hapa duniani ni wapita njia! Watu wanaweza kutumiwa kama nyenzo za watu wenye nguvu ya kiteknolojia! Ulimwengu wa kidigitali umeunda mazingira mapya na kurahisisha uhuru wa mawasiliano na kwamba, katika baadhi ya nchi mitandao ya kijamii ni maeneo muhimu sana katika maisha ya vijana wa kizazi kipya. Lakini, huu umekuwa ni uwanja wa kukuza upweke hasi, dhuluma na nyanyaso, ghasia na vitendo vichafu mitandaoni!

Kuna baadhi ya vijana wamekuwa ni waathirika wa matumizi ya mitandao ya kijamii, kiasi hata cha kugeuka kuwa wagonjwa na kwamba, mitandao hii imekuwa pia ni mahali pa ukatili wa kimtandao, mkondo wa kusafirishia picha za ngono, udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia au michezo ya kamari na upatu! Bado kuna usambazaji wa habari za kughusi “fake news”, mchezo mchafu unaofanywa na watu wenye nguvu ya kiuchumi ili kudhohofisha dhamiri na mchakato wa kidemokrasia. Wakati mwingine, mahusiano kwa njia ya mitandao yanaweza kudhohofisha utu na heshima ya binadamu, kiasi hata cha kugeuka kuwa ni kimbilio la watu kutoka katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tamaduni na maisha ya kiroho, hali ambayo inawatumbukiza vijana wengi katika upweke hasi na hapo ni mwanzo wa kuchungulia kaburi! Wimbi kumbwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo!

Kuna watu wanaokimbia vita, ghasia, dhuluma na nyanyaso za kisiasa na kidini, majanga asilia ambayo kimsingi yanayotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na umaskini mkubwa! Hawa ni watu wanaotafuta hifadhi, usalama na wanayo ndoto ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Baadhi ya wakimbizi na wahamiaji wanajikuta wakitumbukia katika mitego ya magenge ya uhalifu kitaifa na kimataifa; wanaowatumbukiza katika biashara ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo! Haya ni matukio ambao yanatengeneza hata mnyororo wa biashara haramu ya silaha duniani pamoja na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya! Sehemu kubwa ya waathirika hawa ni vijana wa kizazi kipya anasema Baba Mtakatifu Francisko, wanaotishiwa maisha hata wanapokuwa ugenini kwa kubandikwa majina ya watu hatari. Baba Mtakatifu anagusia pia nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo na kwamba, Kanisa linawashukuru na kuwapongeza waathirika wote waliokuwa na ujasiri wa kuzungumza na kushuhudia ukweli.

Viongozi wa Kanisa waliohusika na kashfa hii ni wachache, ikilinganishwa na idadi kubwa ya wakleri wanaojisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Hata katika madonda ya watoto wake, bado Kanisa litaendelea kuwa ni Mama na Mwalimu, tayari kuanza mapambazuko ya Pentekoste mpya! Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata katika kipindi kigumu cha giza la maisha na utume wa Kanisa, bado kuna uwezekano wa kusikia Habari Njema ya Wokovu, kwa kusoma alama za nyakati, ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa kutumia maendeleo ya teknilojia ya mawasiliano ya jamii! Kamwe, vijana wasikubali kupokwa furaha na matumaini ya maisha kwa kutafuta furaha za mpito ambazo mara nyingi zinawaachia machungu moyoni! Lengo la maisha yao, liwe ni utakatifu, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza na pale wanapojisikia kunyongo’nyea kutokana na changamoto za maisha, wamkimbilie Kristo Yesu, ili aweze kuwanyanyua tena juu na kuwaingiza katika maisha ya kijumuiya!

Papa: Christus vivit
20 November 2019, 16:34