Tafuta

Papa Francisko: Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa. Ni mahali muafaka pa uinjilishaji na utakaso! Papa Francisko: Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa. Ni mahali muafaka pa uinjilishaji na utakaso! 

Papa Francisko: Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa!

Baba Mtakatifu anasema Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Inasikitisha kuona kwamba, kuna waamini wengi ambalo hawashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa parokiani: Watafutwe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 18 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na wahudumu wa vikundi vya uinjilishaji parokiani. Amesema, utamaduni wa kukutana na watu unasaidia kuleta mabadiliko katika maisha ya watu, kwa kuwagusa kutoka katika undani wa sakafu ya maisha yao. Amempongeza Padre Piergiorgio Perini kwa kujisadaka bila ya kujibakiza katika maisha na utume wa Kipadre kwa muda wa miaka 65, wakati anamshukuru Mungu kwa kumkirimia miaka 90 tangu alipozaliwa. Wakristo wanakumbushwa kwamba wamechaguliwa na Kristo Yesu ili waende wakazae matunda na matunda yao yapate kukaa! Baada ya kuchakarika kwa muda mrefu, watu wanatamani kuona matunda ya kazi ya mikono yao, lakini, Injili inatoa mwelekeo tofauti kabisa kwa kusema “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mlioagizwa, semeni, “Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya”. Lk. 17: 10.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa daima tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili; huku wakikesha na kusali, ili Bwana wa mavuno atakapokuja awakute wakiendelea na kazi na hapo wataweza kuona matunda ya jasho lao. Ni katika muktadha huu kwamba, historia ya vikundi vya uinjilishaji parokiani inaweza kueleweka kwani hadi wakati huu, vimeenea sehemu mbali mbali za dunia, huku vikijitahidi kufuata mwongozo na dira ya Kristo Mfufuka bila ya woga wala makunyanzi licha ya matatizo na changamoto wanazokumbana nazo katika mchakato mzima wa uinjilishaji. Pale wanapojisikia kuwa ni mitume wamisionari, hapo wanapata ari na mwamko mpya, kwani wanafarijiwa na kutiwa nguvu na Roho Mtakatifu, ili kamwe wasitindikiwe katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Baba Mtakatifu anawataka wahudumu katika vikundi hivi kuhakikisha kwamba, sera na mikakati yao ya uinjilishaji inagusa na kuacha chapa katika maisha ya watu.

Adhimisho la  Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa ni kiini cha Parokia. Kimsingi, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa siku ya Bwana; Jumuiya ya waamini inapopata nafasi ya kusikiliza, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kutumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani ntendaji! Neno Parokia, linapata asili yake kutoka katika lugha ya Kigiriki yaani “παρоικια” maana yake “Ujirani”. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Inasikitisha kuona kwamba, kuna waamini wengi ambalo hawashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa parokiani.

Kumbe, kuna haja ya kuweka mbinu mkakati ya kuwaendea na kuwatafuta waamini hao, mahali wanapoishi na kufanya kazi, ili kuwapatia tena nafasi ya kukutana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao. Waamini wawe tayari kuwashirikisha wengine uzoefu na mang’amuzi yao katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji. Kila wakati waamini wanapokutana na watu watambue kwamba, hapo wanatekeleza dhamana na wajibu unaoweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu. Watu wanavutwa kwa ushuhuda wa maisha na wala si wongofu wa shuruti. Waamini wawe na ujasiri wa kuwaonjesha jirani zao Injili ya upendo, huruma na matumaini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa kutekeleza yote haya watambue kwamba, wanamtendea Kristo Yesu ambaye amejitambulisha na maskini pamoja na wahitaji mbali mbali. Wahudumu wa vikundi vya uinjilishaji parokiani wanatekeleza wajibu wao kwa njia ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; Huduma kwa maskini na wanyonge zaidi, Ibada ya Misa Takatifu pamoja na shuhuda za maisha yao zinazobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili.

Papa: parokia

 

19 November 2019, 15:22