Vatican News
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu nchini Poland kwa moyo wao wa upendo na mshikamano kwa familia ya Mungu nchini Poland. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu nchini Poland kwa moyo wao wa upendo na mshikamano kwa familia ya Mungu nchini Poland.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Mshikamano wa upendo na Sudan ya Kusini

Baba Mtakatifu anawapongeza watu wa Mungu kutoka Poland wanaosherehekea Jumapili tarehe 10 Novemba 2019, Siku ya 11 ya Mshikamano wa Upendo kwa kuunga mkono juhudi zinazotekelezwa na Shirika la Kipapa kwa ajili ya huduma kwa Makanisa hitaji. Msaada huu kwa namna ya pekee unaelekezwa Sudan ya Kusini. Mchango wa hali na mali unasaidia sana watu wanaoteseka duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano, tarehe 6 Novemba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatiacan, amewataka Wakristo kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie neema ya kujenga madaraja na wale wasioamini; daima wakiwa tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Upendo wa dhati ni ushuhuda hata kwa watu wenye shingo ngumu kama walivyokuwa wanafalsafa wa mji wa Athene. Waamini wamwombe Roho Mtakatifu nguvu na neema ya kumfahamu zaidi Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo na kweli za Kimungu! Katika shida, magumu na dhuluma mbali mbali za maisha, waamini wajitahidi kuomba neema ya kuwa ni wajenzi wa madaraja na vyombo vya: imani, huruma, mapendo na matumaini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha.

Waamini wawe tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Mfufuka; imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; ili kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anawapongeza watu wa Mungu kutoka Poland wanaosherehekea Jumapili tarehe 10 Novemba 2019, Siku ya 11 ya Mshikamano wa Upendo kwa kuunga mkono juhudi zinazotekelezwa na Shirika la Kipapa kwa ajili ya huduma kwa Makanisa hitaji. Msaada huu kwa namna ya pekee unaelekezwa Sudan ya Kusini. Mchango wa hali na mali ni muhimu sana kwa ajili ya kuwasaidia wale wote wanaoteseka kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu, sehemu mbali mbali za dunia! Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, Mwezi Novemba, umetengwa maalum na Mama Kanisa kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwambea waamini marehemu wote waliolala kwenye usingizi wa amani, wakiwa na matumaini ya maisha na uzima wa milele.

Kwa kuongozwa na imani ya umoja katika mambo matakatifu, waamini wanahimizwa kuwakumbuka ndugu, jamaa na marafiki zao kwa kuomba nia za Misa takatifu katika maeneo yao. Kumbu kumbu ya waamini marehemu wote iwe ni fursa kwa waamini kutafakari maana ya maisha yao hapa duniani na kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kumwilishwa katika sadaka na huduma kwa Mungu na jirani!

Papa: Sudan ya Kusini
06 November 2019, 14:34