Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na mauaji ya kidini na kikabila yanayoendelea kujitokeza nchini Ethiopia. Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na mauaji ya kidini na kikabila yanayoendelea kujitokeza nchini Ethiopia. 

Papa asikitishwa na mauaji ya kidini na kikabila nchini Ethiopia

papa Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, aliyaelekeza macho yake Barani Afrika kutokana na dhuluma na nyanyaso za kidini ambazo Wakristo wa Kanisa la Kiorthodox la Tewahedo nchini Ethiopia wanaendelea kukumbana nazo kila kukicha! Papa ameonesha uwepo wa karibu na mshikamano wa upendo kwa Patriaki Abuna Matthias wa Kanisa la Kiorthodox la Tewahedo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 3 Novemba 2019 aliyaelekeza macho yake Barani Afrika kutokana na dhuluma na nyanyaso za kidini ambazo Wakristo wa Kanisa la Kiorthodox la Tewahedo nchini Ethiopia wanaendelea kukumbana nazo kila kukicha! Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuonesha uwepo wa karibu na mshikamano wa upendo kwa Patriaki Abuna Matthias wa Kanisa la Kiorthodox la Tewahedo. Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema waliokuwepo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kusali kwa pamoja ili kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo hao nchini Ethiopia.

Itakumbukwa kwamba, Wakristo wa Kanisa la Kiorthodox la Tewahedo nchini Ethiopia ni sawa na asilimia 40% ya idadi ya wananchi wote wa Ethiopia wanaokadiriwa kufikia milioni 110. Viongozi mbali mbali kutoka Jumuiya ya Kimataifa wanaendelea kulaani na kushutumu machafuko ya kidini na kikabila ambayo yamepelekea watu zaidi ya 70 kupoteza maisha. Ghasia zimeendelea kujitokeza mjini Addis Ababa na karibu na Jimbo la Oromia. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu milioni mbili ambao hawana makazi maalum nchini Ethiopia kutokana na machafuko na hali tete ya kidini na kikabila. Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema, kuna njama ya kutaka kugeuza machafuko haya ya kidini na kikabila kuwa ni janga na maafa ya kitaifa kwa kuchoma nyumba za ibada na waamini wake, hayo yamebanishwa na Kamanda Kefyalew Tefer, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Oromia.

Papa: Ethiopia
03 November 2019, 10:25