Papa Francisko anatarajiwa kuchapisha waraka wa kitume kuhusu umuhimu wa Pango la Noeli katika maisha ya Wakristo! Papa Francisko anatarajiwa kuchapisha waraka wa kitume kuhusu umuhimu wa Pango la Noeli katika maisha ya Wakristo! 

Papa Francisko: Maana na umuhimu wa Pango la Noeli kwa Wakristo!

Kanisa litafungua Mwaka Mpya wa Kanisa kwa kuadhimisha Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio. Papa anasema, atatumia fursa hii kwenda kutembelea katika Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio, Rieti, Mkoani Lazio, Italia, ili kusali kwenye Pango la kwanza kabisa la Noeli lililotengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi ili kuonesha maana na umuhimu wake kwa Wakristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 27 Novemba 2019 amesema, Jumapili ijayo tarehe 1 Desemba 2019, Kanisa litafungua Mwaka Mpya wa Kanisa kwa kuadhimisha Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio. Baba Mtakatifu anasema, atatumia fursa hii kwenda kutembelea katika Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio, Rieti, Mkoani Lazio, nchini Italia, ili kusali kwenye Pango la kwanza kabisa la Noeli lililotengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi. Atatumia nafasi hii kuwaandikia Waraka wa kitume waamini na watu wote wenye mapenzi mema maana ya Pango la Noeli katika maisha ya Wakristo. Baba Mtakatifu amewatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema maandalizi mema ya maisha ya kiroho na kimwili, ili kuweza kuingia kikamilifu katika Kipindi cha Majilio, huku wakiwa na moyo unaosheheni matumaini na furaha, kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Askofu Domenico Pompili wa Jimbo Katoliki la Rieti anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa upendeleo wa pekee aliouonesha kwa ajili ya kufanya hija ya kichungaji kwenye Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio. Haya ni Madhabahu yenye utajiri na amana kubwa ya historia na maisha ya kiroho mintarafu Fumbo la Umwilisho. Ni mahali patakatifu, penye ukimya unaomwezesha mwamini kusali na kutafakari matendo makuu ya Mungu katika historia nzima ya ukombozi. Hapa waamini wanaonja na kugusa tasaufi  ya Wafranciskani mintarafu: ufukara na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, unavyomwilishwa katika uhalisia na ubora wake. Kwa mara ya kwanza Mtakatifu Francisko wa Assisi alitengeneza Pango la Noeli huko Greccio kunako mwaka 1223 na huo ukawa ni mwanzo wa Mapokeo ya Kanisa kutengeneza Pango la Noeli wakati wa Sherehe za Noeli kila mwaka Jimbo Katoliki la Rieti linajiandaa pia kuadhimisha kumbu kumbu ya Katiba ya Wafranciskani ya Mwaka 1223.

Uwepo na ushuhuda wa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na vipaumbele vyake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro yaani: Amani, Maskini na Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote ni changamoto na mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Fumbo la Umwilisho ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi memwa kujiandaa kumpokea Mtoto Yesu atakayezaliwa kwenye Pango la kulishia wanyama, kwa sababu wazazi wake hawakupata nafasi kwenye nyumba ya wageni! Hii ni mara ya pili kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio, Rieti, Mkoani Lazio, nchini Italia. Mara ya kwanza, Baba Mtakatifu alitembelea Madhabahu haya kwa faragha tarehe 4 Januari 2016, Baba Mtakatifu akapata nafasi ya kusali pamoja na vijana waliokuwa wamekusanyika kwenye Madhabahu haya. Kwa lugha ya Kilatini “Presepium” yaani “Pango la Noeli” lina utajiri na amana kubwa katika maisha ya waamini wanapotafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho.

Pango la Noeli ni alama ya mahali ambapo Mtoto Yesu alizaliwa katika hali ya umaskini, ili kuonesha utajiri wa imani katika Fumbo la Umwilisho. Kipindi cha Majilio na Noeli, kuna umati mkubwa wa waamini wanaotembelea kwenye Madhabahu haya, ili kuona jinsi ambavyo “Mwenyezi Mungu alivyoamua kujifunua kama Mtoto Mdogo”, ili kuwaonjesha na kuwashirikisha waja wake upendo na huruma isiyokuwa kifani. Pango la Noeli limekuwa ni sehemu ya utajiri wa tamaduni mbali mbali duniani zinazoendelea kuguswa na Fumbo la Umwilisho.

Papa: Pango la Noeli
29 November 2019, 17:30