Kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Caritas Romana: ushuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Caritas Romana: ushuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. 

Papa Francisko: Kumbu kumbu ya Miaka 40 Caritas Romana: Maskini

Caritas Romana imewahi kutembelewa na Mt. Yohane Paulo II kunako mwaka 1992, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI mwaka 2010 katika maadhimisho ya Mwaka wa Mapambano dhidi ya Umaskini Barani Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 18 Desemba 2015 alifungua Lango la Huruma ya Mungu kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jimbo kuu la Roma linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Msaada la Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Roma, Caritas Romana na Don Luigi di Liegro kunako mwaka 1979 na baada ya huduma kwa maskini, akafariki dunia tarehe 12 Oktoba 1997. Katika maisha yake, ni kiongozi aliyethubutu kusimama kidete kuomba nafasi na haki kwa maskini waliokuwa wananyanyaswa utu na heshima yao mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 29 Novemba 2019 majira ya jioni, anatarajiwa kutembelea: Kituo cha Tiba kwa Magonjwa ya Kinywa “Centro Odontoiatrico”, ambamo kuna madaktari 40 wanatoa huduma kwa wagonjwa wa meno zaidi ya 350 na wengi wao ni watoto wagonjwa wanaotoka kwenye familia zenye kipato cha chini kiasi cha kutoweza kumudu gharama za tiba ya meno. Nyumba ya Maskini ya “Santa Giacinta”, inatoa hifadhi na malazi kwa watu 82 ambao wana matatizo ya afya na hali ngumu ya uchumi.

Kituo cha Mshikamano “Emporio della Solidarietà” hii “Supermarket iliyoanzishwa kunako mwaka 2008 kwa ajili ya kutoa huduma ya mahitaji msingi kwa maskini na wenye shida kutoka Roma. Hiki ni kituo kinachowahudumia: wakimbizi na wahamiaji; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Mwishoni Baba Mtakatifu atatembelea Bwalo la Chakula kwa ajili ya maskini wa mji wa Roma. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Caritas, maskini wa Roma pamoja na watu wa kujitolea, wanao endelea kujisadaka kila kukicha kwa ajili ya kuwaonjesha maskini ushuhuda wa Injili ya upendo na mshikamano. Padre Benoni Ambarus, Mkurugenzi wa Caritas Romana anasema, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Makao makuu ya Caritas Romana ni sehemu ya maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 40 ya Caritas Romana.

Huu ni muda wa kumshukuru na kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuwateuwa na kuwatuma kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Caritas Romana imewahi kutembelewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1992, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI mwaka 2010 katika maadhimisho ya Mwaka wa Mapambano dhidi ya Umaskini Barani Ulaya. Bila shaka, itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 18 Desemba 2015 alifungua Lango la Huruma ya Mungu kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Hawa ni walengwa wa kwanza wa mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa.

Katika muktadha huu mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni: Ufahamu wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani sanjari na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha utandawazi wa mshikamano wa upendo na katika maisha ya kiroho dhidi ya sera na mikakati ya kiuchumi inayowatenga na kuwanyanyasa maskini.  Kwa sasa tofauti kati ya watu inakuwa ni chanzo cha kinzani, uhasama na vita. Lakini, ikumbukwe kwamba, dunia inahitaji wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na Uso wa huruma; wajenzi na vyombo vya amani duniani; manabii wa huruma na wasamaria wema wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja wa binadamu, kati ya watu wa mataifa, familia na tamaduni zao.

Kwa upande wake, Kardinali Angelo De Donatis Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, anawataka watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, kwa kuwasikiliza na kuwashirikisha katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kugundua mifumo mipya umaskini katika ulimwengu mamboleo. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa Mataifa. Chachu ya huduma ya upendo ipate chimbuko lake ndani ya: familia na Jumuiya za Kikristo. Hakuna huduma mbadala ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wakati huo huo, Padre Benoni Ambarus, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Msaada la Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Roma, Caritas Romana amewashukuru watu wa kujitolea pamoja na Parokia 337 zinazoendelea kutoa huduma kwa maskini na wahitaji zaidi.

Kuna hosteli 52 zinazotoa huduma ya chakula na malazi kwa maskini; wakimbizi na wahamiaji; wagonjwa na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kuna watu wanaoelemewa na upweke hasi, kumbe, kwanza kabisa wanapaswa kusikilizwa kwa makini; kupewa chakula, malazi na huduma ya afya. Wazee na wagonjwa wa muda mrefu wanapaswa kuhudumiwa kikamilifu. Caritas Romana inataka kuendelea kujizatiti katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa sababu wao ni shule makini ya huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena anapenda kuwaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwenye shule ya maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Hawa ni watu wa kawaida wanaopaswa kuonjeshwa upendo na kuthamini utu wao. Kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humo kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho.

Wasanii wasaidie kuhamaisha tunu msingi za maisha  kama vile: upendo kwa Mungu na jirani; umoja na mshikamano wa kidugu. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwamba, wao ni shule makini kwa vijana wa kizazi kipya kuhusu umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea ustawi na mafao ya wengi. Maskini ni kielelezo cha Kristo kati ya watu wake. Jimbo kuu la Roma limekuwa ni kielelezo cha upendo na mshikamano kati ya watu. Hapa Kanisa linajivunia kuwa na viongozi ambao wamejisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, daima wakitenda kama Wasamaria wema kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Laurenti, Shemasi na shahidi pamoja na Padre Luigi Di Liegro, muasisi wa Shirika la msaada  Roma, Caritas Romana bila kuwasahau watu wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia maskini ndani na nje ya Roma. Katika shule ya upendo, watu wanatafuta faraja, mahusiano, utu na  heshima ya binadamu na kwa njia hii, waamini wanaweza kujifunza kutoka kwa maskini kwa kuwakaribisha, kuwasikiliza, kuwakirimia na kuwahudumia kwa upendo na nidhamu ya hali ya juu.

Caruitas Romana

 

 

28 November 2019, 17:48