Vatican News
Papa Francisko, Jumamosi tarehe 9 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano la Tatu la Muziki Mtakatifu Kimataifa. Papa Francisko, Jumamosi tarehe 9 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano la Tatu la Muziki Mtakatifu Kimataifa.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Kanisa, Muziki na Watafsiri wake katika Liturujia

Mkristo anao wajibu wa kutafsiri mapenzi ya Mungu katika maisha yake kwa kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Wimbo huu ndio Injili ambayo imetafsiriwa na Kanisa katika hija ya maisha yake hapa duniani. Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa katika utenzi wake wa “Magnificat” wakati ambapo watakatifu wametafsiri mapenzi ya Mungu kwa njia ya maisha na utume wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 9 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano la Tatu la Muziki Mtakatifu Kimataifa, lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Kanisa, Muziki na Watafsiri wake”: Umuhimu wa Majadiliano”. Kongamano limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa kushirikiana na Taasisi ya Kipapa ya Liturujia katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselm, kilichoko mjini Roma. Kongamano hili pamoja na mambo mengine, limekuwa likipania kupyaisha: Mang’amuzi ya Injili, maisha ya Kiliturujia, huduma kwa Kanisa na kwa tamaduni. Baba Mtakatifu amewataka wale waliopewa dhamana na wajibu wa kutunga na kutafsiri muziki mtakatifu ni kuhakikisha kwamba, waamini wanazifahamu tungo hizi, ili waweze kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada na Liturujia ya Kanisa. Hii ni kazi inayopaswa kutekelezwa kwa unyenyekevu wa hali ya juu kabisa, ili yule anayetasiri kazi hii aweze kuguswa kutoka katika undani wake kwa kuzingatia pia weledi katika kazi, ili hatimaye, kuweza kuwaonjesha watu uzuri wa muziki mtakatifu.

Baba Mtakatifu anawataka watasiri wa muziki mtakatifu kuwa makini sana na wabunifu katika huduma ya sanaa inayoburudisha roho za watu sanjari na kutoa huduma kwenye jumuiya. Maagizo haya ni muhimu sana ikiwa kama mhusika anafanya kazi hii kwa ajili ya huduma ya kiliturujia. Watafsiri wa muziki mtakatifu wana uhusiano wa karibu sana na wasomi wa Maandiko Matakatifu pamoja na watangazaji wa Neno la Mungu bila kuwasahau watu wanaosoma na kutafsiri alama za nyakati; kwa kuwa makini na wakweli katika majadiliano. Kimsingi, kila Mkristo anapaswa kutambua kwamba, anao wajibu wa kutafsiri mapenzi ya Mungu katika maisha yake kwa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Wimbo huu ndio Injili ambayo imetafsiriwa na Kanisa katika hija ya maisha yake hapa duniani. Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa katika utenzi wake wa “Magnificat” wakati ambapo watakatifu wametafsiri mapenzi ya Mungu kwa njia ya maisha na utume wao.

Mtakatifu Paulo VI anasema, utume wa Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ili iweze kuwafikia na kueleweka kwa wengi, kwa kusaidia kufanya mambo yatembee hata yale yasio onekana kama alivyo kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe, yaweze kuonekana na kuwagusa watu. Watafsiri kama ilivyo kwa wasanii wanapaswa kutumia milango yao ya fahamu kufikisha ujumbe unaokusudiwa, ili kwa njia hii, kama sehemu ya “visakramenti” iweze kuonekana katika uzuri wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, wasanii, watafsiri na kwa upande wa muziki mtakatifu wasikilizaji, wote wanayo kiu ya kutaka kufahamu uzuri wa muziki na kwamba, sanaa itumike kwa ajili ya kutambua na kukiri ukuu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Hii ndio kiu kubwa ya walimwengu wa nyakati hizi, pengine kuliko hata ilivyokuwa kwa nyakati zilizopita. Tafsiri ya ukweli huu ni muhimu sana. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru wadau mbali mbali wanaoendelea kujisadaka na kujitosa kwa ajili ya kusoma na kujifunza muziki, lakini zaidi muziki wa liturujia, ili siku kwa siku, waendelee kuwa ni watafsiri wazuri wa Injili pamoja na uzuri ambao Mwenyezi Mungu ameufunua kwa njia ya Kristo Yesu pamoja na sifa na utukufu unaotolewa na binadamu kama watoto wa Mungu.

Papa: Muziki

 

 

09 November 2019, 14:26