Vatican News
Tume ya Taalimungu Kimataifa Mwaka 2019 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na Mtakatifu Paulo VI: matunda ya Mtaguso II wa Vatican na Sinodi za Maaskofu Tume ya Taalimungu Kimataifa Mwaka 2019 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na Mtakatifu Paulo VI: matunda ya Mtaguso II wa Vatican na Sinodi za Maaskofu  (ANSA)

Papa Francisko: Jubilei ya Miaka 50 ya Tume ya Taalimungu Kimataifa

Tume ya Taalimungu Kimataifa iliyoanzishwa na Mtakatifu Paulo VI ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na Sinodi za Maaskofu. Tume hii kwa mwaka 2019 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake: Imechangia sana kuhusu: Dhana ya Sinodi; Sakramenti za Kanisa, Haki Msingi za Binadamu, Uhuru wa Kuabudu na Umoja wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya Taalimungu Kimataifa katika kipindi cha Mwaka 2019 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na Mtakatifu Paulo VI, kama sehemu ya matunda ya maadhimisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatican, ili kuwasaidia viongozi wa Kanisa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao kama sehemu ya Mamlaka funzi ya Kanisa. Jubilei hii ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa historia hii makini katika maisha na utume wa Kanisa. Wanataalimungu walioteuliwa kuunda tume hii, wamekuwa ni mashuhuda wa malezi, majiundo na tafakari makini kutokana na mchango wao uliwezesha kuchapishwa kwa nyaraka nyingi ambazo kwa sasa ni msaada mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni mchango muhimu sana wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, unaokazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”.

Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo. Inahimiza umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa kama chemchemi ya neema na baraka za Mungu katika hija ya maisha yao sanjari na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Waamini wanapaswa kukuza ari na mwamko wa kimisionari tayari kuyachachua malimwengu kwa utakatifu wa maisha kama ushuhuda na kielelezo cha imani tendaji! Huu ni ushuhuda wa Fumbo la umoja linalopata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, chemchemi ya furaha, imani na matumaini wanayopaswa kushirikishwa hata vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anakaza kusema, dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni kati ya vipaumbele vya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa ufupi, dhana ya Sinodi ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kielelezo cha umoja na mshikamano katika utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa. Tume iliangalia: dhana, historia, taalilimungu na mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa katika kukuza na kudumisha urika wa Maaskofu na utekelezaji wake katika ngazi mbali mbali za maisha ya Kanisa bila kubeza taasisi za Kanisa na uwiano wake katika maisha ya kiroho. Uhuru wa kuabudu na kidini ni nguzo ya haki msingi za binadamu; ni kiiini cha Habari Njema ya Wokovu na ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Uhuru wa kuabudu na kidini unaweza kusaidia kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Hii ni chachu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa na kwamba, ukweli na uwazi ni kanuni msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene.

Kumbe, hapa kuna haja ya kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Haya ni mambo msingi ambayo yamepewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 29 Novemba 2019 katika hotuba yake kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Taalimungu Kimataifa. Uhuru wa kidini na kuabudu unakazia kanuni maadili na utu wema; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kuhakikisha kwamba, vijana wa kizazi kipya wanafundwa barabara ili waweze kuheshimu na kuthamini amana na utajiri huu katika maisha ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasistiza kwamba kuna uhusiano wa dhati kabisa kati ya: Imani na Sakramenti za Kanisa; mambo yanayotekelezwa katika mikakati ya shughuli za kichungaji, ingawa hali inatofautiana kutoka katika nchi moja hadi nchi nyingine. Kuna mwelekeo potofu wa kutaka kuondoa imani katika Sakramenti za Kanisa, na wengine wanashindwa kuona uhusiano kati ya Sakramenti na Kanisa.

Baadhi ya waamini wanataka kupokea Sakramenti za Kanisa hata kama hawana imani, kwani mambo haya yanakuwa ni kama mtindo wa maisha kama inavyotokea kwa baadhi ya waamini kutaka kufunga Ndoa Kanisani hata kama hawana imani na maamuzi magumu wanayofanya. Kuna waamini wanaotaka kupata Ibada ya maziko Kanisani hata kama hawana imani katika ufufuko wa wafu na uzima wa milele; mambo yanayofumbatwa katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Mambo yote haya yanaweka mazingira magumu na tatanishi kwa viongozi wa Kanisa. Kumbe, kuna haja ya kukazia kwamba, kuna uhusiano wa dhati kati ya Imani na Sakramenti za Kanisa na kwamba, imani ni muhimu sana katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kwani hapa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anakutana na mwanadamu dhaifu na mdhambi.

Jubilei ya Miaka 50 ya maisha ya Tume ya Taalimungu Kimataifa ni fursa nyingine tena ya kutaka kukazia na kuimarisha mahusiano na mafungamano kati ya Mamlaka Funzi ya Kanisa na wanataalimungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuimarisha utume wa Kanisa ambao ni uinjilishaji na utamadunisho unaofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi. Wanataalimungu wanaalikwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa mwanga wa Injili utakaowasaidia waamini kufarijika katika nyoyo zao, wakiunganishwa katika upendo ili wapate utajiri wote wa kufahamu na kujua kabisa siri ya Mungu yaani, Kristo, ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika. Wasaidie kutafsiri imani ya watu wa Mungu katika maisha, ili waweze kulipenda Kanisa, huku wakisindikizwa na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu, kwa hakika wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Tume ya Taalimungu Kimataifa iwe ni fursa ya kuunganisha nguvu za wakleri, watawa na waamini walei wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya kuchangia katika ukuaji wa taalimungu katika mwanga wa Injili unaofumbata maisha ya kiroho, umoja na mshikamano wa Kanisa, ili kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya Kanisa  yaani “ In dulcedine societatis quaerere veritate” yaani “ katika unyenyekevu na udugu ili kutafuta ukweli” Taalimungu inatekelezwa kwa kushirikiana pamoja na kuheshimiana na wengine. Wawe ni mashuhuda amini wa imani kwa kuondokana na mawazo ya taalimungu yanayojikita katika unafsia “Subjectivism”. Taalimungu iwe ni sehemu ya maisha na utume wao ndani ya Kanisa, kwani waamini wakikosa mwelekeo wa kitaalimungu wanapoteza pia dira na mwelekeo sahihi wa imani.

Papa: Tume 50 Yrs

 

29 November 2019, 17:48