Tafuta

Papa Francisko anawapongeza viongozi wa Manispaa na Jimbo Katoliki la San Severo, Italia kwa kuwekeana saini makubaliano yatakayosaidia kulinda utu na haki za wafanyakazi wa mashambani. Papa Francisko anawapongeza viongozi wa Manispaa na Jimbo Katoliki la San Severo, Italia kwa kuwekeana saini makubaliano yatakayosaidia kulinda utu na haki za wafanyakazi wa mashambani. 

Papa Francisko: Juhudi za kutetea: utu na haki za wahamiaji Italia.

Papa Francisko anawashukuru viongozi wa Jimbo na Manispaa ya San Severo kwa kuwekeana saini mkataba unaopania kulinda utu na haki msingi za wafanyakazi wa mashambani, ambao wengi wao ni kutoka Barani Afrika ili kupata vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini Italia. Vibali hivi vitakuwa vinatolewa na Parokia Jimboni humo na hatimaye, kusajiliwa na Manispaa ya San Severo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 3 Novemba 2019 amewashukuru viongozi wa Manispaa pamoja na Jimbo Katoliki la San Severo lililoko mkoani Puglia, Kusini mwa Italia, kwa kuwekeana saini makubaliano yatakayowawezesha wafanyakazi wa mashambani, ambao wengi wao ni kutoka Barani Afrika kuweza kupata vibali vya kuishi nchini Italia. Vibali hivi vitakuwa vinatolewa na Parokia Jimboni humo na hatimaye, kusajiliwa na Manispaa ya San Severo. Mkataba huu ulitiwa saini kati ya taasisi hizi mbili tarehe 28 Oktoba 2019 na kushuhudiwa na Kardinali Konrad Krajewski, mtunzaji mkuu wa sadaka ya kitume kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, makubaliano haya yanafikiwa kwa ajili ya kulinda, utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi wa mashambani huko Kusini mwa Italia.

Hii ni fursa kwa wafanyakazi mashambani kupata vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini Italia. Hii ni sehemu ya mchakato na juhudi za Kanisa kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi wa mashambani ambao wengi wao ni wahamiaji na wakimbizi zinalindwa na kudumishwa. Hii ni hatua kubwa ya kuondokana na nyanyaso na dhuluma walizokuwa wanatendewa wafanyakazi wa mashambani kwa kufanya kazi za “suluba kwa mshahara kiduchu” na katika mazingira magumu na hatarishi. Kwa makubaliano haya, wafanyakazi wa mashambani waliokuwa wanafanya kazi kwa vificho sasa wanaweza kutambulikana na kupewa haki zao msingi katika masuala ya kazi na huduma za kijamii. Sheria mpya za wahamiaji zilizokuwa zimepitishwa hivi karibuni na Serikali ya Italia, zilikuwa zinazuia wakimbizi na wahamiaji kujiandisha katika Manispaa kwa ajili ya kupata vibali vya kuishi, kufanya kazi pamoja na kupatia huduma za kijamii.

Bila nyaraka hizi anasema Kardinali Konrad Krajewski ni vigumu sana kufanya mkataba wa kazi, kupata matibabu au hata nyumba ya kupanga. Mkataba huu ni sehemu ya mchakato unaopania kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuwasaidia watu wanaotaka kujipatia riziki yao kwa njia halali na kwa malipo halali badala ya kuendelea na mfumo uliokuwa unawaneemesha baadhi ya wajanja wachache katika jamii kwa jasho la damu kutoka kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta maisha bora zaidi nchini Italia. Baba Mtakatifu anapenda kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu, ili kufahamiana, kusaidiana, kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini wawe mstari wa mbele kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji ambao kutokana na hali yao tete wanajikuta wakitumbukizwa kwenye kazi za suluba, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake na hata wakati mwingine kwenye utumwa mamboleo!

Papa: Pongezi

 

04 November 2019, 10:03