Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kuboresha huduma za shughuli za kichungaji kwa wafungwa magerezani, ili kuwajengea matumaini mapya! Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kuboresha huduma za shughuli za kichungaji kwa wafungwa magerezani, ili kuwajengea matumaini mapya! 

Papa Francisko: Huduma za shughuli za kichungaji kwa wafungwa!

Papa Francisko amegusia: Matatizo yanayowakumba wafunga magerezani; umuhimu wa kuwa na mwono mpya kuhusu wafungwa na kwamba, huduma kwa wafungwa ni sehemu ya matendo ya huruma kimwili! Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu ndilo ambalo limekabidhiwa dhamana ya kuratibu shughuli za kichungaji kwa ajili ya wafungwa magerezani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu pamoja na Monsinyo Segundo Tejado Munoz, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza, tarehe 7 Novemba 2019 wamezindua mkutano wa kimataifa wa waratibu wa kitaifa, kikanda na kimkoa wanaohusika na shughuli za kichungaji kwa ajili ya wafungwa magerezani. Mkutano umeongozwa na kauli mbiu “Maendeleo fungamani na shughuli za kichungaji za Kikatoliki Magerezani”. Wajumbe wamejadili kuhusu: matatizo na changamoto katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji na kijamii magerezani. Changamoto hizi zimejadiliwa pia kwa kuzingatia maeneo ya kijiografia yaani: Bara la Afrika, Amerika, Asia na Bara la Ulaya na Oceania. Wajumbe hawa, Ijumaa, tarehe 8 Novemba 2019 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.

Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: matatizo yanayowakumba wafunga magerezani, umuhimu wa kuwa na mwono mpya kuhusu wafungwa na kwamba, huduma kwa wafungwa ni sehemu ya matendo ya huruma kimwili! Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu ndilo ambalo limekabidhiwa dhamana ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wafungwa magerezani, ili kuonesha wasi wasi na ukaribu wa Mama Kanisa kwa wafungwa wanaoteseka magerezani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni dhamana na wajibu wa Kanisa zima kama sehemu ya utekelezaji wa utume wake unaomwilisha matendo ya huruma katika uhalisia wa maisha ya watu. Wakati wa hukumu ya mwisho, watu watahukumiwa kadiri walivyowatendea ndugu zake walio wadogo, na kwa kufanya vile, walimtendea Kristo Yesu mwenyewe. (Rej. Mt. 25:40) Kristo Yesu anajitambulisha kuwa kati ya watu wenye njaa, kiu, wageni, watu walio uchi, wagonjwa na wale walioko kifungoni.

Baba Mtakatifu anasema taswira inayotolewa na magereza sehemu mbali mbali za dunia inaonesha ukweli wa jamii ambamo uchoyo, ubinafsi na utandawazi wa kutoguswa na mahangaiko ya jirani vinatawala. Kuna maamuzi ambayo yamefanywa kisheria lakini yanakiuka utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kujidai kukuza na kutaka kudumisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Matokeo yake ni watu kutengwa na kutupwa magerezani kama suluhu ya matatizo mbali mbali yanayoisonga jamii. Lakini ikumbukwe kwamba, kuna kiasi kikubwa cha rasilimali na utajiri wa nchi unaotumika kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa magerezani, ikilinganishwa na kiasi cha fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuchochea kasi ya maendeleo fungamani ya binadamu, ambayo yangewezesha idadi kubwa ya wafungwa kupata kazi na kipato halali badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya uvunjaji wa sheria.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni rahisi sana kufumbia macho umuhimu wa elimu na malezi makini kwa jamii, sanjari na kushindwa kuona ukweli halisi wa matatizo na ukosefu wa haki na hivyo suluhu ya haraka inayoweza kupatikana ni ujenzi wa magereza, ili “kuwashikisha adabu wale wote wanaovunja sheria za nchi”. Umefika wakati wa kutoa msukumo wa pekee kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu kwa raia wote. Kwa bahati mbaya, magereza mengi yameshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuweza kutoa mafunzo bora zaidi, ili wafungwa wanapomaliza adhabu zao na kutoka magerezani waweze kuwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani. Ni ukweli usioweza kufumbiwa macho kwamba, kuna uhaba mkubwa wa rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na changamoto za kijamii, kisaikolojia na kifamilia wanazokabiliana nazo wafungwa magerezani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, magereza yamegeuka kuwa ni mahali hatari sana, ambapo utu na heshima ya binadamu vinasiginwa. Mafunzo makini kwa wafungwa yanaanza pale ambapo wafungwa wanapewa fursa ya kushiriki katika mchakato wa maendeleo, wanapopewa elimu makini na kufanyishwa kazi zenye staha. Yote haya lazima pia yazingatie huduma bora za afya kwa wafungwa pamoja na kuunda mazingira ambayo, wafungwa wataweza pia kushirikiana kwa karibu na raia wengine. Jamii inapaswa kuwa na mwelekeo tofauti sana kwa wafungwa magerezani, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali, ili kuboresha maisha yao, kama sehemu ya faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa bahati mbaya sana, wafungwa wamekuwa wakiangaliwa kwa “jicho la kengeza” kiasi kwamba, si rahisi sana kuthamini utu na heshima yao. Wafungwa waonjeshwe matumaini na kupewa tena fursa ya kufanya kazi, ili kujipatia mahitaji yao msingi. Pale ambapo wafungwa baada ya kumaliza adhabu yao wanashindwa kutambuliwa utu na heshima yao, wanajikuta wakiwa kwenye majaribu makubwa kati ya kutafuta fursa za kazi, kutenda uhalifu pamoja na kujenga mazingira yasiokuwa salama. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya waamini kuwaonjesha wafungwa huruma na mapendo, dhamana na utume unaopaswa kutekelezwa na Makanisa mahalia. Kila mwamini awe ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa wafungwa, ili kuiwezesha jamii kukita mizizi yake katika misingi ya haki na amani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni nyenzo thabiti katika mchakato wa huduma kwa wafungwa magerezani. Huu ni mchakato unaowawezesha watu wa Mungu kutoa huduma kwa wafungwa na hivyo kujenga ndani mwao matumaini. Waamini waendelee kumtambua Kristo Yesu anayejitambulisha kati ya wafungwa magerezani. Baba Mtakatifu anawapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wafungwa pamoja na familia zao, hasa katika kipindi hiki kigumu cha majaribio. Baba Mtakatifu mwishoni anawaombea heri na baraka wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafungwa magerezani sehemu mbali mbali za dunia, kwani kwa kufanya hivi, wanaendeleza utume ambao Kristo Yesu ameliachia Kanisa lake. Mwishoni mwa maisha yao hapa dunia, wataweza kusikia “Njooni mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu”. Mt. 25:35.

Papa: Huduma kwa Wafungwa

 

08 November 2019, 16:58