Papa Francisko: Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu: Ni chachu ya majadiliano ya kidini Papa Francisko: Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu: Ni chachu ya majadiliano ya kidini  

Papa Francisko: Hati ya Udugu wa Kibinadamu: Amani na Utulivu!

Papa Francisko anasema majadiliano ya kidini si alama ya udhaifu, bali ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Majadiliano ya kidini hayana mbadala, kwani waamini wa dini zote wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujenga utamaduni na madaraja ya kuwakutanisha watu! Majadiliano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anasema majadiliano ya kidini si alama ya udhaifu, bali ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Majadiliano ya kidini hayana mbadala, kwani waamini wa dini zote wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha utamaduni wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, ili hatimaye, familia ya binadamu iweze kukua na kukomaa katika mchakato wa upatanisho, kwa kuwakirimia watu matumaini yanayobubujika kutoka katika huduma. Dini mbali mbali zina uwezo wa kujenga utamaduni wa kuwakutanisha watu ili kujenga na kuimarisha umoja. Hati hii ni kikolezo cha ujenzi wa misingi ya usawa, haki, amani na maridhiano duniani.

Udugu wa kibinadamu unavuka mipaka ya kisiasa na kijiografia. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 18 Novemba 2019 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkutano wa Majadiliano ya Kidini ulioandaliwa na Taasisi ya Majadiliano ya Kidini kutoka Buenos Aires kwa kushirikiana na Ubalozi wa Argentina mjini Vatican kwa njia ya ufadhili wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kushikamana ili kulinda na kuendeleza mazingira nyumba ya wote; kudumisha haki msingi za binadamu; kwa kutoa majibu muafaka dhidi ya vita, kinzani na migogoro sehemu mbali mbali za dunia. Waamini na watu wenye mapenzi mema wakishirikiana kwa dhati wanaweza kukomesha pia vita, rushwa na ufisadi; kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; kwa kubainisha na kutekeleza sera na mikakati ya uchumi fungamani pamoja na kuwakirimia watu wa Mungu matumaini katika hija ya maisha yao.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu inakazia pamoja na mambo mengine, ujenzi wa utamaduni wa majadiliano ya kidini; umuhimu wa waamini wa dini mbali mbali kufahamiana, ili kushirikiana na kushikamana, kwa kutambua na kuheshimu tofauti zao msingi. Udugu wa kibinadamu ni sehemu ya utu wa mwanadamu unaowasukuma kusumbukiana katika maisha anasema Baba Mtakatifu Francisko. Udugu huu unapaswa kusimikwa katika matendo, kwa kuondokana na vizingiti vinavyowatenganisha watu kwa misingi ya udini pamoja na vita vya kidini. Hii ni changamoto ya kushikamana ili kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Ikumbukwe kwamba, majadiliano ya kidini yanapata chimbuko lake katika majadiliano kati ya Mungu na waja wake.

Waamini wa dini mbali mbali hawana budi "kufyekelea" mbali misimamo mikali ya kidini na kiimani ambayo imekuwa ni chanzo cha maafa na mahangaiko ya watu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu itaendelea kupokelewa kwa mikono miwili na Jumuiya ya Kimataifa, ili kujenga jamii stahimilivu inayosimikwa katika amani, kwa kushirikiana na kushikamana kwa dhati katika huduma kwa watu wa Mungu. 

Papa: hati ya Udugu
19 November 2019, 15:00